Baada ya kushudia mshike mshike, kasheshe na patashika ambapo kila mtu anautaka urahis wa kaya hii, Kijiwe kwa taadhima kimeniomba nigombee urahis. Sambamba nami, Kijiwe kimependekeza Msomi Mkata tamaa awe mgombea wangu mwenza huku Mijjinga akipewa cheo cha waziri mkuu kama tutatoboa. Pia kwa vile urahis ni ufalme wa mlango wa nyuma, Kijiwe kimenipa jukumu la kuhakikisha wanakijiwe wote wanapata ulaji kuanzia ubalozi, uwaziri, ubunge wa kuteuliwa, ukuu mkoa na wilaya na ujumbe kwenye bodi za ulaji.
Mgosi Machungi ndiye aliyetoa hoja hii. Analianzisha, “Jamani, nadhani sote timeona jinsi mafisi mafisadi hata na vigetemezi vyao wakiwania kutitawaaa. Kwa vie nasi hatiko nyuma, napendekeza titeue mwenzetu mmoja agombee na asiwe mwingine ila Mzee Mpayukaji.” Ananiangalia kwa kutabasamu nami natikisa kichwa na kutabasamu.
“Usemayo ya kweli ntupu. Maana naona hata vitoto vilivo na nepi eti navyo vyautaka! Wallahi sasa imekuwa fujo tupuu. Heri nasi tuwe na ntu wetu ati.” Anachangia Mpemba huku akitabasamu na kukamua kahawa yake.
Kapende anatia timu, “Wazo hili la mbolea na hapa mahala mwake. Maana hatuwezi kuruhusu vikongwe vilivyokwishaishiwa, vichanga vilivyovaa nepi tena za kununuliwa na wazazi wake vigombee nasi tuwe watazamaji. Mkiogopa mie nitajitosa muda si mrefu. Hata hivyo, namuunga mkono mzee Mzima najua atatuvusha walipotuzamisha hawa wajalaana wanaojitiatia na kujiletaleta wakati tulishawastukia.”
“Kwa hali ilivyo, tukiteua mchovu mwenye sifa kama mzee Mpayukaji bila shaka tutapeta na kupetuka hasa usawa huu ambapo Chama cha Mafisi na Mafisadi (CcMM) kimeshikwa pabaya tokana na kila mmoja kuutaka ulaji rahisi kupitia urahis.” Anachomekea Mzee Maneno.
“Naungana nawe mia kwa mia. Wale hawana sera zaidi ya sera moja tu yaani vurugu za kifisadi. Kwa vile sisi tunajulikana tangu zama na enzi, tuna uwezekano mkubwa wa kukamata Dola halafu tukalaga madola au vipi?” Anasema Mipawa.
Mheshimiwa Bwege anakatua mic, “Kama sura mzee unayo tena ya nguvu.” Ananigeukia na kusema, “Wewe ni bonge la handsome tena asiyechekacheka wala kupayuka hovyo. Kama ni elimu wewe ni profesa na kama ni sera, wewe ndiyo alpha na omega hapa kayani maana hata machache waliyofanya hawa waduwanzi wameiba na kukopi sera zako hapa Kijiweni. Tusiruhusu hawa wafanya vurugu na mafisadi na vichanga watujazie mbu. Zao zilishapita zama gani?”
Msomi Mkatatamaa aliyekuwa anamtext mtu wake anakatua mic, “Nilikuwa nawaza kutoa hili wazo. Mgosi ameniwahi. Hata hivyo, hakuna tatizo. Nakubaliana na michango ya wajumbe kuwa lazima tujiandae kuchukua kaya. Napendekeza tuwakaribishe na wapingaji watuunge mkono tuchukue hii kitu ili tuonyeshe nini maana ya dhana nzima ya utawala bora na wa sheria. Lazima tukuchukue hii kitu na kuwatupilia lupango hawa mafisi na mafisadi wanaokula kaya kiasi cha kula kwa miguu na mikono huku –kama mainzi –wakitapika, kunonihino na kuogelea kwenye sahani hiyo hiyo wanamokula.”
Anapiga chafya na kuendelea, “Hatuwezi kuacha huu upuuzi ukaendelea. Hivyo, basi lazima tujiandae kuzungukia vijiwe vyote kuhakikisha kila mmoja anapiga kampeni na kushinda ki-Tsunami.”
Sofia Lion aka Kunungaembe hangoji. Anamchomekea Msomi, “Kumbe sera zenu ni za kulipiza visasi! Nilidhani mna sera lau za kuendeleza kaya kumbe mambo yenyewe michosho!”
Kabla ya kuendelea, Mbwamwitu anamchomekea Sofi, “Da Sofi hapa umepoteza pwenti. Hivi ulidhani unaweza kusafisha nyumba kwa kusukumizia uchafu ndani au nje?”
Kabla ya kuendelea Mijjinga anachomekea, “Sidhani kama Sofi amemuelewa Msomi. Tunachofanya hapa ni kutaka kuondoa ufisadi once and for all. Hivyo, lazima afungwe ngurumbili hapa. Hivyo, hatutaomba msamaha kwa hili sana sana kulitekeleza tena ndani ya siku mia za kuwa kwenye ulaji.”
Kanji naye hajivungi. Anachomekea. Maana leo ni siku ya kuchomekeana kama vile mafisadi wanavyochomekeana wakitafuta urahis. Anakula mic, “Hebu seme kweli jamani. Je veve naweza kamata fisadi yote natupa lupango? Kwanini hapana samehe yeye dugu yangu?”
“Kanji isitake kitiudhi. Eti tiwasamehe? Kama kusamehe dii basi kasamehe Bombei akini si kwenye kaya hii. Dawa ya inzi ni kumuua ili asiozeshe kidonda.” Machungi anaongea kwa ukali kidogo huku akitupa kipisi cha sigara kali.
“Kama sera zenyewe ndiyo hizi hampati kitu ng’oo.” Anasema Sofi kama mtu anayezodoa.
Kapende anamchomekea, “Wewe ukitunyima wengine watatupa. Bania usibanie wapo wanaotuzimia na kutuelewa. Hivyo, ngoma lazima isonge na washenzi wote na majambazi lazima waipate utake usitake utoe usitoe.”
“Mheshimiwa inatosha. Hiyo dozi uliyompa da Sofi nadhani inamtosha.” Anachomekea mzee Maneno.
Wakati nikiwa sina hili wala lile si Msomi akanigutua! Alisema, “Mzee sasa mpira uko kwako.” Alinikazia macho na kuendelea, “Lazima tuanze kujipanga lau tuwakomboe wachovu na walevi. Hivyo, ningeshauri tukitoka hapa tukutane mimi nawe ili tuweze kuangalia vipaumbele, sera, hali halisi na mambo mengine hasa namna ya kutumia mitifuano ya mafisi kuwamaliza. Hapa tunamkaanga samaki kwa mafuta yake au vipi?”
Kabla hata sijajibu si ikaji misafara ya watangaza nia wakitaka tuwadhamini. Tuliwarushia vikombe vya kahawa wakatimka kama vibaka.
Ndipo Mbwamwitu akasema. “Kum…nina zenu wana hizaya nyie mna bahati tungewafanyia kitu mbaya.”
Chanzo: Tanzania Daima Juni 17, 2015.
No comments:
Post a Comment