Mwenzenu leo nina furaha ajuaye ni Mungu na bi mkubwa wangu ambaye kama mpango huu utajipa lazima ajinome kama hana akili nzuri au vipi? Nina dili bab kubwa. Naona yule anatoa mimacho akidhani dili hii ni escrow au kupiga njuluku kwenye uchakachakachuaji wa katiba mpya. Ungejua mimi si fisadi wala jambazi wa kutumia kalamu, usingefikia hitimisho hili. Hata hivyo, si makosa yako. Makosa ni ya mfumo unaotengeneza ngurumbili wanaoamini kuwa kufanikiwa lazima kuwa kupitia wizi na ufisadi badala ya kuchangamkia ntchito.
Basi mwenzeni ni mbunifu wa kupigiwa mfano. Na karibuni nitaukata bila kuwaibia wachovu wala walevi kama wale. Nina mpango wa kuanzisha kampuni ya kuwatungia vitabu vya sifa wagombea urahisi hata ubuge kayani. Sichagui chama wala itikadi. Ni pochi yako tu. Huna haja ya kwenda Bagamoyo au Sumbawanga kuroga.
Najua kaya yetu imetwaliwa na kutawaliwa na mazingira ya mazingara karibu katika kila kitu. Wengi wa wachovu na wavivu wa kujituma na kufikiri hufikiri kuwa mja hawezi kufanikiwa bila kufanya ushirikina. Njoo kwangu nikuwezeshe uukwae hata kama utanisahau. Muhimu ni kukatiana mapema kabla ya kuingia kwenye mjengo au jumba la ulaji almaaruf ikulu. Inashangaza kuona jitu zima na akili yake eti linakwenda kwa mganga njaa kihiyo kutafuta dawa ya kushinda mtihani wakati mganganjaa mwenyewe hata hajui kusoma na kuandika na kama amesoma hajavuta madarasa. Wengine eti wanakwenda kutafuta utajiri kwa wezi wanaowatoza fedha huku wao wakiwa wananuka umaskini. Wangekuwa wanajua dawa ya utajiri si wangejitajirisha wao kwanza kabla ya kuwatajirisha wengine. Wanawapa dawa ya utajiri au ujinga na ufukara? Mtaishia kuwamaliza zeruzeru na vikongwe na kufia gerezani msitajirike msipobadilika.
Kwa wale wanaoamini katika ushirikina mmekishwa. Mtatapeliwa na kuliwa bure muishie kulalamika bila sababu wakati kiboko ya ushindi nipo naita kwa wenye mshiko waje tushikishane na mambo yaende bien au vipi? Au mnataka nitangaze neema hii kwenye magazeti na runinga ndiyo mjue nafanya kweli? Njoo nikutungie kitabu watu wakusome na kukupenda hata kama wabongo si wasomaji wa vitabu. Hata ukiamua kujihoji na kujijibu wewe njoo unipe uchache wangu ubandike jina langu kuwa mimi ndiye nilikuhoji hata kama ukweli ni kwamba ulijihoji na kujijibu kama wale ninaoanza kuwastukia.
Njoo unikodishe nikuandikie makala za kuimba sifa zako na kukumwagia sifa kemkem ili watu wakupende na kukupa kura ya kula. Nitakutungia hata zaburi na mashairi, ngonjera na tenzi kuhakikisha kila mtu anakupenda na kukupa ulaji. Nitaipamba na kurembesha sura yako hata kama ina namna hadi kila mtu akukubali kuwa wewe ni handsome and flamboyant. Hivyo, akupe ulaji. Nitakupamba kuwa wewe ni chaguo la Mungu, watu, miti, wadudu hata wanyama. Kazi hii ninayopanga kufanya imeishafanyiwa majaribio na magwiji kama vile Silvia Rweyempendeza. Mara hii mmesahau akina Rweyependekeza waliopewa ulaji ikuu na ukuu wa wilaya siyo?
Mie sihitaji kazi zenu wala kulipwa fadhila zaidi ya kunikatia mshiko wangu kila mtu anakwenda zake kivyake. Ukipata au kupatikana tusilaumiane ati. Nitakutungia vitabu na mashairi na nyimbo vinavyoingia akilini ili hata ukidondoka angalau uwe na cha kujisomea. Mie siyo kama wale kasuku mfano Bangendagenda aliyeandika upuuzi kibao akijigonga kwa Njaa Kaya akitegemea kupewa ubalozi akaishia kuvishwa mkenge aliotaka kumtwisha msanii mkuu. Mie naandika vitu vilivyokwenda chuo vyenye kuwavuta hata nyoka watoke pangoni. Naandika nyimbo ambazo hata nyuki na nyoka wakizikia wanafurahi na kuweka mbali sumu na ukali wao. Njoo kwangu niwapeni ulaji, urahisi hata ukubwa wa kila aina. Mimi ni kiboko wa Bagamoyo na Sumbawanga. Huna haja ya kunyotoa roho za mazeruzeru wala kutembea uchi au kubakwa na waganga ndiyo upate huo ulaji. We njoo kwangu nitayamaliza matatizo yako.
Tuache utani. Hakika huu ni wakati wa kukwapuana. Mwanasiasa anawakwapua wapiga kura na wachovu
Mwanasiasa naye anakwapuliwa na wauza maneno. Unamkwapua huyu naye anamkwapua yule mradi mkwapuano ngoma droo au vipi? Hii ndiyo Bongo kaya ya wasanii.
Uhitaji kuwa na kijana kama hawa wanaotumia ujana wao kama silaha dhidi ya vikongwe. Mie nitakuweka mkorogo wa kimaandishi na wachovu watakuzimii. Nitasema wewe ni kijana wa miaka 99. Hapa lazima nipandishe na kubadilisha namna ya kuangalia umri wa mtu. Kwa vile kuna imani kuwa maisha huanzia miaka 50, hivyo ukiwa na miaka 99 utakuwa sawa na mtu mwenye miaka 40 na ushei. Hujawa kijana hapa? Ili kuwatibulia ulaji hawa vijana wanaojiletaleta wakati hawana uzoefu zaidi ya uchu na uroho wa madaraka, nitawaita vichanga ambavyo vinapaswa kuwa kwenye shule za vidudu kisiasa na si kwenye ulingo au vipi? Wale wenye mvi nitabadilisha maana ya mvi na kuziita busara hata kama ni mafisi na mafisadi who cares kama nitapata mshiko wangu?
Eneo jingine nyeti linalohangaisha watu hadi wakaghushi na wengine kupata shahada kwa kuvua nonihino. Elimu, elimu, elimu. Uhitaji kuwa na PhD na makandokando mengine. Hata kama wewe ni kihiyo au mgonjwa hata wa miwaya wewe niachie mimi nitajua jinsi ya kukujenga. Hata kama u fisadi au kibaraka wao wewe niachie mimi.
Kama wewe ni kibabu nitakupamba uonekane kijana hata kwa kubadili maana ya ujana kama ilivyokuwa mwaka 2005. Mara hii mmesahau jinsi vibabu vilivyoitwa vijana!
Chanzo: Nipashe Feb., 21, 2015.
No comments:
Post a Comment