BI Sofi Lion aka Kanungaembe akiwa ameandamana na Kanji, anaingia kwa furaha ya aina yake. Si kawaida yake kununua gazeti ukiachia mbali kushobokea yale ya udaku.
Leo kavunja mwiko. Anaingia akiwa na gazeti la Tanzania Daima la leo. Baada ya kuamkia na kupewa kahawa yake analianzisha: “Mmeona nyie mnayependa kumkandia mkuu?”
“Unamaanisha ni?” Anauliza Mijjinga akionyesha kuudhika.
Kabla hata ya Sofi kujibu Kanji anakwanyua mic: “Veve iko ishi dunya gani? Hapana jua kuwa kuu ikofanywa bora ongozi Afrika inayotumikia vatu yake?”
“Eti amefanywa nini?” Anauliza Mbwa Mwitu ambaye leo ametinga vazi la Kinigeria na kuonekana mnene kuliko kawaida yake.
“Sasa yeye bora ongozi Afrika yote, tena tumia bora. Veve hapana soma gazeti nini?”
Msomi Mkatatamaa anaamua kuingilia kati na kusema: “Go tell it to the bird. Ana ngozi gani bora au unaongelea hii tuzo ya kienyeji ya urahisi bora na kutumia umma iliyotolewa na NGO ya kitapeli isiyo na ithibati? Ajabu watu wanajisifia ujinga na kuingizwa mkenge. Uongozi bora hupimwa na watawaliwa, haupimwi na matapeli wa kimataifa. Hata hivyo, hujakosea Kanji. Kweli ni rahisi bora kwa wachukuaji na majangili na wauza bwimbwi.”
Kapende anamega mic. “Yaani hata kanyabwoya nyinyi mwajisifia tena kuingizwa nkenge? Huenda hawamaanishi utumishi bali utumiaji wa jamii, tena usio bora. Kwani hao waliompa huo ujiko ni akina nani kama si wasasi ngawira wanaolewesha walevi wa madaraka na kuwatumia kutukwapulia vyetu?”
Mgosi Machungi anatia guu. “Hawa waiotoa huu ujiko wanaijua Danganyika au wamekaa huko majuu na kuamua kutoa hizo sijui tuzo sijui heshima? Yaani pamoja na ujangili, ujambazi, ufisadi, uvivu, uzuuaji, ufujaji mai za kaya, matumizi mabaya na upuuzi wowote, bado kuna watu wanatuona mafaa kiasi cha kututia vidoe machoni? It can’t be. Lazima tikue na kubadiika.”
Mipawa anatupa kichungi cha sigara na kudema: “Laiti hii heshima sijui tuzo ingetolewa na The Mail on Sunday kidogo ningeamini. Kimsingi, hawa waliotoa hiyo wanayoita tunzo wana wanachotaka kama si kutuona mabwege. Kama si hivyo, basi wameamua kutusimanga.”
Anakunywa kahawa yake na kutafuna kashata kabla ya kuendelea: “Hiyo tisa, kumi ni pale hili litakapogeuka sera kiasi cha wachovu waliozoea sanaa kuanza kuandamana na kupongezana kwa kusifiwa ujinga. Hivi kama tutaangalia mambo bila miwani ya mbao wala makengeza, jamaa ana nini cha kumfanya awe bora? Mbona wenzake kama Theodoro Obiang Nguema, Joel M7, Bob Mugabe, Jake Zuma, Mfalme Mswatii, Paulo Biya, Yahya Jammeh, Ali Bongo, Faure Eyadema, Abdel Aziz Bouteflika hawakupewa au “ubora” wao hautambuliki?”
“Hee! Inatosha mkuu maana inaonekana unawajua viranja wote wa bara hili.” Anachomekea mzee Maneno.
“Kwanini nisiwajue wakati nina PhD ya Political Science? Unadhani nimegushi kama wahishiwa wenu?” Anajisifu Mipawa.
Mpemba aliyekuwa amechelewa kuwasili anaamua kuvaa buti. “Yakhe nina wasiwasi. Huenda wapo wasanii ima ubalozi au huko majuu wanaojua udhaifu wa mtu wetu waloamua kuandaa hili zengwe ili wampate. Maana, haiingii akilini ati.”
“Unashangaa nini wakati sera zetu zinatoka huko huko majuu? Laiti jambo hili lingefanywa na magazeti yanayosifika kama vile New York Times, Washington Post, The Huffington hata The Daily Mail on Sunday. Ingetolewa tuzo ya kupamba ujangili na bwimbwi na ufisadi, kidogo ningeelewa,” anajibu Msomi.
Kabla ya kuendelea, Mzee Maneno anamkatiza. “Msomi inatosha. Maana naona magazeti yote ya huko Ubushini na Uchakani unayajua sana. Hata hivyo, kuna haja ya sisi kuanza kukua na kujiamini. Hivi kweli Danganyika Daima inaweza kumpa heshima au tuzo Baraka Obamiza akaichukua?”
“Subutu.” Anajibu Mipawa.
Mgosi anachomekea. “Mgosi umeaua. Huoni wanavyokwenda kue wanavyopitishwa mlango wa nyuma kuingia White House? Unakumbuka alipokuja Obamiza watu walivyojikata na kujikanyaga wakati wao wakienda kwake wanapangiwa madakika ya kwenda kupiga picha na kutimliwa kama wezi?” Mgosi anaamua kukandia.
“Yakhe hata juzi kule Ukamerunini jamaa alionekana na Waziri wa Mambo ya Nje huku akiingizwa kinyume nyume kwenda piga picha. Hii aibu wallahi. Mbona Nchonga hawakunfanya hivyo?”
“Ami usilinganishe tembo na inzi ati. Mchonga ule ulikuwa mtambo si mchezo. Ilikuwa ni think power ile siyo hawa hamnazo,” anajibu Mipawa huku akikamua kahawa yake. Kwa alivyobukanya think power badala ya powerful thinker Msomi ananikata jicho la wizi.
Kapende anaamua kuharibu zaidi. “Hawa jamaa wanajua udhaifu wetu. Wanachonga vioo na kutuingiza gharama ya kuwaibia wachovu kwa kusafiri kwenda kupokea vipande vya vioo. Jana alikuwapo bi mkubwa akijitafutia ujiko kwa kupewa tuzo za uongo na ukweli. Kesho dingi naye kiguu na njia kwenda kupokea vioo. Wenzetu wanacheza nasi kisaikolojia.”
Sofi kashikwa pabaya! Anaamua kukwanyua mic. “Watu wengine wanaongea kama hawajasoma. Huwezi kuita tuzo kipande cha kioo halafu ukaendelea kujiona unajua mambo wakati ni mzungu wa reli.”
“Sofi pasha hii yote nayokandia tuzo ya kuu. Halo halo sasa tapasuka nyingi ile nachukia fanikio ya kuu.” Kanji anaamua kuwa mtu wa mipasho.
“Kanji hujakosea kusifia jamaa wenzio wa Kinigeria hawa. Hakuna waliponiacha hoi kama pale nilipogundua kuwa tuzo yenyewe inatolewa na balozi wa Nigeria.
“Huna haja ya kushagaa. Nimekwenda kwenye wavuti wao na kukuta madudu ya ajabu. Kwanza hawajielezi wao ni nani. Pili maelezo yao ni ya kijanja kijanja. Kwa ufupi hawana tofauti na Richmonduli iliyotuibia njuluku zetu kwa kushirikiana na hawa hawa wanaopewa tuzo za ubora bila ubora. Sijui hawa kama wanasoma habari za kaya na kuona tembo na faru wanavyouawa ukiachia mbali ile hotuba ya kuvuruga Bunge la Katiba. They must be crazy and stupid so to speak. When it comes to who is deserves the accolade, the punks anointed the sick anyways?” Msomi anaamua kumwaga Ukameruni kwa usongo.
Kijiwe kikiwa kinanoga, si likapita shangingi la Ben Maembe akirejea kutoka kujivua nguo. Tulilikimbiza kwa mawe na kashata hadi likatokome.
Chanzo: Tanzania Daima Aprili 16,2014.
3 comments:
Sasa na wao wenyewe wanadai kuwa ni wasomaji wa "jarida" hilo ndio walimchagua, ni nani hao? Mimi huwa nawauliza marafiki zangu waCameroon and Wanigeria kama wanamjua huyu bozo lakini hawana habari naye, wao wanamjua Nyerere tu. Basi wawe na aibu kidogo kabla ya kujidhalilisha kila sehemu duniani.
Usishangae hao wasomaji tunaoambiwa ni wale uliowaona kwenye hafla. Unasema wawe na aibu wakati matapeli waliumbwa bila aibu? Anyways, they are fooling but themselves.
Usanii ndani ya wasanii!
Post a Comment