The Chant of Savant

Friday 27 March 2009

Kweli hii imepinda, eti turudi na matrekta?


JUZI sikulala kutokana na upupu, sijui upuuzi, sijui pwenti, sijui. Si huyu jamaa wa Mizengwe iliyopinda ambaye hivi karibuni nusu tumnyotoe roho kwa kudai tuwafinishi wanaodedisha matupinkele!

Una habari? Jamaa anaaza kuwa Mpayukaji kama Joe Kamba au Joni Chilingati. Eti anasema tuliojaliwa kukimbia usanii, ufisi, ufisadi na ujambazi mbuzi wa Bongolala tukaishia majuu, tukiamua kutia timu, tuje na matrekta badala ya mishangingi na malaptopu!

Hivi huyu jamaa ana akili nzuri kweli? Kwa nini haya asimwambie Njaa Kaya na Bi Mkubwa wanaomaliza njuluku zenu kwa kuzunguka dunia ili Bi Mkubwa atoe ushamba na kufanya shopping? Hawa kweli wakiamua kila tripu warudi na matrekta si haba, nchi itajaa na kufurika.

Kwanza, wanazo njuluku za bure wanazochota kwenye kodi ya walevi. Pili, wao ndio sera zao zimeshindwa. Maana, walituahidi maisha bora kwa wote tusijue wote ni wao na si sisi!

Viumbe wengine hawana hata huruma. Yaani tunavyosotea gamba (passport) ili kukitoa huku Magabacholi na Wasomali wakiuziwa bure na watu wale wale tunaowalipa njuluku zetu, siwezi kufanya kosa hili msee wangu!

Tunavyowekewa kauzibe na madingi wa kaya hii sina hamu. Bila aibu eti tukiishaula wanataka nao watule! Mmenoa haleti mtu trekta wala harrow. Siku nikitia timu nitakuja na vitu vya maana kama shahada feki nyingi ili kila mtu anione msomi kama akina Mustaafu Mkulu, Imma Mchimbi, Dorora Kamalau, Meri Nangu, Didie Massamburi na wengine wengi wenye kago feki.

Kumbe zamani nilidhani bingwa wa kufoji ni Richie Ndassaa na Sam Chililo! Kumbe mko wengi! Jitu zima linaringia lidigrii la vichochoroni. Eti linajiita dokta. Ingekuwa rahisi hivyo mbona mzee mzima ningeitwa Profesa Emeritus. Unakijua cheo hiki? Ili kupewa sifa hii lazima uwe umepayuka hadi koo lipasuke.

Juzi nilicheka sana niliposikia watu wanaojipendekeza kwa Njaa Kaya wakimuita dokta kwa sababu ya kupewa shahada ya heshima isiyo kuwa heshima. Hizi ndude huwa wanapewa wakuu wa vijiwe vya Kiswahili. Hata Joji Kichaka pamoja na ukihiyo wake asingekubali kupewa shahada ya heshima.

Jamaa baada ya kuona Njaa Kaya anawaminya kwenye jumuia uchwara ya Afrika ya Mashabiki waliamua kumtuliza kwa kumpa heshima isiyokuwapo. Endelea kuzubaa. Kuna siku Ewassa na Rost Tamu watapewa haya madudu, shauri yenu.

Nikirejea kwa wa kupinda, ingawa alichemsha kudai tulioko majuu turejee na matrekta wakati lisirikali lake likirejea na mishangingi, alipatia kitu kimoja; kumwamuru mpiga mahesabu wa serikali kushughulikia familia jizi ya Kimdunge Ngumbaru Mweha pale UBT. Huyu jamaa Bi Mkubwa atamponza kama Annaa alivyomponza Benny. Wanawake wengine kwa tamaa, utadhani Salamaa au Annaa pale jumba jeupe!

Mijitu mingine kwa tamaa hata fisi ana nafuu. Ubunge wa dezo, uwaziri wa porojo, ulaji katika halmashauri kuu ya wizi ya kiama wewe, UBT wewe! Kustaafu ndiyo usiseme. Jitu lina miaka mia nane bado linataka vyeo na biashara haramu! Kwa nini hamkujifunza kwa Musa wa Mchonga?

Kitu kingine nitakachorejea nacho ni nakala ya katiba. Hii huenda itawaamsha walevi wawaijie juu wezi wao waheshimiwa wanaopenda kuiba na kuombaomba utadhani kaya haina madini na samaki wa mabilioni.

Pia nitarudi na jeuri na unywanywa wa kudai kila haki kama jamaa wa majuu. Ukikatika umeme wanatimua serikali. Bei za vitu zikipanda serikali bye bye. Huku hakuna kutishana kama alivyofanya yule daktari wa giza, Idilisha Rushdie. Ukimtisha mwananchi siku inayofuata unatimuliwa hata kama wewe ni mkwewe rais au waziri mkuu. Huku si kama Bongolala ambako utawala ni uungu.

Huku mambo tofauti. Mijitu inaua kilimo kwa kushabikia ufisadi na ulanguzi wa madini wanyama na roho za watu inakusanifu tuje na matrekta. Ili iweje? Nayo yabinafsishwe kama viwanda na mashirika ya umma mliyoyauma bila huruma? Kwanza nani anapenda kulima iwapo kuna michoro rahisi ya kutengeneza mabilioni kama Kagoda, EPA, CIS, CCM, ANBEN, Fosnik, Tanpower, uchaguzi na madude mengine?

Kilimo waachie punda si watu. Nani ana haja ya kulima iwapo uchuuzi na umachinga unalipa hata kama mgambo wa Kondoo wanawaibia machinga wa Kiswahili wakiwaacha wa Kihindi na Kichina?

Najua. Nikija watanigwaya, maana nikianza kumwaga ung’eng’e watajua ni Mjamaica au Mmarekani. Kwanza nikija nitabadili hata uraia ili nisikumbwe na laana inayowakumba wenzangu.

Kwa vile walevi wana njaa sana, kingine nitakachokuja nacho ni unga. Usiniulize kama sembe au bwimbwi.

Ili wakupinda afanikishe azma yake, aliambie lisirikali lake kuacha kununua mitumba ya mitambo kama ile ya IPTELO na badala yake inunue matrekta. Pia iache kuwekeza kwenye uchukuaji uitwao uwekezaji, badala yake ikawekeze kwenye kilimo cha kisasa na si cha kisiasa kama sasa.

Pia nitarejea na bibi kizee wa Kizungu kuwakogea walevi. Lazima nimlete hata kama mzee kuliko mimi. Lazima nije naye hata kama atakuwa akinitumikisha kama mkewe kiasi cha wenye wivu kuniuliza: ‘Mpayukaji, we na mkeo nani kaolewa?’

Lazima hata kama anathamini mbwa wake kuliko mimi, lazima hata kama ni mvivu wa kupika, kufua na kuzaa. Mbona kuna wavivu wengi tena wanalipwa kwa uvivu wao?

Kitu kimoja kiko wazi. Sitarejea Bongolala kabla ya Wabongolala kupelekwa Kanani na kupewa maisha bora badala ya haya yaitwayo maisha ya usanii bora.

Kwanza, kuna jamaa wa Intelijensi amenitonya kuwa nikija nitakolimbwa au kubalaliwa kwa sababu nasikia wakubwa hawapendi mawe yangu. Nasikia mganga wao amewaambia kama wanataka kupata sanaa nyingi za kuwazugia walevi, basi wapate ubongo wangu waule ili wawe na akili. Nilishangaa maana mimi si albino. Kwa nini asiwaambie wale ubongo wa fisi ili ufisi uwatoke?

Kabla sijasahau, nitarudi na meli ya uvuvi haramu. Nimegundua Bongolala sawa na shamba la bibi ambalo unaweza ukaiba, ukatapeli na ukafanya kila utakacho bila kushtukiwa. Walevi wangejua kuwa kila mwaka meli zaidi ya mia zinawaibia samaki kwa tani, wangesimamia ili waweze kuwa nchi yenye kutoa misaada hata kwa Watasha!

Wambie akina Chenga, Liumbaa, Nkapa, Dk. Rushdie na wengine wafanye kazi hiyo si sisi.
Chanzo: Tanzania Daima Machi 25, 2009.

No comments: