Jogoo ni ndege mbabe afugwaye tena wa kuhurumiwa. Anasifika kwa kuwanyanyasa majike na vifaranga huku naye akinyanyaswa na aliyemfuga. Pia ndege huyu shaufu lakini dhaifu husifika kwa kupenda kuimba. Hata hivyo, ana kasoro moja kuu, huimba wimbo ule ule kila uchao miaka nenda miaka rudi. Ni ndege asiye na ubunifu wala kumbukumbu wala asiyejali alama za nyakati. Kwani hufikia mahali akachinjwa hata baada ya kushuhudia wageni wakija nyumbani akijua fika lazima atatolewa kafara kwao. Ya jogoo tuyaache.
Hivi karibu Tume ya Kupambana na Kudhibiti Rushwa (TAKUKURU) ilijivuvumua kwa kusema eti itawashughulikia watuhimiwa wakuu wa wizi wa escrow ambao umezamisha mabilioni ya fedha za umma huku ukiwagusa na kuwaondoa vigogo wengi wa serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM). Mkurugenzi wa Takukuru Dk Edward Hosea alikaririwa na vyombo vya habari hivi karibuni akisema, “Tunawachunguza wote, hatuwezi kufanya kazi harakaharaka kama zimamoto, tunakwenda hatua kwa hatua, uchunguzi ukikamilika wote watakaopatikana na hatia watapelekwa mahakamani.” Kuchunguza ni jambo moja na kuja na matokeo tarajiwa ni jambo jingine. Kwa wanaokumbuka jinsi Takukuru hii hii ilivyotaka kumsafisha waziri mkuu za zamani aliyetimka kwa kashfa ya Richmond, Edward Lowassa, hawana imani nayo tena. Kwani licha ya kuwa idara nyeti lakini dhaifu, Takukuru imegeuka shahidi wa jinai nyingi nchini hasa zinazohusisha wizi wa fedha nyingi za umma. Rejea kwa Takukuru kushindwa kuwakamata majambazi wa wizi mwingine wa mabilioni wa EPA, RITES, Meremeta, Mwananchi Gold, orodha inachosha. Je ni kitu gani Takukuru watafanya tofauti na walivyozoea?
Wapo wanaoona kama hakuna jipya na kauli ya Takukuru ni ya kujivuvumua na ya kisiasa zaidi ya kitaaluma. Takukuru wanaweza kujipiga kifua na kuapa kwa miungu yote kuwa watashughulikia kashfa ya escrow ili kujenga picha kuwa serikali inafanya kazi na inapambana na ufisadi.kimsingi, tamko hili laweza kuwa la kisiasa hasa wakati huu tunapoelekea kwenye uchaguzi mkuu. Timming ya Takukuru ni nzuri hasa ikilenga kuwaingiza mkenge wananchi hasa wapiga kura kuihukumu vizuri serikali yao. Kesho kesho utawasikia viongozi wa CCM wakijisifu kuwa wanapambana na ufisadi na wanaweza hata kunukuu au kunasibisha maneno yao na ya mkurugenzi wa Takukuru. Baada ya uchaguzi? Kila kitu kitafutikwa chini ya busati kama ilivyotokea kwa Kagoda na wizi mwingine na tunaendelea na business as usual.
Takukuru wamefanya nini kuwachunguza na hata kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria wezi katika serikali za mitaa ambao wanasifika kuzamisha fedha nyingi kila mwaka kuanzia kulipa mishahara hewa na kupandisha gharama za miradi? Takukuru imefanya nini kupambana na majangili wa kimfumo waliosafirisha wanyama wetu tena hai nje?
Tokana na historia ya utendaji tata na wa shaka ya Takukukru, wengi wanadhani hiki kinachoitwa kuchunguza wezi wa escrow ni wimbo ule ule wa jogoo. Kuna maswali mengi ya msingi ya kuulilza: Hadi wanafikia hapo walipo Takukuru mlikuwa wapi kama siyo kutumika na kuwatumikia mafisadi waliowateua. Fanyeni kama mwendesha mashtaka wa Argentina ambaye hata kama aliuawa ilikutwa hati ya kutaka kumkamata rais wa nchi bila kujali ukubwa wa cheo chake. Umma umechoshwa na Takukuru kuonekana kama nyumba ndogo ya CCM na mafisadi. Rejea CCM ilivyohusishwa na wizi wa EPA na hakuna kigogo hata mmoja aliyehata hojiwa. Rejea expose ya mwanasheria Michael Bhyndika Sanze aliyesimamia wizi huo aliyekiri baadaye. Takukuru ilishindwa hata kumhoji na kuchukua maelezo Sanze, pamoja na kukiri kushiriki kikamilifu kwenye wizi wa EPA.
Hata hivyo, wangewezaje kuchunguza wizi wa EPA wakati uliwahusisha wale wale waliowateua wakuu wa Takukuru? Hata maafisa wengi wa Takukuru ni mafisadi wenye utajiri wa kutisha utokanao na rushwa. Takukuru walishindwa hata kuchunguza ajira ya Salva Rweyemamu aliyewahi kupewa kazi ya kuisafisha Richmond ukiachia mbali ajira yake kuonyesha mazingira yote ya rushwa hasa kutumika kuwachafua wagombea wa urais walioonekana tishio kwa mtu wake mwaka 2005.
Ukitaka kuonyesha madudu ya Takukuru utajaza msahafu hasa ikizingatiwa kuwa Tanzania inaweza kuwa mojawapo ya nchi inayoongoza kwa kuwa na kashfa nyingi za wizi wa fedha za umma huku wezi wanaoufanya huu wizi wakiendelea kuwa watu wa heshima mitaani. Wako wapi wezi waliotajwa wazi wazi wa kampuni ya Kagoda iliyotumika kwenye uhamishaji wa fedha za EPA? Si leo tunaambiwa ni miongoni mwa mabilionea waliozalishwa na taifa hili linaloabudia mibaka huku likiwachoma moto vibaka.
Tumalizie kwa kuwashauri Takukuru waachane na wimbo wa jogoo. Badala yake wafanye kazi kama wanavyopaswa au wajinyamazie kama hawana la kusema kuliko kuendelea kutupotezea muda. Wananchi wasingetaka kusikia tambo bali kuwaona wahusika wakiburuzwa mahakamani hasa kutokana na ukweli kuwa kutimliwa kwa baadhi ya watendaji wa serikali ni ushahidi tosha kuwa jinai ilitendeka na walioitenda wanafahamika kwa sura na hata majina yao. Wahenga walisema: Ada ya mja kunena muungwana ni kitendo. Tendeni basi badala ya kuimba wimbo ule ule na kufanya mambo yale yale kwa namna ile ile mkitegemea matokea tofauti. Huu waingereza huuita wehu.
Chanzo: Dira.
No comments:
Post a Comment