Imekuwa kama fasheni sasa.
Kila mtangaza nia ya kutaka kuteuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupeperusha
bendera yake katika uchaguzi ujao, anamponda rais Jakaya Kikwete wanayenyukana
kumrithi. Wanamuona kama mtu ambaye hana lake tena baada ya kutundika viatu
mwishoni mwa mwezi wa kumi. Kila anayekuja anakuja na gea ile ile ya kufanya vyema kuliko Kikwete ambaye wanamuonyesha
kama mtu wa hovyo, asiye na msimamo, mwoga na ambaye ameruhusu nchi ijiendee.
Hawamtendei haki rafiki yao hata kama kweli ana udhaifu wake unaojulikana. Pia wanampomshambulia
Kikwete bila kuushambulia mfumo uliomtengeneza, wanawandanganya wananchi. Kwani,
bila kubadili mfumo jambazi wa sasa, hata akichaguliwa malaika ataondoka ikulu
akiwa shetani. Huu ufisadi na ulegevu wanaomshambulia Kikwete kwao,licha ya
kuushiriki, watautenda wakiingia madarakani. Kama tungekuwa na mfumo
unaoshikisha adabu watawala baada ya kuondoka madarakani kwa kuwashitaki
wanapofanya madudu, Kikwete sasa asingekuwa analaumiwa. Tuliyaona alipoondoka
Benjamin Mkapa akiwa na tuhuma za kuiibia umma. Kesho atafuata Kikwete na kesho
kutwa atafuata mmoja wa hawa wanaomuandama.
Haiingii akilini watu wanaounda
serikali ile ile kuitupia madongo wakati walikuwamo –na bado wengine wamo –ndani
na walikuwa na uwezo wa kutoa ushauri au kurekebisha mambo kwa nafasi zao. Hata
hivyo, wanaomshutumu Kikwete wakati walikuwa naye kitanda kimoja wana bahati.
Angekuwa marehemu baba wa Taifa marehemu Mwl Julius Nyerere sina shaka. Angeishawafukuza
wengi kazi ukiachia mbali kuwapaka kuhakikisha hawapenyi kwenye chujio la CCM.
Washukuru Mungu CCM imeishiwa hata uongozi wenye kuweza kukaripia watovu wa
nidhamu kama hawa. Hata hivyo, haimaanishi kuwa watu wasikosoe. Kinachopaswa kuzingatiwa
ni kwanini wakosoe sasa wakati walikuwa humo humo wakitenda makosa
wanayojifanya kukosoa sasa? Hii ni aina fulani ya unafiki unaonuka.
Kwa vile
Kikwete amejigeuza punching bag –kwa
sababu anazojua mojawapo ikiwa kuwamo ukweli kwenye madai ya wahusika –wanaweza
kumtukana watakavyo na asifanye kitu kwa vile naye alipoingia aliingia kwa gea
hii ya maisha bora kwa wote akinaanisha wakati ule maisha hayakuwa bora chini
ya Mkapa. Ukimpiga mzazi wako nawe mwanao atakupiga tu. Inashangaza hata akina
Salva Rweyemamu anaowalipa vizuri wafanye kazi ya kumtetea hawafanyi hivyo. Je nao
wamemgeuka wakitafuta fursa ya kupata mwingine wa kuwatumia ili wamtumikie
baadaye kama walivyofanya kwa Kikwete? Je hawa nao wanalipwa kwa kazi gani
iwapo wanalala kwenye usukani?
Makala hii hailengi kumtetea Kikwete. Hiyo
ni kazi ya watajwa hapo juu hata kama hawaiwezi au kuigwaya kwa sababu ya maslahi
binfsi baadaye. Tunachotaka kuweka wazi ni kwamba wananchi wasihadaike na
kuwaona hawa wanaomkosoa au kufichua udhaifu wake ni tofauti naye. Ni wale
wale. Jogoo wote hunya ndani kiasi cha kuwafundisha vifaranga. Wanachofanya ni
utapeli wa kutaka waonekane wao ni safi wakati wamo kwenye dimbwi moja la
matope liitwalo CCM. Kwa lugha nyingine ni kwamba anayeiponda serikali ya
Kikwete akitokea mle licha ya kuwa moungo ni mnafiki ambaye anapaswa kuogopwa
kuliko hata ukoma. Kwani, anajiponda mwenyewe au kujivua nguo akiadhani
anamfanyia hivyo Kikwete. Kama ameweza kumgeuka huyo aliyemtengeneza atashindwa
kuwageuka wananchi? Wanachosema kingekuwa na maana kama wangekuwa nje ya
serikali husika tena baada ya kujitoa kupinga hicho wanachosema sasa. Waulize:
Mlikwina au mlikuwa wapi?
Ukisikia kauli kama hii iliyotolewa na
waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Uhusiano wa Kimataifa Bernard Membe
unashangaa. Membe alikaririwa akisema, Ninawatumia
salamu mapema, sitakuwa na kigugumizi kwa wanaotesa Watanzania. Nitahakikisha
Watanzania wanachukia rushwa na kutakuwa na sheria kali dhidi ya mtoa na
mpokeaji rushwa. Kama ni watumishi wa umma, watakwenda na maji....” Je asemayo
Membe ni ya kweli au funga kamba? Akiwa kama waziri alifanya nini kupigana na
rushwa. Kama Membe alishindwa kupambana na rushwa kwenye wizara yake ambapo
mabilioni ya shilingi yametumika kifisadi kwenye balozi zetu nje ataiweza nchi
nzima?
Mwingine aliyewaacha wengi hoi ni
Samuel Sitta aliyekaririwa akisema, “Ili
kukomesha tatizo la rushwa, hatuna budi kutunga sheria itakayotenganisha
biashara na uongozi.” Ni ajabu anayesema haya ni mwanasheria na aliyewahi kuwa
spika wa Bunge. Kwani Kikwete ndiye aliwazuia kutunga hiyo sheria au ni kamba
kama kawaida ili uonekane una sera na mipango vya kuwakomboa wananchi wakati
letu moja?
January Makamba naye hakubaki nyuma
kwenye kurusha madongo kwa serikali ya Kikwete aliyefanya kosa akamteua tokana
na ushawishi wa baba yake. Sasa anamlipa ambavyo hakutegemewa. Alikaririwa
akisema, “nitafanya mabadiliko ya
kisheria, kimfumo, kitaasisi na kijamii ikiwamo kuipa meno Takukuru kuwa na
mamlaka kisheria ya kuwashtaki watuhumiwa wa rushwa moja kwa moja mahakamani.”
Hivi bila rushwa itokanayo na kujuana na kulipana fadhili Makamba angekuwa hapo
alipo tokana na jina la baba yake?
Mwingine aliyewaacha wengi hoi ni
Stephen Wassira aliyekaririwa akisema, “Kumbukeni
sijatajwa katika kashfa kama za Escrow, EPA, Richmond na nyinginezo.” Je
aliyetajwa kwenye hizo kashfa zote zaidi ya rais Kikwete ni nani? Je kutotajwa
kwenye EPA Escrow na Richmond ndiyo kigezo cha kuwa msafi wakati kuna kashfa
nyingi zinapita bila kutangazwa wala kushughulikiwa?
Tumalizie kwa kuwashauri wananchi hasa
wapiga kura kuwa makini na waongo na wanafiki wanaofanya u-Petro wa kumkana
Bwana na u-Yuda wa kumsaliti Bwana. Kambale wote wana sharubu na nyani wote
mchezo wao ni mmoja. Hivyo, msiwaamini sana sana wakaange kwa mafuta yao
kambale hawa.
Chanzo: Dira Juni 29, 2015.
2 comments:
Salamu Mwalimu Mhango,
Kama tunavyojua siasa ni mchezo mchafu kama mabingwa wa uchunguzi wa siasa wanavyosema,na hili linadhihirika hapa kuhusu CCM kupigania kwa kila njia kubaki madarakani kama walivyotuahidi kwamba watatuwala kwa miaka 50 ijayo.Hii tulionalo sasa hivi katika mbio hizi za kupigania tiketi ya kuwania kinyangányiro cha urais ni kama show tu ya Tom and Jerry,ukweli ni kwamba kupakwa maptope kwa Kikwete,kushutumiwa,kumpiga vijembe na blah blah blah zote hizo ni kuwafunika watanzania akili na macho (divert attention) ili akili zao na macho yao yashughulishwe sana na hawa wagombea kinyanga'anganyiro cha urais ndani ya CCM kuliko watanzania hao kuwashugulikia viongozi wa kambi ya upinzani na kujipanga na kujizatiti kuiangusha CCM na kuitoa madrakani, na kwa hili CCM wamefanikiwa.Swali linalojiuuliza hapa kwa nguvu ni hili kwani kuchukua hizo fomu za kugombea urais ndani ya CCM imekua ni kama kuchukua kadi za mwaliko wa sherehe za harusi?iweje mpaka usawa huu kuna zaidi ya wagombea 30 ndani ya CCM wengine hata hatuwajui walikuwa wapi ndani ya CCM hiyo lakini wameibuka from nowhere na kila mmoja wao kwa hamasa ya hali ya juu kabisa anadai kwamba anastahiki kuuvaa urais,sasa kama si kutuona sisi wananchi ni matahira ni nini basi?
Mwalimu Muhango,walimtukana,walimbeza,walimkosoa Kikwete kwa wenye akili akili tunajua tu kwamba ,mara hii kabla ya uchakachuaji wa kura zetu wameanza na uchakachuaji wa akili na macho yetu kwa hiyo watanzania shughuli inayotushughulisha ni kuwasoma na kuwachambua wagombea hao zaidi ya 30 kana kwamba uchaguzi ni wa chama kimoja.Mwalimu Mhango,kadhia sio kumkana au kumsaliti Bwana wote hao ni timu moja na ndio wale wale wale.Kwa hiyo hakuna sababu ya wananchi kupoteza wakati wao kwa kuwashughulikia, kuwafuatilizia na kuwachambua majambazi,wanafiki,waongo na mafisadi wa level ya juu ya nani atakuwa Rais mtarajiwa kana kwamba hakuna hapo kambi ya upinzani.Ni show tu hiyo ya Tom and Jerry tuwe na hadhari vinginevyo tumeumia.
Anon nisingependa kuongeza kitu kwenye nasaha zao kwa watanzania kuwa hawa jamaa ni karata tatu. Unaodhani ni wachezaji kumbe ni mtapeli wale wale wanaotaka kukuviti kwenye mkenge wao. Kimsingi nami naona kama lao ni moja.
Hivyo, muhimu wananchi kuustukia huu mkakati wa kuwachakachua kiakili. Nimependa analogue yako.
Post a Comment