Baada ya kung’atuka na hatimaye kuaga
dunia kwa Mwl Julius Nyerere, walibaki viongozi wenye udhu wachache sana. Ni bahati
mbaya hata wale aliowaamini akawabeba hadi kubezwa amebeba nyago la mpapure walimgeuka wakageuka mafisadi wa kunuka.
Hata hivyo,
bado Tanzania ina watu wa kupigiwa mfano. Hawa si wengine bali wanafunzi wa
kweli wa mwalimu Nyerere. Mmoja wa watu hawa ni Joseph Butiku ambaye pia ana
uhusiano wa damu na Nyerere. Mzee huyu, licha ya kuwa muwazi na muadilifu, si
mwoga na anapokuwa au kukerwa na jambo huwa hasiti kulisema.
Hivi kariubuni
Butiku alikaririwa akisema, “Sasa
tunatoka kwenye utaratibu wetu wa vyama tunashiriki katika kufanya uovu. Kama
haki inauzwa, hatuwezi kupata amani. Viongozi wanatoa rushwa hata kabla ya
kupewa nchi. Je, wakipewa nchi itakuwaje?”
Tofauti na wakongwe kama vile Kingunge Ngombale Mwiru, Butiku na wengine
wachache kama vile Joseph Warioba ni wazee wachache unaoweza kuamini dhati na
yale wayasemayo.
Wazee hawa
wameshinda vishawishi na kuonyesha uzalendo wao wakati huu ambapo chama chao
kinatafuta mtu wa kupeperusha bendera yake. Wamejitenga na ukuwadi uchwara na
unepi ambao umewashinda wengi waliopwakia hongo hadi wazee wazima wakajivua
nguo hadharani. Kwa lugha nyepesi ni kwamba Butiku analionya taifa kuwa kama
halitajirekebisha likaendelea na ugunia wa kumeza kila kiingiacho litajikuta
pabaya huko tuendako.
Butiku bila
woga wala kumung’unya maneno alionyesha chanzo cha matatizo tunayoshuhudia
ambapo watia nia wanatembeza hongo mchana kweupe bila kuchelea lolote. Alisema, “Mtandao huo iliamua kufanya kazi nje ya CCM
kwa sababu itikadi zao na sisi zilitofautiana. Eti wanasema CCM ni chama cha
mizengwe kinawachelewesha kutajirika. Sasa hao watu ndiyo wameendelea kuwapo na
kusababisha haya matatizo yaendelee.” Butiku alikuwa akielezea uchafu
ulioasisiwa na wasaka tonge hapo mwaka 1995 kiasi cha kuendelea kuitafuna CCM.
Butiku hakuwa
peke yake kukemea uhovyo na uhalifu vinavyoanza kuonekana kama vitu halali na
vya kawaida ndani ya CCM na serikali zake. Mzee Warioba naye aliongeza kwa
akionyesha chanzo kingine kinachoweza kuleta uvunjifu wa amani nchini. Alisema, “Tunakwenda katika uchaguzi lakini huku
tukiwa na viashiria vya uvunjifu wa amani. Hivi nani hajui kuwa kuna rushwa
kubwa katika uchaguzi.” Kwa mujibu wa Warioba ni kwamba kinachoendelea kwenye
kutafuta atakayepeperusha bendera ya CCM ni rushwa tupu. Hii maana yake ni
kwamba watanzania kama hawatajifanya kuwa mataahira wanapaswa kutomchagua
mgombea wa chama kinachopata mgombea wake kwa rushwa na kuvunja kanuni
walizojiwekea. Kama wanaweza kuwa wazembe kiasi cha kuvunja hata kanuni
walizojiwekea, wakipata madaraka si watavunja sheria za nchi kama walivyofanya
kwenye kuua katiba ya wananchi? Je watanzania wanataka washikwe wapi au
watukanwe matusi gani au kuonyeshwa dalili gani wachukie na kuchukua hatua
mujarabu? Je itakapotokea nchi ikaingia kwenye machafuko watamlaumu nani kama
si kujilaumu wenyewe?
Watanzania wanapaswa
kuzingatia wosia na maneno ya wakongwe hawa wa CCM. Kwani wanachosema ni ukweli
ambao hauna shaka. Sasa kama wana CCM tena wakongwe wameishaona hatari na uhovo
wa CCM kunaja gani ya wapiga kura kuendelea kuipa hadhi ya kupeleka nchi
kuzimu? Nadhani ufisadi ambao CCM imeuasisi, kuusimamia na kuutekeleza
vinatosha kuwafanya watanzania wachukie na kutoa hukumu yako ya haki.
Najua baada
ya CCM kushikwa pabaya na wanachama wake wenyewe na kuishiwa, kwa sasa watakuja
na mzengwe wa kusema fulani tuliyempitisha ni mtu safi. Well, well, mnaweza
kuwa na mtu safi je chama ni safi? Huko nyuma
tuliwahi kuonya kuwa hata kama CCM wangemsimamisha malaika, mwisho wa siku
watamchafua naye awe kama wao. Watambadili lakini yeye hatawabadili kwa vile
chama kina mamlaka makubwa kuliko mtu kitakayemfadhili kugombea ili kulinda
maslahi yake hata kama ni maslahi haramu.
Wanaotilia
shaka ukweli huu wajiulize Mr. Clean aliishia wapi? Si aliaminiwa na Mwl Julius
Nyerere akambeba na kumpatia ushindi lakini akageuka kuwa Mr. Dirty? Je huyu ni
nani atakayedhaminiwa na chama kichafu asichafuke au atakayeweza kutumia usafi
binafsi kusafisha chama kisichoweza kusafishika. Sijui kama kipande cha sabuni
kinaweza kuisafisha bahari. Sana sana kitayeyushwa na kumezwa na kugeuka maji
ya bahari basi. Hivyo, wanaoitakia nchi mema wanapaswa kutohadaiwa na yeyote
atakayeteuliwa na chama ambacho hata waanzilishi na wakongwe wake
wameishakichoka na kukiona hakifai tena kuaminiwa madaraka.
Chama kilichoanzishwa
kupambana na uonevu na dhuruma kinapoyatenda haya kinakoma kuwa kile kile. Kwa sasa
CCM iliyopo ni chama kingine tofauti na CCM aliyoanzisha Mwl Nyerere ambaye
alipokufa na CCM yake ikafa ikabakia ya mafisadi, wala na watoa rushwa kama
wanavyobainisha Bujiku na Warioba. Je tusipowasikiliza na kuwaamini hawa
wakongwe tunataka tupate ukweli toka kwa akina Kingunge Ngombale Mwiru au
Paskari Ndejembi?
Tumalizie kwa
kuwapa heko Butiku na Warioba hata kama wanawapigia mbuzi gitaa. Maana, hatujui
kama CCM au watanzania watawasikiliza na kujiepusha zahama wanayotaka kuipa
ridhaa tena.
Chanzo; Dira Julai 16, 2015.
1 comment:
Hi jamani wamechoka hao hata sura zinatisha CCM hiyo
Wamechoka kwa akili hadi sura
Hawa wamechoka kinachowakeka CCM
Pension zao
Tumekwisha
Post a Comment