Hivi karibuni vyombo vya habari vilimkariri rais Jakaya Kikwete akiwa ziarani Ulaya Magharibi aliposema eti alikwenda kuaga. Kitendo hiki japo kinaweza konakena kama cha kawaida, kina maana zaidi yale yanayoweza kuonekana juu. Kwa wenye akili wanajiuliza: Inakuwaje rais achaguliwe Tanzania, aanze kwenda Ulaya kuaga kana kwamba wapiga kura wake wako kule? Je inakuwaje rais anawapa kipaumbele wazungu badala ya wapiga kura?
Kimsingi, wakoloni walitukomesha kwa jambo moja kuu. Waliondoka lakini wakabakiza ukoloni nyuma. Waliwaachia wakoloni weusi wauendeleze na kuhakikisha Afrika inaendelea kunyonywa na kunyenyekea. Hii ndiyo maana rais anaweza kutoa kipaumbele kwa wazungu badala ya wapiga kura. Na hii si kwa wazungu tu. Jikumbushe watanzania wanavyohangaika kumchagua rais lakini baada ya kuapishwa akadakwa na makundi ya wafanyabiashara tena wengi wa kigeni wasiopiga hata kura.
Kwa vile serikali za kiafrika huishi kwa kutegemea kuombaomba na kukopakopa, wanaozifadhili wana thamani zaidi ya wale wanaozipigia kura. Katika kitabu changu kinachotarajiwa kutoka hivi karibuni nchini Kameruni cha Africa Reunite or Perish, nimeelezea dhana kuwa Afrika lazima iwe tegemezi yenye kujigonga na kuombaomba kama ukuku ambapo kuku huzalisha mayai yenye virutubisho kibao akaishia kutoyala na badala yake akalishwa makapi na nafaka. Haiwezekani Afrika iwe na mali na raslimali nyingi lakini iendelee kuombaomba.
Kwa wanaoujua maana ya uzalendo na uhuru wa kweli, kitendo cha rais kuwapa kipaumbele wafadhili badala wapiga kura, ni ushaidi tosha kuwa Afrika haijawahi kuwa huru. Sikumbuki waziri mkuu wa Uingereza au rais wa Marekani kuja kuwaaga waswahili kwa kuendelea kuipa serikali yake mali ghafi iliyomsaidia kukuza uchumi wa taifa lake. Sikumbuki. Je watawala wetu wanaridhikaje na udhalilishaji huu? Je tutaendelea kuwa tegemezi hadi lini kiasi cha kuridhika na udhalilishaji huu?
Ukiangalia utawala wa Kikwete na ule uliomtangulia, unagundua kitu kimoja, ulithamini wageni kuliko wapiga kura. Sijui ni kwa sababu marais walikuwa mawaziri wa mambo ya nchi za nje au uwezo wa kuelewa hata sijui. Rais mstaafu Benjamin Mkapa alikuwa na furaha alipokuwa nje ya nchi kuliko alivyokuwa nchini. Alifikia mahali kuwakandia waandishi wa habari wenzake wa nchini kuwa huwa hawamuulizi maswali ya kumsisimua na kumfikirisha utadhani alikuwa na usomi wa kuzidi wengine zaidi ya ulimbukeni. Hata akina profesa Ibrahim Lipumba hawawezi kuwa na ulimbukeni kama huu.
Kikwete licha ya kuonyesha kuwa mpiga kura si chochote mbele ya mfadhili, ameacha historia kuwa rais aliyesafiri sana duniani akiandamana na watu wengi tena ambao majina yao yaligeuzwa siri kwa sababu ajuazo. Ni rais ambaye –kutokana na kupenda kusafiri sana –watani wake walimpachika jina la Vasco da Gama. Tofauti na da Gama ni kwamba, Kikwete alikuwa akienda kuomba si kwa lengo la kujikomboa kama alivyofanya da Gama aliyeenda kupora kwa lengo la kujikomba kiuchumi.
Kitendo cha Kikwete kwenda kuaga ughaibuni –hata hivyo –kinabeba tafsiri nyingi. Wapo wanaoona kama ni uugwana wa mhusika kwenda kuwashukuru wafadhili wake kana kwamba nchi inatoweka. Wanasema hii si uungwana bali udhalilishaji kwa vile kinachosaidiwa si yeye bali ni taifa. Hivyo, anapoondoka atakuja mwingine na kumalizia. Wapo wanaoona kam alichofanya Kikwete ni kupenda kutanua tu huku akilipwa per diem na tabia ambayo watani wake wanaona aliishaijenga ya kutokaa ndani. Alichofanya Kikwete kinakupa faida au somo gani, inategemea uko upande gani.
Ila kwa wanaojua utegemezi wa Afrika, kitendo cha Kikwete ni kikwazo kwa uhuru na umoja wa kweli wa Afrika kwa vile kinaonyesha alivyoridhika na kuombaomba na kukopakopa. Katika kitabu nilichotaja hapo juu kuna sura nzima ya begging will nary build Africa au uombaomba hautaijenga Afrika. Kwani watawala wanapaswa kuwa na mipango na mikakati ya kutumia raslimali kuinufaisha na kuiendeleza Afrika badala ya kutegemea kuombaomba. Katika sura hiyo mwandishi anaonyesha namna watawala wa Kiswahili wanavyopenda kuombaomba na kukopakopa bila kujali maslahi ya mataifa yao kwa vile wengi hawatakuwa madarakani wakati wa kulipa. Mwandishi anawaeleza watawala wa kiafrika kama wakoloni weusi walitumia mfumo wa jambazi wa kiingereza Fredrick Lugard wa gawanya utawale kuwatawala, kuwanyonya na kuwauza ndugu zao nao wakijiuza pia. Anatoa mifano mingi kwenye when da Gamas are in the state houses akionyesha marais wanaosifika kwa kusafiri sana barani. Mwandishi analinganisha ziara za viongozi wa nchi tajiri na watawala wa nchi maskini na matanuzi yao.
Ingawa rais Kikwete ana uhuru wa wapi na nani aanze kuaga, kitendo cha kuwapa kipaumbele wafadhili au tuseme wazungu haikiwezi kuwafurahisha wapiga kura waliomwezesha kuwa pale tena si kuwa pale tu bali kumwajiri. Ni bahati mbaya kuwa kwa Afrika rais si mtumishi wa umma tena bali mtumikishaji wa umma. Maana haiwezekani wakati wa kustaafu mwajiriwa akaenda kuwatembelea marafiki zake kabla ya mwajiri ambaye humpangia hata malipo baada ya kuondoka kazini. Kikwete huyu huyu anayewapa vipaumbele wazungu anasahau kuwa akistaafu ataendelea kutunzwa na kulipwa fedha ya wapiga kura na walipa kodi hawa hawa anaowapa kipaumbele cha mwisho. Kama kuaga ni dili basi ningekuwa Kikwete ningeanzia majimboni nikamalizia Ulaya kuliko kufanya tofauti.
Chanzo: Dira
2 comments:
Tutegemee karumangira atawashawishi hawa watu wa magharibu nao waje kutuaga watakapokaribia kutoka madarakani!
Anon, ni bahati mbaya kuwa aliyemroga Kikwete alikwisha kufa. Tuombe amalize muda wake atokomee mwana kutokomea.
Post a Comment