Kila wanapoandika jina lake, waandishi wengi, hasa wanaomuunga mkono, humueleza Edward Lowassa kama waziri mkuu mstaafu wakati siyo. Sijui kama wahusika wanafanya hivyo kwa makusudi au bahati mbaya au ujinga kwa sababu ya ujinga wa kawaida. Mstaafu ni mtu ambaye amefanya kazi na kufikia ukomo wa kazi fulani kwa mjibu wa sheria. Kamusi ya Kiswahili Sanifu ya Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI, 1981) inatoa maana ya kustaafu ikisema ni kitendo cha, “kuacha kazi ya kuajiriwa baada ya kufikia umri au muda maalamu uliowekwa,” (Uk, .264).
Kwanza, kwa maana ya kamusi tajwa, Lowassa si mstaafu kwa vile –chini ya sifa ya pili ya, “kufikia …muda maalumu uliowekwa” hakufikia ukomo wa muda maalum wa uwaziri mkuu wake ima baada ya kumalizika muda wa ukomo wa awamu aliyokuwa akiitumikia kama itakavyotokea kwa waziri mkuu wa sasa Mizengo Pinda hapo Decemba, au kubadilishwa kazi na mamlaka iliyomteua yaani rais. Lowassa alilazimika kuachia ngazi na si kujiuzulu kama wengi wanavyosema baada ya kubainika kuwa alishiriki kuingiza kampuni la kitapeli la Richmond lililoiba fedha nyingi ya umma.
Pili, kwa wanaojua mazingira yaliyomsababisha Lowassa kuondoka madarakani tena mapema, watakubaliana nasi kuwa hakidhi sifa ya kuitwa waziri mkuu mstaafu. Tumeishabainisha hapo juu kuwa aliondolewa na kashfa ya Richmond. Mstaafu si mfukuzwa bali mtu anayeagwa na mamlaka iliyomwajiri huku akipewa masurufu na marupurupu kwa kufanikisha kazi yake vizuri.
Je ustaafu au kutokustaafu kwa Lowassa kuna umuhimu gani kwa taifa? Kustaafu au kutostaafu kwa Lowassa ni muhimu, kwanza, kwa sababu amekuwa akilipwa malipo yote ya ustaafu wakati hastahili. Kwa lugha nyingine, Lowassa amekuwa akiliibia taifa tangu mwaka 2008. Je tangu wakati huo Lowassa ameliingizia hasara taifa hasara kiasi gani ukiachia mbali ile aliyolisababishia kwenye kashfa ya Richmond ambapo watanzania walikumbwa na mgao mkali wa umeme pamoja na kulanguliwa umeme?
Si kwamba Lowassa hajui kuwa hastahili malipo na maslahi anayopewa. Anajua fika. Ila kwa vile fedha ni tamu na kilichomuondoa mamlakani kiliepusha anguko la chama chake yaani Chama Cha Mapinduzi (CCM), amekuwa akilipwa fedha hiyo kinyume cha sheria. Je mtu wa namna hii anayeweza kuingiza makampuni tapeli na kupoteza fedha za umma halafu akaendelea kupokea mamilioni ya shilingi kinyume cha sheria anaweza kulifaa taifa?
Nadhani hata Makongoro Nyerere aliposema kuwa baadhi ya wahusika ni vibaka na vidokozi alijua alichokuwa akisema na aliyemlenga anajulikana. Haiwezekani Lowassa akaendelea kupokea malipo asiyostahiki akawatendea kodi walipa kodi tena maskini wa Tanzania.
Kwa hiyo, katika maswali makuu ambayo watanzania wanapaswa kumuuliza Lowassa ni: Kwanini amekuwa akipokea malipo asiyostahiki? Je anajua nini kuhusiana na kashfa nzima ya Richmond?
Swali jingine muhimu kuhusiana na Lowassa linapaswa kwenda kwa serikali ya CCM. Nalo ni: Kwanini ilimzawadia mamilioni ya shilingi ya fedha ya umma Lowassa bila kujali kuwa hakustahili na kufanya hivyo ni kinyume cha sheria? CCM lazima iwe na kibarua kikubwa cha kujieleza hasa ikizingatiwa kuwa hata wale watuhumiwa wakuu wa Richmond hawajawahi kufikishwa mahakamani wala kuchukuliwa hatua zozote za kisheria zaidi ya baadhi yao kupindiwa sheria na kuendelea kuhomola mamilioni kama anavyoendelea kufanya Lowassa.
Kimsingi, kama wapiga kura na watanzania watakuwa makini, Lowassa ni mojawapo ya sababu zinazoweza kusababisha kushindwa vibaya CCM kama wachambuzi wengi walivyobainisha.
Kwanza, watanzania bado wanakumbuka madudu yake tangia zama za marehemu baba wa taifa Mwl. Julius Nyerere aliyetaka Lowassa na Jakaya Kikwete –kama hawakuwa mafisadi na vidokozi –walikuwa wamepata wapi fedha ya kukodi ndege kwenda na kurudi Dodoma kuchukua fomu za kugombea kupitishwa na CCM kugombea urais mwaka 1995.
Pili, Lowassa atazusha kimbembe na kufanya kazi ya kuchaguliwa CCM iwe ngumu kutokana na hili la kuendelea kuchotewa mamilioni kinyume cha sheria. Hivyo, kwa lugha rahisi ni kwamba Lowassa ni mzigo mkubwa tu wa CCM. Wampitishe wasimpitishe, madudu yake yana mchango mkubwa katika kuiangusha CCM.
Nadhani, kwa kutambua hili, ndiyo maana CCM wenyewe –kupitia mwenyekiti wao rais Kikwete –wameanza kumbeep kwa kuonyesha wazi kuwa hawatampitisha. Kwa wanaokumbuka maneno ya Kikwete kwenye hotuba yake ya hivi karibuni akisema kuwa CCM ikifanya mchezo inaweza kwenda na maji, watakubaliana nasi kuwa mojawapo wa walengwa na wahanga wakuu alikuwa Lowassa hasa pale Kikwete alipoongelea kupitisha mtu anayekubalika ndani na nje ya chama. Alisema wazi kuwa CCM isiangalia urafiki au kujuana. Kwani inaweza kuangukia pua. Katika watangaza nia wote wa CCM ni nani rafiki mkuu wa Kikwete kama si Lowassa? Je ni nani madudu yake yameanikwa sana sana zaidi ya Lowassa?
Tumalizie tulikoanzia, kwa mujibu wa maana ya Kamusi ya Kiswahili fasaha Lowassa si waziri mkuu mstaafu bali waziri mkuu wa zamani. Pia Lowassa hana stahiki kisheria kulipwa marupurupu na haki za ustaafu. Hivyo, kuendelea kulipwa haki hizi licha ya kuwa wizi na matumizi mabaya ya fedha za umma ni kuvunja sheria.
Chanzo: Tanzania Daima Juni 21, 2015.
No comments:
Post a Comment