Mkurugenzi wa Taasisi ya Kupamba na Kushiriki Rushwa (TAKUKURU) nchini Dk Edward Hosea |
Taarifa ya Afrobarometer, taasisi inayotathimini viwango vya rushwa nchini kuwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ni moja ya taasisi kumi zilizotajwa kuongoza katika kuomba na kupokea rushwa zinasikitisha na kuondoa maana nzima ya uwepo wa taasisi hii. Kabla ya kufichuliwa, wengi tuliiamini na kuiasa ipambane na ufisadi mbali mbali tusijue kuwa nayo imo!
Wengi walidhani kuwa TAKUKURU ilipaswa kujikita kwenye kupambana na kuzuia rushwa. Kumbe si hivyo, inashiriki vilivyo jinai iliyoanzishwa kupambana nayo. Huu ni ushahidi wa mfumo mbovu wa kifisadi uliotamalaki kuozoeleka, na kwa kiasi fulani, kuanza kukubaliwa na wakubwa tokana na kutamalaki. Inashangaza maafisa wa TAKUKURU wanalipwa kwa kazi gani iwapo ni washiriki wazuri wa rushwa. Kwa mujibu wa Afrobarometer,iliyoshirikiana na Repoa kwenye utafiti huu, TAKUKURU inashika namba ya pili baada ya polisi kwa kudai na kupokea rushwa nchini. Taarifa ya Afrobarometer inabainisha, “Utafiti umebaini kuwa polisi ni vinara wa rushwa kwa asilimia 50, wakifuatiwa na maofisa wa TRA (37), Majaji na Mahakimu (36), Takukuru (29), Maofisa wa serikali za mitaa (25), watumishi wa umma (25), wabunge (22) na rais na maofisa wa Ikulu (14). Alisema pamoja na ongezeko hilo, wananchi hawaridhiki na juhudi za serikali katika kushughulikia rushwa.” Kwa kushika nafasi ya pili ni kwamba TAKUKURU imekiuka malengo ya uwepo wake ukiachia mbali kuchangia vilivyo katika kuongezeka kwa jinai inayopaswa kupambana nayo na kuizuia. Hii maana yake ni kwamba tumewapa wezi kulinda benki au duka. Je tutegemee nini? Je nini kifanyike kuondokana na kadhia hii?
Kimsingi, mfumo wa sasa unaifanya TAKUKURU kuwa chombo cha kula rushwa badala ya kupambana nayo. Inaipamba rushwa badala ya kuizuia. Kitendo cha kuiweka TAKUKURU chini ya ofisi ya rais kinazusha shaka juu ya uhuru wake katika utendaji wake. Tujalie kuwa rais au jamaa zake wanatuhumiwa kupokea rushwa, unategemea iwashughulikie wakati inapokea amri toka kwa rais mwenyewe? Nadhani hii ndiyo maana marafiki wengi wa wakubwa wanaotuhumiwa wazi wazi kwa rushwa hawakamatwi wala kuchunguzwa. Tumeyaona na tunayajua. Wako wapi watuhumiwa wakuu wa wizi wa mabilioni ya fedha za umma chini ya kashfa ya escrow? Ilifikia hata kuwawajibisha baadhi ya mawaziri ilikuwa ni mbinde baada ya rais kuonyesha wazi kutokuwa na nia wala utashi wa kuwashughulikia hadi umma ulipokuja juu kiasi cha hali kutovumilika ndipo wakaachia ngazi. Rejea kuendelea kulipwa kwa marupurupu ya kustaafu kwa waziri mkuu wa zamani Edward Lowassa aliyeachia ngazi tokana na kubainika kuwa nyuma ya kashfa ya Richmond mwaka 2008 ambapo alidai bayana kuwa alikuwa akiripoti kwa rais kila hatua iliyokuwa ikichukuliwa. Hii maana yake ni kwamba rais alikuwa akijua na alishiriki.
TAKURURU imeonyesha – tena tangu zamani – ilivyo chombo cha kula rushwa pale ilipotaka kumsafisha Lowassa bila mafanikio baada ya umma kuja juu hasa bunge la Jamhuri ya Muungano kuunda tume iliyomng’oa madarakani. Kwa wanaokumbuka maneno ya rais wakati akikubali Lowassa kuachia ngazi, wanajua kilichokuwa kikiendelea angalau kwa ushahidi wa kimazingira.
Watanzania wanajua kuwa TAKUKURU imekuwa ikiwakamata dagaa huku mapapa ikila nao meza moja ili kujionyesha kuwa inafanya kazi. Imekuwa ikikamata makarani, mahakimu wa ngazi za chini, walimu, manesi na wafanyakazi wadogo wadogo huku ikiendelea kuwafumbia macho mapapa. Uliza ni majaji wangapi wamekamatwa kwa kula rushwa. Hata hawa waliotajwa wazi wazi kupokea fedha toka kwa mtuhumiwa mkuu wa escrow bado wako kazini huku serikali ikikaa kimya kutaka mambo yapoe waendelee na mchezo kama kawaida. Namna hii hatuwezi kuishinda vita dhidi ya rushwa, na kushindwa huku ni maafa kwa uchumi wa taifa letu. Mfano mwingine wa karibuni ni kutajwa kuwa baadhi ya vigogo wameficha mabilioni ya shilingi kwenye mabenki ya Uswisi na kwingineko ughaibuni. Pamoja na serikali ya Uswisi kuahidi kutoa ushirikiano, hakuna aliyejihangaisha kutafuta huu usaidizi ili kuwabaini na kuwashughulikia waliotorosha hii pesa na kuirejesha. Nani amkamate nani iwapo kambale wote wana sharubu? Mifano ni mingi tu.
Mbali na kuiondoa TAKUKURU chini ya ofisi ya rais, inapaswa kufumuliwa na kusukwa upya chini ya utaratibu mpya ambao utawachuja na kuwachunguza maafisi wake. Hapa ndipo haja ya kurejesha sheria ya maadili unapoonekana. Kwani kwa sasa katika Tanzania mtu yeyote anaweza kulala maskini akaamuka tajiri na asishughulikiwe wala kuhojiwa alivyopata huu utajiri wa ghafla bin vu. Watu wanashiriki vitendo vya jinai kuanzia kula rushwa, kuuza mihadarati, ujambazi na wizi wa mabilioni ya umma bila wasi wasi kutokana na sababu kuu mbili yaani kutokuwapo sheria inayowabana na kuwataka wataje mali zao na kueleza walivyozipata. Pili ni ile hali ya taasisi husika kuwa kinara wa rushwa ambayo kimsingi, ni mama wa jinai zote. Jambazi mkubwa anakamatwa anatoa rushwa na kuendelea na mchezo kama kawaida. Mla rushwa anabanwa anatoa chochote na mchezo wa “tua tugawane” unaendelea.
Kwa sasa, kwa mfano, kuna haja ya kuwachunguza maafisa na watumishi waote wa taasisi zilizotajwa kuongoza katika rushwa ili kujua wana ukwasi kiasi gani na wameupata vipi. Si ajabu ukakuta maafisa wengi wa TAKUKURU ni matajiri wa kutupwa kwa vile wanatumia nafasi zao kujineemesha kwa kupokea rushwa waliyoapa na kuajiriwa kupambana nayo. Hawa wanapaswa kuchuguzwa kwanza na kuamriwa wataje mali zao na jinsi walivyozipata. Hata hivyo, hili linakuwa gumu kidogo hasa ikizingatiwa kuwa hao wakubwa waaopaswa kuamrisha uchunguzi huu wameshika na kigugumizi wanapotakiwa kutaja mali zao. Kuna haja ya kuwa na tume huru ya kukagua taasisi nyingine za serikali kuhusiana na utendaji wake kwa kushirikiana na ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Fedha za Serikali (CAG) ambayo imefichua uoza mwingi bila kushughulikiwa.
Chanzo: Dira.
2 comments:
Fisi wakilinda mali ya nchi(Mbuzi na mifupa)!!!!!!!!!!!
Anon umeniacha hoi. Ina maana Bongo sasa ni mifupa mitupu siyo?
Post a Comment