“Kuna majangili 40 waliotambuliwa na tumetambua mtandao mzima, pale Arusha kuna mtu mkubwa alikuwa anaendesha biashara. Kazi ilikuwa ni kutambua mtandano wote, ule mtandao ni mpana sana,” hayo ni maneno ya rais Jakaya Kikwete aliyotoa aliporejea nchini akitokea kwenye mkutano wa kupambana na ujangili huko London Uingereza. Je baada ya kutambua huu mtandao serikali imechukua hatua gani? Je Kikwete ameamua kutangaza kabla ili kuwastua wahusika waishie au waache ujangili? Je ni kweli anaujua mtandao huo au ni yale yale ya orodha ya majina ya vigogo wa mihadarati? Je Kikwete yuko tayari kuwataja wahusika?
Huenda Kikwete aliongelea ukubwa wa mtandao ili aonewe huruma au kueleweka kuwa ni vigumu kuuchukulia hatua. Je huo mtandao ungewinda madaraka yake angeishia kulalamika au kuchukua hatua? Je Kikwete anathibitisha ukweli wa madai kuwa marafiki na jamaa zake wanahusika na kufaidika na ujangili kama lilivyodai gazeti la The Mail on Sunday la Uingereza la Februari 8? Gazeti hilo liliandika, “Utawala wa Rais Kikwete umetawaliwa na mauaji ya tembo yaliyovunja rekodi katika historia ya nchi yake. Kibaya zaidi, wahifadhi wanasisitiza kuwa, ndani ya Serikali kuna viongozi wanaoshiriki biashara hiyo.”
Gazeti lilidai kuwa wabunge, maofisa wa juu na wafanyabiashara, wametajwa bungeni na kwenye vyombo vya habari, lakini uchunguzi unapotezwa. Pia lilieleza kuwa hata meno yaliyomo gharani mengine yanauzwa kinyemela ili kutafuta pesa kwa ajili ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kushinda kwenye uchaguzi ujao. Japo ujangili ni tatizo kubwa barani Afrika, chanzo ni mfumo fisadi na mbovu wa kijambazi wa utawala. Huwezi kuwa na sera za hovyo zinazoruhusu majangili kumilki vitalu vya uwindaji ukakwepa kuwa na tatizo. Watanzania wanajua fika. Ugawaji vitalu vya uwindaji unafanyika kifisadi kiasi cha kutoa fursa kwa majangili kumaliza wanyama wetu. Chukulia mfano kitendo cha awamu ya pili kummilkisha mbuga ya Loliondo meja Ali toka Uarabuni. Hii maana yake ni kwamba mwenye kumilki vitalu amepewa rungu la kufanya atakavyo ilmradi analipa mrahaba ambao nao ni upuuzi mtupu.
Kama Afrika haitaiga mfano wa nchi kama Australia ambayo huzuia wanyama wao kununuliwa na kuweka kwenye zoo nje ya nchi, tutaendelea kulalamika na kupoteza urithi huu muhimu. Uzoefu unaonyesha kuwa unaweza kukuta wanyama toka Afrika kwenye zoo duniani kote. Ila hukuti mnyama kama Kangaroo ambaye ni kivutio cha utalii kikubwa nchini Australia akiuzwa kwenda kufungiwa hovyo hoyo kwenye zoo nje ya Australia. Wanafanya hivyo ili kuondoa mnyama huyu kuwa kivutio nje ya nchi yao na kuwapunguzia utalii na urithi.
Kimsingi, mwenye nia ya dhati ya kupambana na ujangili si wa tembo wala faru tu barani Afrika, lazima azuie huu uuzaji wa kipumbavu wa wanyama hai kwenda nje. Wengi wanakumbuka kesi chafu na ya aibu ambapo wanyama hai walitoroshwa kupitia uwanja wa ndege wa kimataifa wa KIA. Kujua ni vipi majangili wa maofisini ambao kimsingi ndiyo muhimili wa wale wa mbugani unavyoathiri kila kitu, jiulize. Yule mpakistani Kamran Ahmed aliyekamatwa kwa kosa la kutorosha wanyama wapatao Zaidi ya 130 yuko wapi na baadaye kuwa na pesa bandia kiasi cha sh. 18,000,000? Tunaambiwa eti alipewa dhamana akatoroka. Je alitoroka au alitoroshwa ili kuepuka kuwaumbua wakubwa wetu wanaoshiriki ujangili kwa kuwatumia wageni? Kama mamlaka zingemfungulia mashtaka kwa vifungu vinavyohusiana na jinai yenyewe chini ya kosa la kuhujumu uchumi, asingepewa dhamana. Ila kwa vile wanajua udhaifu na mianya ya kisheria, wahusika walimfugulia mwenzao mashtaka chini ya vifungu rahisi ili apewe dhamana na kupotea. Kwa nchi yenye kujua faida ya maliasili mpakistani huyu, kwanza hakupaswa kupewa dhamana wala kutoka gerezani akiwa hai. Angeishia huko ili liwe somo kwa wengine wenye kufikiri kuhujumu taifa kwa njia kama hizi. Na hili si tukio la kwanza kuonyesha jinsi wakubwa zetu walivyo washiriki wakubwa wa uhujuu na unjangili huu. Nani amesahau kashfa ya Chavda ya kuiba mamilioni ya fedha za umma kwa kisingizio cha uwekezaji? Baada ya wakubwa waliomtumia kugundua kuwa uchafu wao ulikuwa umewekwa wazi eti walimuammu kuondoka nchini ili kuficha uovu wao. Hapa ndipo tunaposema wazi kuwa utetezi wa rais Kikwete wa kuwepo mtandao mkubwa ni wa hovyo.
Unapokuwa na serikali ambayo inashindwa kupambana na hata wahalifu wa kawaida, maana yake ni kwamba haifai. Maana, pamoja na wajibu mwingine, kazi kuu ya serikali ni kulinda watu na mali zao ziwe za binafsi au za pamoja. Huwezi kuwa na serikali inayolalamikalalamika bado ukatembea kifua mbele kuwa wewe ni taifa. Isitoshe, rais Kikwete amekuwa bingwa wa kulalamika lalamika tangu aingie madarakani. Viko wapi vita dhidi ya ujambazi, ufisadi, wiza wa pesa za umma na sasa ujangili? Kikwete amekuwa rais mlalamika na si mtendaji. Ameshindwa. Tangu aingie madarakani amefanya kazi mbili tu ambazo ni kulalamika na kusafiri hovyo hovyo bila kuwajibika.
Inakuwaje wenzetu wa Kenya walinde na kufaidi urithi wao sisi tuishie kulalamika kama hakuna namna kwenye uongozi? Japo wengi wanaogopa kumwambia Kikwete ukweli huu wenye uchugu, ukweli ni kwamba hana nia wala uwezo wa kutulinda sisi pamoja na mali zetu. Ameshindwa yeye na serikali yake ya CCM. Kama yanatolewa madai kuwa serikali inafumbia macho ujangili ili kuruhusu Chama Cha Mapinduzi kipate mtaji wa uchaguzi na serikali haileti utetezi unaoingia kichwani unadhani hii ni bure? Mfano wa hivi karibuni ni utetezi mwepesi uliotolewa na Kikwete baada ya kubanwa ajibu tuhuma kuwa anawajua na kuwalinda majangili wa vile wengi ni watu wake. Alipobanwa ajibu mapigo eti alisema hawezi kujibu kwa vile akutukanaye hakuchagulii tusi. Ya kweli haya? Inakuwaje rais akubali kutukanwa wakati anavyo vyombo vya kuweza kuchukua hatua kisheria kama hakuna namna? Ni ajabu na hasara kuwa na rais wa namna hii anayeweza kutukanwa akabaki kulalamika na kukwepa kujitetea hasa ikizingatiwa kuwa rais ni alama na kielelezo cha taifa.
Kumbe rais anawajua majangili waishipo na wafanyacho ila hataki kuwashughulikia kama alivyofanya kwa wauza mihadarati ambao alisema ana orodha ya majina yao. Kwanini? Kikwete anapaswa kutupa majibu yanayoingia kichwani vinginevyo awajibishwe yeye na serikali yake. Hakuna haja ya kuendelea kubebembelezana wakati taifa letu likiangamia.
Chanzo" Dira Aprili 7, 2014.
3 comments:
Kikwete hawachukulii hatua kwa sababu anahusika kwa namna moja au nyingine. Hayo mambo hayawezi kuwa yanafanyika bila baraka yake au manufaa yake. Hiyo "playing dumb" kwa ughaibuhi ni kitu cha kufedhehesha lakini kwa watanzania unapata watetezi wajinga, "Rais mwenyewe ni mtu mzuri lakini ni watendaji wake tu!
Hey, hata na mimi nina orodha ya mambo mengi yanayompa Kikwete sifa mbaya, Ujangili, rushwa, uhaba wa ajira, umeme, maji, maadili, heshima ya nchi, uzembe, ubadhirifu, wizi, kutowajibika, safari zisizo na tija, mauaji ya wapinzani.......
Niwakumbushe tuu, Ndege kubwa kabisa ilikaa pale Kilimanjaro International Airport majuma mawili, na [pia kuchukua wanyama pori wakubwa kabisa maumbile nao hawakuonekana.
Eti anasema watu walioko ughaibuni kazi kukosoa tuu kwenye ma-blogu kwamba mambo kama haya je humsifie kwa jambo lipi hasa!!!?
Anon na Jaribu mmeeleweka ingawa wahusika watajifanya hamnazo na kuendelea na business as usual. Natamani jamaa hawa wasimame na kupinga madai ya The Mail on Sunday kwa hoja yakinifu na zinazoingia akilini. Hata hivyo ngoma nzito hawaiwezi zaidi ya kuwatumia makanjanja na wanywanywa kama Salva Rweyemamu kuharibu zaidi wakijifanya wanajibu.
Post a Comment