Baada ya songombwingo na kila aina ya
ngurumbili kutangaza nia ya kuwania ulaji wa dezo na rahisi yaani urahis,
Kijiwe –kwa furaha –kimekaa kama kamati na kudurusu mtifuano na mshike mshike
huu wenye kila aina ya patashika kasheshe, vitimbwi na mitimbwiriko.
Mpembe anaingia akiwa na gazeti la Toboa. Anaamkua na kumwaga mada mezani. “Yakhe
mmesikia hii mipasho ya wasaka urahis na ulaji wa dezo?”
Kapende anadakia, “Hawana lolote hawa.
wengi mafisadi wa kunuka japo wanajifanya wana sera za kutukomboa wakati moyoni
wana mipango ya kutuangamiza kama hawa wanaoondoka.”
Mbwamwitu anachomekea, “Wengi
viherehere kama alivyosema mwana wa Mchonga japo naye hafai.”
“Wengine wanafuata mkumbo ukiachia
mbali kutengeneza mazingira ya kutaka wawemo kwenye ulaji kama mmoja wao
atapenya. Nionavyo mwaka huu hapenyi mtu. Maana kwa wanavyochafuana lazima wapingaji
wachuke waweke waa kama watakuwa makini kutumia huu mtifuano.” Anasema Mijjinga
huku akibwia kahawa yake.
Mgosi anatia timu kwa chati, “Hakuna
sehemu wameniacha hoi kama yule
Kimbelembele Mwehujuu Michembe kusema eti atativusha. Kumbe timekwama
bahaini. Ina maana huyu dogo anakii kuwa Njaa Kaya ametizamisha? Makubwa haya
wagosi tate nane tate nane.”
Msomi Mkatatamaa aliyekuwa akibofya
ki-Samsung Galaxy 5 anaamua kula mic, “Wote wamepayuka hakuna aliyeniacha hoi
kama Freddie Sumayi aliyekumbuka blanketi wakati kumekucha. Eti anasema kuwa
Chama Cha Maulaji kikipitisha fisadi atajitoa. Mbona amechelewa. Kama chama
chenyewe ni genge la mafisadi anategemea huyu msafi kitampata wapi.”
Kabla ya kuendelea mheshimiwa Bwege
anamchomekea, “Naona huyu buda anaweweseka hasa ikizingatiwa kuwa hawezi
kupenya kutokana na kuwa na kashfa ya kuuza nyumba za wachovu wakati wa utawala
wake na Chinga Dugong Ben Makapi. Kama anataka kufanya kweli angeishajitoa
zamani gani! hata hivyo, sishangai. Hawa ni wanasiasa ambao –mara nyingi –huwa hawana
tofauti na vyangu kimaadili na madili.”
Msomi anaendelea, “Hakuna aliyeniacha
hoi kama profwedheha Muongo kusema eti ataongoza kaya kisayansi. Sijui alisahau
kusema kifisadi au kiescrow akasema kisayansi? Huyu kama kuna kinachomfaa si
kingine bali kwenda kwa bosi wake Jimmy Lugemalayer na Singasinga wakamtumie
kule.”
Kanji anadandia, “Kama yeye kwenda
escrow tumia yeye si tapata aibu? Veve sema witu zito sana Somi. Ile yote
nashiriki escrow hapana paswa gombea rahis jamani.”
Sofia Lion aka Kanungaembe aliyekuwa
na usongo wa kuchangia anakula mic, “Jamani tunapaswa kuwa makini tunapotoa
shutuma. Hivi kuna mtu ana ushahidi dhidi ya mheshimiwa huyu au fitina na chuki
binafsi?”
Msomi hangoji mwingine ajibu. Anakula mic
huku akitabasamu na kumwangalia Sofi kama kwa dharau hivi na kusema, “Da Sofi
unataka ushahidi gani? kwani alifukuzwa ulaji kwa sababu gani na kwanini? Je huu
si ushahidi tosha sawa na ule uliomfukuzisha Eddie Luwasha ambaye kwenye
kigwena chake aligwaya kugusia Richmonduli akidhani sisi tutasahau?”
Inaonekana Sofi kashikwa sehemu nyeti.
Kwani badala ya kutoa macho na kunung’una hajibu maswali ya Msomi.
Mpemba anarejea,”Wallahi usemayo Nsomi
mazito kweli kweli. Hawa wajalaana wadhani sisi mataahira na wasahaulifu kiasi
cha kujitiatia na kujiletaleta eti tuwape ulaji watuuze zaidi?”
Mzee Maneno anachomekea, “Ami eti
wanajitiatia na kujiletaleta? Au ndicho hicho kimbelembele cha vidokozi
anachosema Makorongo Mchonga?”
Mipawa anatia timu, “Wajameni
mwashangaaga kusikia hii mipasho. Hamjui kuwa wakati waliozoea kula wenzao
kuliwa umefika? Watabwabwaja mengi na kuvuana nguo sana tu. Nadhani laana ya
kukwanyua njuluku za wachovu inaanza kuwaandama kiasi cha kumalizana wao kwa
wao. Hatuna haja ya kusherekea anguko hili la ghafla la genge la mafisadi.”
Sofi anamkata jicho la chuki lakini hasemi kitu.
Msomi anarejea, “Usemayo mheshimiwa
Mipawa ni kweli tupu. Hamuoni wanavyoanza kugeukana kiasi cha wale waliojidai
ni marafiki wa mtukufu tena si wa kukutana barabarani wanavyolialia kama
vichanga? Huoni kila mmoja anavyojitahidi kumtupia Njaa Kaya mzigo wakati
walikula na kuvurunda wote. Namuonea huruma rafiki yangu Njaa Kaya ambaye
alionywa kuwa ufisadi haulipi akaendeleza urafiki. Usishangae wakabwagwa na
jamaa wakaishia lupango kutokana na ujambazi na ufisadi waliotenda. Hakuna aliyeniacha
hoi kama Makorongo kutaja kabisa kuwa kuna wajaalaana wana mahekalu Dubai na
kwingineko. Nadhani kazi sasa ni kwa wapingaji kupeleka ukweli huu mchungu kwa
wachovu vijijini. Nadhani kilichoikuta Kanu kule kaya ya nyayo kinainyemelea
CcM. Nadhani tuombe Mungu wazidi kuvuana nguo na kujitiatia kujua ili umma
ustuke na kuwapiga chini.”
Mbwamwitu anachomekea kwa utani, “Eti
wanavuana nguo na kujitiatia! Ama kweli mmewachoka jamaa hawa!”
Msomi anarejea, “Jamani haya si maneno
yangu. Ni maneno ya Makorongo Mchonga aliyesema kuwa wengine wana kimbelembele
na kiherehere asijue ni wote. Hivi ulitegemea nini jitu kama Dume la Nyani
Steve Wahasira kutia timu wakati hana jipya wala lolote au kitegemezi cha Mgosi
na huyu tabibu Kingwalangwala? Acha wapigane ngwala na kuchimbiana mikwara huku
wakivuana nguo na kumwaga mtama kwa kuku tufaidi.” Anamgeukia Sofi na kuuliza, “Mbona
akina mama hawatii guu au wanaogopa kuvuliwa nguo? Ama kweli vita ya kunguru ni
neema ya panzi kama watakuwa makini.”
Kijiwe kikiwa kinaendelea si ukapita
msafara wa watangaza nia wakitaka kutoana mcho. Acha tuwashangae na
kuwashangilia tukiomba waendelee kutupa uhondo!
Chanzo; Tanzania Daima Juni 10, 2015.
No comments:
Post a Comment