The Chant of Savant

Saturday 22 June 2013

Mghorofa wa Udosini na mkangafu vyamtishia mlevi

 Si juzi mlevi nikajifanya mdosi kwenda kwenye mitaa ya udosini eti kusaka vidosho nisijue vidosho vya kidosi huwa haviolewi wala kuchukuliwa na walevi vinginevyo waende kusoma kule na kuvizoa kama dagaa! Hawa jamaa kwa ubaguzi especially wakiwa huku! Ajabu hawabagui dada zetu wala nyanya na njuluku zetu hasa wakiwa kwenye vigwena vyao na mafwisadi wetu wenye ulaji! Hayo tuaache si mwake leo.
Mlvevi nikiwa nachungulia kwenye maghorofa ya Msajili wa Wadosi si lile ghorafa lililomshinda profwesa Ana Tiba Ijuka likanitazama na kusonya mswahili nakwenda kule kufanya nini. Nilisikia jumba likisema kwa hasira, “We swahili mi taagukia veve dugu yako ikose zika veve.” Nilistuka kusikia jengo likongea.
Bahat nzuri wakati mghorofa ukinitishia nilikuwa na mgosi Machungi yule kichaa wangu toka Mashidei Usambaani. Kusikia vile aliamua kujivuvumua na kulijibu, “Mgosi si uende uangukiane na poofesa Anna Tiba Ijuka mnayeshindana?” Naye alisonya na kuongeza, “Unadhani wote ni wala rushwa kama wale uliowahonga na kukugwaya. Nitakupiga zongo hata uembue mimacho.” Baada ya kumalizia sentensi yake tulitoka mkuku kwenda kusimulia yaliyotusibu udosini.
 Baada ya kutoka pale tulikwenda kuwapa stori walevi wenzetu ya jengo kuongea na kututishia. Hawakutukawiza kutupa laivu kuwa tuache ushamba.  Kwani lisingekuwa linaongea si lingekuwa limeishabomolewa miaka mingi iliyopita? Alichomekea mlevi. “Mmesahau kuwa waziri mzima alijivuvumua kudai livunjwe na wenye nazo wakamzunguka kwa bosi wake na ghorofa likaendelea kupeta? Huoni alivyonywea na kupwakia matapishi yake? Mnacheza na sirikali ndani ya sirikali nini? Nijuavyo mimi hili ghorofa halitaanguka vinginevyo aanguke au kunga’atuka mtu. Huoni akina Mecky Mecky Saidiki walivyoshika bango kuhakikisha haliangushwi?”
Aliendelea, “Huyu porofwesa anapaswa kurejea skuli akajifunze masuala ya ulaji na ufisadi kujuana na kulindana na jinsi ya kuishi nayo au vipi? Nadhani bi mkubwa huyu atakuwa anaomba liporomoke na kuua tena ili wale wanaolinda ujambazi huu watie akilini.”
Baada ya kumalizia nchapo wetu tulivyonusurika kuangukiwa na ghorofa tulibaki kushangaa. Lile ghorofa lilikuwa linatutisha ili kutoa ujumbe kwa waliolishikilia bango wasijue halitabomolewa. Ukitaka kujua kinachoendelea hebu uliza wale jamaa waliBnyakwa baada ya ghorofa dada kuua walevi wamefanywa nini kama siyo kupigwa dana dana ili hasira zipoe waendelee kupeta. Watu wanajifanya hamnazo kama vile hawaijui hii bongo ya kula na kulana? Mtaendelea kuliwa hadi mmalizike msipoacha ujuha wa kuangalia mambo ya hovyo yakitendeka nanyi kujifanya hayawahusu. Au mwangojea waje wafadhili toka Ulaya wabomoe mijengo mibofu kama hii? Mmenoa sana so to speak.
Baada ya kusogoa na mgosi Machungi kuhusiana na ushamba wetu alikuja na nyingine mpya. Aliapa akisema kulikuwa na mkono wa mtu si bure. Maana tukiwa tunarejea toka kwenye kisa cha ghorofa lililowashinda vigogo, alinusurika kugongwa na ngwala ngwala ambalo tulikuwa tumelipita likiwa limesimamisha na wazee wa mabao. Wawajua wazee wa mabao? Usikonde. Ni trafwiki wanaowatoa kitu kidogo na kitu kikubwa madereva al maaruf wafukuza barabara na kuwaacha waendelee kumaliza walevi wasio na hatia kwa kuwagongelea mbali. Naye mgosi kwa ushamba wake akidhani alikuwa akitembea kwenye mitaa ya Mihelo si alinusurika kukongwa!
Tulishindwa kujua kuwa hii kaya ilishabinafishwa kwa kila mwenye kutaka utajiri wa haraka. Nani anabishia hili? Kwani juzi hamkusikia skandali ya jamaa yangu mpiga debe wa zamani aitwaye daktari wakati ni kihiyo wa kutupwa? Wamjua huyu? Si mwingine ni Chris Mzindikaya Maji ya Pwani ambaye nasikia anakodisha houses 15 za umma kwa njuluku 50,000 na kupangisha wageni kwa dolari 400 hadi 500 kwa mwezi. Jamaa amejua kutuibia. Nani hakusikia skandali ya kujenga bwawa kwa njuluku za walevi zipatazo bilioni moja halafu akalitumia kwa matumizi binafsi huku akiwazuia wenye njuluku kwenda kuchota maji? Bongo hii bwana utadhani walevi hawana bongo!
Kaya ikiwa ya walevi basi kila mmoja anafanya vitu vyake kilevi. Hamkuona kule Arushae ambapo magaidindata walipovamia mkutano wa CHAKUDEMA na kuua walevi wasio na hatia huku ndata wakizuia wana CHAKUDEMA kuwakamata wenzao? Haya si maneno yangu. Ndivyo alivyosema bwana mkubwa Mtuhuru Aikaeli aliyenusurika kudedishwa na wabaya wake anaopingana nao. Ajabu wakati walevi wakinyotolewa roho mkuu alikuwa zake kwa Mother akitanua kwenye vilabu vya boli. Angekuwa Obamiza angekatisha ziara na kuja kutoa msimamo na mwelekeo. Kumbe kaya za walevi hazina mwelekeo wala wakuu wenye nao! Wangekuwa nao si mkuu angeacha matanuzi yake na kuja kuwahami wahanga na wafia au kwa vile walikuwa kwenye mkutano wa wapingaji? Hayo tuyaache.
Hata hivyo, nangoja kusikia jamaa zangu mabingwa wa kutengeneza magaidi Saydou Mwema na Mwijuu Nchembe watasemaje. Nangoja sana kusikia akina Lwakatarehe wengine wakikamatwa kama siyo ‘wasaudia’ wengine. Kaya hii bwana mazingaombwe matupu! Hakuna siku nilinawa mikono kama niliposhuhudia mazingaombwe ya ndata ‘walipowanyaka wasaudia’ halafu wakawatema na kufanya mchezo wa kuigiza kuwa ngoma droo. Nani anabisha? Waulize akina Daktari Ulimboka na Dk Absa Kibanda. Tangu wafanyiwe uhayawani hakuna kilichofanyika. Waliowaigondhu bado wanatesa huku wao wakiteseka. Walimnyonga Sokoine na udume wake itakuwa vifaranga!
Baada ya kupiga stori hizi za kutisha na mgosi tulikubalia yaishe na kumwachia Mungu huku tukingoja kuona nani ataporomoka kati ya ule mghorofa na Profwesa Nchomile aka Kaju wa Mulo wa Tiba ya Ijuka. Hakika hiki kipute kati ya Tiba na Mecky tutaona nani zaidi kwenye gemu hili la kulindana.
Baada ya kumalizana na mgosi ilibidi nimpe ofa lau aende kupata boha ili kupoza machungu ya kunusirika kugongwa na mkangafu pamoja na kuangukiwa na mghorofa wa udosini. Maskini hakujua kuwa huu mghorofa uko kwao wakati yeye yuko ugenini tena ukimbizini.
Je wangapi wataliwa? Who knows? Guess what. I know you all are going kuliwa just soon. Tia akilini mtakwisha hivi hivi mkishangashangaa wakati wenzenu wakizidi kuwatumia kulhali. Mbona huko nyuma hamkuwa hivi?
Salamu wa washikaji wote maeneo ya Ilala mitaa ya Shingo Feni. Mpo?
Chanzo: Nipashe Jumamosi Juni 22, 2013.

No comments: