How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Tuesday, 17 February 2015

Watanzania gomeeni kura ya maoni


          Kwa hali ilivyo, serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamedhamiria kuendelea kuwageuza watanzania majuha na vifaa vya kubarikia mipango yao michafu. Hii inatokana na kuendelea na maandalizi ya kile kinachoitwa “kura ya maoni” ambayo itapigwa ili kupitisha au kutopitisha katiba mpya isiyo na jipya wala upya. Hii ni baada ya wawili hawa kuchakachua – na baadaye – kuua rasimu ya wananchi iliyokuwa imependekezwa na Tume iliyopewa jukumu la kukusanya maoni yao na kuandika katiba kielelezo almaaruf Tume ya Jaji Joseph Warioba.
          Kwanini tunashauri kwa nguvu zote wananchi kugomea kura hii ambayo kimsingi haina faida kwao wala uhalali kwa vile ilikiuka mapendekezo na maoni yao ukiachia mbali kupoteza muda na fedha zao?
          Sababu ya kwanza, ni uhalali wa rasimu inayotaka kupelekwa kwa wananchi. Hii rasimu ni haramu hasa ikizingatiwa kuwa ilipitishwa kihuni na kinyume cha sheria. Rejea uhuni uliofanywa na makada wa CCM wakiongozwa na Samuel Sitta spika wa Bunge la Katiba na Jakaya Kikwete, aliyeonyesha wazi wazi kuwa na ajenda yake ya siri ya kuhakikisha rasimu ya Warioba inauawa.
          Pili, rasimu inayopendekezwa ni mhuri wa kulinda ufisadi. Rejea kuchakachauliwa kwa vipengele karibu vyote vilivyokuwa vikilenga kupambana na ufisadi hasa kwenye ofisi ya rais ambapo vitu kama kutaja mali, kutangaza na kuweka zawadi anazopewa rais na kuwa mali ya  umma, kuwawajibisha wabunge na vingine vingi kuondolewa. Wengi wanaojua jinsi nchi inavyonuka ufisadi na nani wanaotuhumiwa kuufanya, watakaubaliana nasi kuwa katiba husika ni ya kifisadi na inalenga kuwalinda mafisadi. Mlitegemea nini toka kwa watu wanaoonyesha wazi kushiriki na kuulinda ufisadi? Mlitegemea nini pale marais wastaafu wawili wanapotajwa kuficha fedha kwenye mabenki ya Uswisi?
          Tatu, kama rasimu hii ya kifisadi itapita –bila shaka itapita – kama watanzania watakubali kushiriki, wapiga kura waiunge mkono au kuikataa ili kuhakikisha wale waliohujumu rasimu halali wananusirika kufia vifungoni tokana na uhujumu na ufisadi waliolifanyia taifa lazima wataipitisha tu na kuwageuza wapiga kura vifaa vya kupitishia hilaki yao.
          Nne, kushiriki zoezi hili, wananchi watajigeuza nyenzo na mhuri wa mafisadi kupitishia jinai zao kwa kuwatumia.
          Tano, kwa kushiriki zoezi hili ambalo halina uhalali wala ukweli – tokana na mazingira yote kuonyesha haramu itahalalishwa, kupitia uchakachuaji – ni kujihujumu kwa utashi wao au kushiriki kufanya hivyo wakijua matokea yake yatakuwa nini.
          Sita, kushiriki zoezi hili ni kuhalalisha wizi na matumizi mabaya mengine ya fedha za umma ukiachia mbali kupoteza muda na kushiriki zoezi linalolenga kuendelea kuwaumiza na kuwatesa wao na vizazi vyao. Zimeishaanza kuripotiwa taarifa za wizi wa mabilioni ya umma kwa kisingizio cha zoezi hili. Hili halikwepeki kutokana na a) wanaosimamia zoezi hili kutokuwa waaminifu c) uzoefu wakati wa mchakato wa kuengua na kuchakachua rasimu ya Warioba na c)
          Saba, kushiriki zoezi hili haramu ni kuzika matumaini ya kurejeshwa kwa rasimu ya umma kama ilivyokuwa imeandikwa na tume ya Warioba baada ya kukusanya maoni yao.
          Nane, kugomea zoezi hili –licha ya kutuma ujumbe mzito kwa wanaodhani wanaweza kuendelea kuwageuza watanzania majuha – ni hatua ya kwanza ya kurejesha rasimu ya Warioba.
          Tisa, kutoshiriki, ni pigo kwa mafisadi na mipango yao ya kuendelea kuwashikilia mateka wananchi huku wakiendelea kuwaibia na kuwanyonya wao na vizazi vyao hata kwa wanaofanya hivyo kuendelea kurithishana kana kwamba wao ni mali yao binafsi.
          Tisa, baada ya kugomea zoezi hili haramu – bila shaka – wahusika hawatakuwa na kisingizio wala uwezo wowote mwingine wa kuendelea na mipango yao ya kusimika ufisadi nchini. Hivyo, pigo hili la kwanza litawalazimisha kurejesha rasimu ya Warioba ili ifuate utaratibu uliokubaliwa kisheria tayari kuwa katiba mpya yenye mapya kwa ajili ya taifa jipya la Tanzania.
          Kumi, kugomea zoezi hili haramu kutatoa fursa kwa watanzania kupata viongozi wapya baada ya utawala wa hovyo huu uliopo wenye sifa ya kuchakachua rasimu ya Warioba na kuwa mhimili wa ufisadi. Hivyo, kwa kukataa kushiriki kura ya maoni, watanzania watakuwa wanafanya ukombozi wa taifa lao kwa njia ya amani na ya uhakika.
          Tuamalizie kwa kuhimiza watanzania kuwa kushiriki –iwe kwa hiari au kurubuniwa au vyovyote itakavyokuwa – itakuwa ni kuhalalisha ajenda za siri za watu wachache wenye madaraka wanaotaka kuitumia katiba kuwalinda wao na watu wao kwa jinai walizolitendea taifa hili na watu wake. Msiwape wahalifu dirisha la kutorokea. Kuwawajibisha na kujitendea haki ni kugomea zoezi zima. Hivyo, ifahamike wazi kuwa kuwataka watanzania kugomea zoezi hili haramu si uchochezi wala chuki wala siasa bali kukumbushana kuwa kama walitumia wingi wao bungeni tena wa kubadili kanuni, watashindwa nini kuchachua tena? Je sisi tutakuwa ni majuha na mataahira kweli kung’atwa na nyoka kwenye shimo moja mara mbili? Bungeni hatukuwa na uwezo wa kuwazuia. Kwenye kupiga kura tunao ubavu si wa kushiriki –ili wachakachue – ila kuwagomea ili wakose mazingira ya kuchakachua na kupitisha ajenda zao za siri na hilaki. Wananchi gomeeni hiki kiini macho kinachotaka kutumika kuhalalishwa ili baadaye kiwe kitanzi cha kuwanyongea.
 Chanzo: Tanzania Daima Feb., 18, 2015.

4 comments:

Anonymous said...

Ati watanzania gomeni ha ha wewe kweli huna kheri kweli na nchi hii

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Anonymous ama hujui maana ya neno heri au usemacho. Kama unaona katiba pandikizi inakufaa basi hufai na huna heri na taifa letu. Hivyo, acha tunaoona uovu tulitendewa kama taifa tuseme wapo watakaotuelewa. Kushiriki au kugomea kushiriki ni haki yetu kikatiba.

Anonymous said...

Anon....anaonekana ni wale wale wenye akili za wanyama waporini....wanakula chakula bila kulima na pia hawafahamu kuhusu kesho.

Kifupi Anon.. ana-mawazo ya mafupi wakidhani tatizo lao ni pesa tuu kumbe pesa ni kitu cha mwisho katika kuwa na maendeleo yanye mkakati wa muda mrefu.

Binadamu aliye na akili timamu anaishi kwa mikakati ya muda mfupi na mirefu kwa pamoja, siyo mikakati muda mfupi pekee ambayo inafanana na mnyama pori.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Anon siongezi kitu. Umemshindilia huyu mnyama mwitu anavyostahiki. Sishangai. Mafisadi hata ofisi ya mkuu wao huwa wananitembelea na wakati mwingine kurusha vijembe kwangu ila sijali naendelea kupiga tu hadi kieleweke.