How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Friday, 5 June 2015

Mlevi atangaza kugombea urahis


          Baada ya kuona kila ghasia kuanzia vidokozi, mafisadi, viherehere na wachovu wakitangaza nia za kuwania urahis, na Mlevi rasmi najitupa kilingeni ili niwatoe jasho. Sigombei kwa vile rais umegeuka ulaji rahisi na njia ya kutajirika haraka kwa rahis na watu wake. Nafanya hivyo kutokana na kuwa na sifa na nia ya kuwa rahis tangu nikiwa kwenye tumbo la bi mkubwa wangu.
Bila kuchelewesha wala kuzungusha, zifuatazo ni sera zangu:-
Mosi, nitaamuru Mjengo utunge sheria ya kumlazimisha rahis anayeondoka kunipa orodha za majambazi, wauza unga, mafisadi na wahalifu wote alizo nazo ili nizishughulikie ndani ya wiki moja ya kuwa kwangu ikulu.
Pili, nitapiga marufuku uwekezaji wa kichukuaji kwa kufumua mikataba yote iliyomshinda rahis anayeondoka.
 Tatu, nitahakikisha nawanyongelea mbali mafisadi wa EPA, Richmonduli, escrow, Meremeta, SUkiTA, Mwanakaya Gold na wale wanaoua watu wenye ulemavu wa ngozi. Nataka ndani ya mwezi mmoja vitu hivi viwe historia kwenye kaya. Sambamba na hili nitapiga marufuku uganga wa kienyeji kayani bila kusahau uchunaji unaoitwa uchungaji na ushehena unaoitwa ushehe.
Nne, nitazuia kutoa uraia wetu kama njugu pamoja na paspoti zetu kugeuzwa njugu kwa kuuzwa kwa wahalifu wa kimataifa kwenda kudhalilisha kaya yetu kama ilivyo. Wote wanaojulikana kujihusisha na hujuma hili kwa kaya wajiandae kunyongwa na kutaifishwa mali walizochuma kupitia biashara hii kichaa.
Tano, nitapiga marufuku kusafirisha wanyama hai na waliokufa na kufufua ile kesi ya utoroshaji wanyama. Adhabu ya watakaopatikana na nyara za kaya ni kunyongwa.
Sita, nitaanzisha kiwanda cha kuchambua tanzanite na kuhakikisha madini na vito havivushwi kama ilivyo.
Saba, nitapiga marufuku safari za nje za hovyo kuanzia kwangu na maafisa wote wa serikali. Wale waliozoea kwenda nje kufanya utalii kwa kujidai wanatangaza utalii lazima warejeshe njuluku zetu. Nani anataka rahis Vasco da Gama usawa huu? Wale wote waliokwisha tumia njuluku za kaya kufanya utalii nje wajiandae kunyea debe bila kujali wadhifa aliokuwa nao ngurumbili hata awe rahis.
Nane, nitapiga marufuku my wife aka first lady kuwa na NGO ya uongo na ukweli. Wale waliokwisha kuwa nazo watalazimika kurejesha njuluku zote walizochuma kupitia NGO hizi na kufungwa jela miaka 50 bila msamaha wangu.
Tisa, nitapiga marufuku waishiwa kulala mjengoni. Watakaobainika watafukuzwa uishiwa right away baada ya kupigwa bakora hamsini ili wakawaonyeshe wake au waume zao makalio yaliyovimba
Kumi, nitaunda serikali ndogo inayoendana na uchumi wa kaya kwa sharti kuwa yeyote mwenye uhusiano wa aina yoyote nami hataruhusiwa kuwa kwenye serikali yangu. Sambamba na hili nitafuta wilaya na mikoa vilivyoanzishwa kishikaji bila kujali uwezo wa kiufedha na kiuchumi.
Kumi na moja, nitashughulikia vigogo na fito wote waliofoji vyeti vya kitaaluma na kuhakikisha wanafungwa maisha ili liwe somo kwa wengine.
Kumi na mbili, nitarejesha njuluku zilizofichwa Uswizini na kwingineko kwenye mabenki jambazi ya ughaibuni. Mzee wa vijisenti vya ugolo na vijisenti wajiandae kupelekwa majirini huku akina Kagoda wakipigwa na kuchomwa moto kama vibaka.
Kumi na mbili, nitarejesha maadili ya utumishi wa umma na kufuta madili yaliyopo sasa.
Kumi na nne nitahakikisha kila mtumishi wa umma na wanakaya wote wanatangaza utajiri na umaskini wao kwa kufanya kuwa lazima kujaza ripoti za kodi na mapato kwa kila mwanakaya kila mwaka. Atakayekaidi amri hii atafungwa maisha na kutaifishwa mali zake. Kadhalika nitaamuru utunzaji wa fedha, mali na raslimali za umma vinapewa kipaumbele. Kwa mfano, hakuna kutumia simu za umma kutongozeana au kuacha taa zikiwaka maofisini. Idara itakayokuwa na bili kubwa ya umeme italipia bili. Pia nitahakikisha nafunga mita za ruku kwenye ofisi za umma huku walevi wakienjoy umeme bure. Kadhalika mgao utakuwa historia kayani mwetu.
Kumi na tano, nitahakikisha upimaji wa afya za watumishi wa umma kuwa lazima kila mwaka. Na baada ya kufanya hivyo, matokeo ya afya za wazito yatatangazwe kwenye gazeti la sirikali na kunukuliwa na magazeti yote isipokuwa ya udaku ambayo napanga kuyapiga marufuku.
Kumi na sita, nitafufua elimu kwa kurejesha kimombo kuwa lugha ya kufundishia kwenye shule za upili na vyuo. Pia ushenzi wa kutumia kitabu kimoja shuleni nitaufutilia mbali. Sambamba na hili nitahakikisha wote watakaowadunga pregnancy wanafunzi watafungwa maisha. Nyodo ya kwanza nitafunga guest houses zote zinazotumika kama short time facilities za uchangudoa iwe ni kwa wanafunzi au watu wengine.
Kumi na saba, nitawafunga walioua elimu huku nikiongeza mishahara ya walimu na kuamuru elimu itolewe bure kama wakati wa gwiji Mchonga ambaye alikuwa mshirika na rafiki yangu mkubwa.
Kumi na nane, nitahakikisha wote wanaomwaga njuluku kama hongo kwa walevi na wachovu wanafungwa maisha hata kama watashinda kwenye uchaguzi.
Kumi na tisa, nitavunja tume ya uchakachuaji na kuiunda upya kwa kushauriana na vyama huku nikiiondoa Takokuru chini ya ofisi ya rahis ili ipate nguvu na meno vya kuwashughulikia wezi, majambazi na mafisadi katika kaya.
Ishirini, nitafunga vyombo vya habari vinavyochochea uharibifu wa mila za kichovu. Kuanzia siku nitakayoapishwa mambo ya kuvaa hereni kwa wanaume au milegezo na kuonyesha video chafu almaaruf kama pila kwishinei. Wote wanaojihusisha na kadhia hii wajiandae kuozea jela.
Ishirini na moja, nitakagua barabara zote zilizojengwa kijambazi kuangalia ukubwa wake na kama zinafikia viwango vilivyokubalika. Watakaogundulika kuiba njuluku ya umma kwa kujenga barabara zilizo chini ya kiwango ni halali yangu, wallahi nitawanyonga tu. Maana nina usongo na kaya yetu iliyobinafsishwa kwa manyani na mafisi, mafisadi uchwara.
Kwa ufupi nina mengi ya kufanya. Mengine nitayaeleza baada ya kuapishwa. Hivyo nichagueni mimi wengine michosho. Ngoja niende kupata msokoto na kanywaji kwanza. Long live Mlevi son of Boozer.
Chanzo: Nipashe Juni 6, 2015

No comments: