Baada ya lisirikali kugwaya hekalu la mchunaji mwana siasa Gettie Rwakatarehe na ule mjengo uaji wa uhindini, mlevi anapanga kujenga mhekalu wake kwenye maeneo yaliyozuiliwa hasa kule Mbezi kwa wazito. Ili nisisumbuliwe lazima kwanza niongee na mheshimiwa Esta Ulaya asininange mjengoni kam alivyomtolea uvivu Rwkatarehe. Maana kama kaya hii isingekuwa na wenyewe hasa mafwisadi kama Rwakaterehe, kwa jinsi muishiwa huyu alivyosiliba, hili hekalu lingedondoshwa siku hiyo hata kama ni kazi hii kufanyika usiku lakini wapi!
Unajua muishiwa Ulaya alinangaje? Ngoja nimnukuu nisionekane ima namzushia au kuleta rongorongo. Alizoza tena mchengoni tena mbele ya mama Kipaza Sauti na kamera zote za runinga hata zile za mablog uchwara, “Jumba la Shilingi bilioni moja lile bomoeni…mnasema sheria ni msumeno, huu msumeno unakata kwa baadhi tu huku kwa wengine unakuwa butu?” Japo aliyosema muishiwa yana mashiko, namtaarifu kuwa aende akatambikie ndipo asikilizwe vinginevyo anatwanga maji usawa huu ambapo ngedere ndiyo waliokabidhiwa shamba la mahindi.
Kumbe muishiwa Ulaya hakujua kuwa sheria za Bongolalaland ni kama treni –hukata upande mmoja wa wachovu huku ukipuliza upande wa pili wa wanene kama akina Rwakaterehe, Rugemalayer, Singasinga na mafisadi wengine. Ukitaka kujua kuwa kaya yetu ni ya kitapeli na rongorongo, uliza ule mkwara wa yule mchunaji Gwajimama umeishia wapi. Jamaa kawakati chochote kitu wanene wakaamua kumgwaya na kufyata mkia. Hebu niulizie hao ndata waliostukia ujambazi wa huyu mchunaji kiasi cha kutaka awasilishe kila nyaraka za ukwasi wake na asifanye hivyo. Acheni wachovu waliwe wanajiona kwa vile hataki kulianzisha lau kieleweke au pasitoshe kama si kuchimbika bila jembe.
Kama wajalaana wametuibia njuluku za escrew na kutu-screw mchana kweupe na wakaendelea kutesa na kutanua unategemea nini? Hamkumsikia fisadi mwingine eti naye anayegombea urahis akiwasifu akina Ni Ziro Kadamage kuwa ni matajiri wa kupigiwa mfano wakati ni majambazi ya kawaida yaliyojificha nyuma ya ukwasi na vyeo?
Hivyo basi, kwa vile dili langu la kuuza na kusambaza mibwimbwi na kufanya ujambazi mwingine linalipa, basi nitaangusha bonge ya hekalu tena karibu na lile la Rwakatarehe nione watanifanya nini. Nani mara hii kasahau mhekalu mwingine wa Heze Maige wa mabilioni ya njuluku ambao hauna maelezo? Nani ameishamweka kikaangoni aeleze alivyopata hayo maelfu ya dolari tena akalipa kashi. Mara hii mmesahau hata zile tambo za kurejesha njuluku za ughaibuni! Zimeishia wapi? Sana sana wajalaana na majambazi yanakamua na kuendelea kuficha nyingine zaidi huku wachovu na walevi wakiendelea kufungwa kamba kuwa lisirikali litarejesha njuluku wakati kiendacho kwa mganganjaa huwa hakirudi.
Ili kunogesha mchezo, nitavamia eneo wazi liwe la shule au mtaa mimi sijali. Nitalivamia kulitwaa na kuangusha kitu cha haja halafu nione watanifanya nini. Kama waliiba na kuuziana nyumba za kaya na wakaendelea kujikeshachekesha eti wanapambana na ufisadi wakati wanaupamba, nani aogope kuvamia viwanja vya wazi na kufanya kweli kama walivyofanya akina Rwakatarehe na majambawazi wengine?
Ili kuhakikisha project yangu inapeta, lazima niwaite wajalaana wa site na kuwakatia kitu kidogo wahakikishe ima wananighushia hati za kumilki kiwanja au wanafanya vitu kinyume cha sheria kama wenzao wa kwenye lisirikali wanavyofanya kwenye mikataba ya uchukuaji uitwao uwekezaji ili nikienda kwa pilato nipewe haki.
Siku hizi ujanja si kufuata sheria bali kuzivunja. Ujanja si kuwa muadilifu bali mbadhilifu. Wale wanatakaoshikilia uadilifu watachekwa hata na kunguru usawa huu ambapo kaya imegeuka shamba la bibi na chizi ambapo kila kinyama mwitu huja na kujichumia na kuukata na kutanua. Anayebisha aende akaulize wazee wa site ilipo kampuni ya wanuka jasho ya UdA. Si habithi mmoja akitumiwa na vigogo na watoto wao ameitwaa na kuimilki huku wazee wa site wakikatiwa chao na mchezo kuisha. Nasikia kuwa jamaa hawa majambawazi wakubwa wanyemelea mradi wa mangwala ngwala yaendayo kasi jijini ili wazidi kutengeneza njuluku. Kama yote haya yanafanyika na hakuna anayenyea debe, niogope nini kuangusha hekalu langu ugogoni na uzitoni kama Rwakatarehe?
Hata hivyo akina Rwakatarehe wana bahati ya mtende. Maana kama nisingeamua kucheza mchezo wao nikaamua kuwa upande wa pili ningewahamasisha walevi tukaenda kuangusha ule mjengo wenyewe bila kujali nani wala nini. Kwa vile ukienda Roma fanya kama waroma, uzalendo umeiniishia na kuamua kuwa kibaka na jambazi kama wao. Maana ukiangalia walevi ninaowapigania na kutaka waache kuliwa na kaya yao kubakwa, unapata kichefuchefu. Wadude wenyewe hawajitambui wala kutambua mazonge wanayoletewa na ngurumbili wenzao wanene. Sasa mimi niwafanyeje kama wameamua wenyewe kujirahisi na kuliwa mchana tena wakijiona? Hivi jamani, hawa wadude washikwe wapi ndipo wastuke?
Kujua kuwa walevi na wachovu wataliwa sana na kuendelea kufanyiwa kitu mbaya hebu soma maneno haya na Nipe Mapepe Ninaye yule kidhabi mkuu wa rongorongo chamani. Alisema, “Rangi inayoenda Ikulu ni hii (anaonyesha shati lake la kijani ambayo hutumiwa na chama hicho). Tuna uhakika na ushindi wa Rais. Kwa namna yoyote ile, CCM itarudi Ikulu hata kama ni kwa bao la mkono... bao ni bao tu ili mradi refa hajaona.” Hili ni tangazo kuwa Nambari wahedi itachakachua uchaguzi na kuendelea kuwashika mateka walevi. Pamoja na makufuru haya, umesikia nani akiingia mtaani kupinga njama hii chafu. Ama kweli walevi ndiyo waliwao. Msipobadilika mtaliwa sana wakati mimi nikijinoma kwenye hekalu langu ninalopanga kuangusha kama Rwakatarehe. Nyie liweni lakini mimi simo!
Chanzo: Nipashe Juni 27, 2015.
No comments:
Post a Comment