Kifo mwandishi chipukizi lakini mwenye athari kubwa katika tasnia ya uandishi wa habari marehemu Edson Kamukara kimetufundisha jambo moja kubwa. Kifo cha ghafla cha Kamukara licha ya kusababishwa na ajali ya kimaskini kimetuachia somo kuwa kumbe mbele ya serikali yetu wasanii ni bora kuliko waandishi wa habari!
Nani alitegemea kuwa mwandishi kama huyu aliyeanza kujijengea umaarufu kwa ithibati na taaluma angeagwa bila kupokea lau rambirambi toka Ikulu? Sina sababu ya kuilaumu ikulu hasa ikizingatiwa kuwa huwa ni utashi wake juu ya nani imepende au kumchukia. Nasema –kama mwana taaluma na mwandishi –kuwa kitendo cha ikulu kukaa kimya kwenye msiba huu kinaacha maswali mengi kuliko majibu. Tulizoea kusoma salamu za rambirambi toka ikulu na wakati mwingine kumuona rais Jakaya Kikwete akishiriki ima kuaga au mazishi ya watu mbali mbali wengi wakiwamo wasanii. Tulimuona kwenye misiba ya Kanumba, mzee Small na wengine. Sasa tunajiuliza: Mbona hatukumuona rais wetu kwenye msiba wa mwenzetu kunani? Je inaweza kuwa ukweli kuwa waandishi wa habari hufunga ndoa na wanasiasa wanapokuwa wakisaka ulaji na kuivunja wanapopata ulaji?
Kwa wanaojua thamani ya taaluma ya habari, wameshangaa na kusikitika hasa ikizingatiwa kuwa katika jamii yetu –hata hivyo –mambo ni tofauti. Msanii anapewa umuhimu zaidi ya mwandishi kwa vile watu wetu wengi hawana muda wa kufikiri. Unashangaa mwandishi –kwa mfano wa vitabu –kazi zake haziuzi wakati za wasanii zinauza. Je hii maana yake ni nini kama siyo kujenga taifa la kidaku na kijinga lisilopenda maarifa na badala yake likapenda mambo rahisi rahisi na mengine ya hovyo?
Jambo ambalo nimejifunza ni kwamba waandishi wamewekwa kwenye matabaka ya wanaokubalika na watawala na wasiokubalika. Maana haiingii akilini ikulu itoe salamu za rambirambi ulipotokea msiba wa mtangazaji wa zamani wa radio Tanzania Mshindo Mkeyenge hapo Mei 25, 2015 na kwenye msiba wa mama wa Mwaibale ukiachia mbali ule wa Florence Dyauli lakini ishindwe kufanya hivyo kwenye msiba wa Kamukara uliotokea mwenzi mmoja baadaye. Je ni kwa sababu Kamukara hakuwa anaandikia magazeti ya chama na serikali au ni kutokana msimamo wake wa kutopenda kutumiwa kama nepi? Je huu si ubaguzi wa kiitikadi? Je kama wote tungekuwa nepi kofia ingekuwa wapi?
Ukiachana na kukosekana kwa rais kwenye msiba wa Kamukara, unaweza kujikumbusha utitiri wa magazeti ya udaku tena yakiuza kama keki huku magazeti yasiyo na udaku yakiozea kwenye mbao. Tunaandika hili si kumtetea mwenzetu aliyetangulia mbele ya haki bali kutumia mwitikio wa baadhi ya taasisi za umma kuonyesha uoza wa kimfumo ambao unalikabili taifa letu.
Baada ya watawala kuua elimu na kuendekeza mambo ya hovyo kama vile kufanya siasa karibu katika kila kitu, kuna hatari ya vizazi vijavyo vikatawaliwa na wageni ndani ya nchi yao kutokana na kutokuwa na utamaduni wa kujisomea, kutunga vitabu na kudurusu mambo.
Zamani nakumbuka nilimtembelea rafiki yangu maeneo ya Masaki. Nilipoingia sebuleni kwake nililakiwa na kabati kubwa la vyombo vya kulia. Nilipata mstuko. Baada ya kuamkuana na kukaa kitambo nilimuuliza kama ana maktaba yake binafsi. Alisema kuwa ana vitabu vichache lakini viko kwenye maboksi. Nilishangaa zaidi. Ilibidi nimuulize kwanini asivinunulie shelf na kuviweka. Naye aliniuliza: Nikinunua shelf nitaiweka wapi? Nilimjibu kwanini umepata nafasi ya kupamba vyombo vya kulia ambavyo kimsingi vilipaswa vikae jikoni lakini unakosa nafasi ya kuweka vitabu ambavyo kimsingi ndivyo vimekuwezesha kupata kazi nzuri ya kuishi Masaki na kuweza hata kununua vyombo vya thamani vya kulia?
Rafiki yangu alipigwa na butwaa na akaniahidi angerekebisha kasoro ile. Je ni nyumba ngapi zimejaza upuuzi kama vyombo vya kulia kwenye sebule wakati vitabu vikiozea kwenye maboksi?
Tukirejea kwenye kifo cha Kamukara na jinsi ambavyo mwitikio wa baadhi ya wenzetu tena wanaowategemea waandishi wa habari umekuwa haba, mara nyingi inategemea mhusika alikuwa nani katika jamii. Kama angekuwa kanjanja huenda angeenziwa na wale wanaoweza kumtumia kama nepi. Tofauti na hapo anachoweza kuambulia ni kile kilichowahi kuwakumba akina Absalom Kibanda walipokataa kuwa kitanda kimoja na mafisadi au Stan Katabaro aliyeuawa kwa kushupalia kashfa ya Loliondo zama za ruksa.
Ila ni aibu kwa watu wanaojulikana kuwa sauti ya wasio na sauti, the voice of the voiceless kuchukiwa kiasi hiki. Hatuna sababu ya kuwalazimisha wahusika watupende, lakini tuna haki ya kuwaambia kuwa wanajenga jamii ya kijinga na kitwahuti inayochukia maarifa na kupenda upuuzi. Ukienda nchi jirani kama Kenya Rwanda na Uganda hata Burundi pamoja na mitafaruko yake, hawana magazeti ya udaku kama Tanzania. Je kuwa na wingi wa magazeti ya udaku ni sifa nzuri au ni kielelezo kuwa sisi ni wadaku tofauti na wenzetu ambao siyo?
Tunaomba tumalizie kwa kuitaka jamii ibadilike ianze kuthamini michango ya watu na ijenge utamaduni wa kuthamini maarifa kuliko upuuzi kama vile burdani. Japo binadamu hawezi kuishi kwa kusoma tu, anahitaji burdani lakini ahitaji kwa kiasi kikubwa kuliko taarifa na maarifa. Ni aibu tunaposhabikia upuuzi na kupuuza mambo ya maana.
Chanzo: Dira Julai 12, 2015.
2 comments:
Nilianza kuifahamu Kenya kwa undani nilipoanza kwenda kufanya utafiti mwaka 1989. Niliona tofauti baina ya Kenya na Tanzania katika masuala haya ya vitabu. Kwa mfano, wakati vitabu vya Mwalimu Nyerere vilikuwa nadra kuviona Tanzania, vilikuwa tele Kenya. Niliviona katika maduka ya vitabu sehemu kama Nairobi na Mombasa. Huo ni mfano moja.
Mfano wa pili ni magazetini. Ilikuwa ni kawaida kuona uchambuzi na taarifa za vitabu katika magazeti ya Kenya. Na bado hali ni hiyo. Magazeti ya Tanzania hayana utamaduni huo.
Mfano wa tatu ni kuhusu waandishi. Magazeti na vyombo vingine vya habari Kenya huandika kuhusu waandishi. Kwa mfano alipofariki Grace Ogot, kulikuwa na taarifa mbali mbali magazetini juu yake na kazi zake. Anapofika Ngugi wa Thiong'o nchini mwake Kenya, kama alivyofika hivi karibuni, magazeti yao na vyombo vya habari huchangamkia jambo hili kwa namna mbali mbali. Kwa Tanzania hakuna utamaduni huo.
Mfano, miaka mitatu minne iliyopita, mwandishi maarufu Moyez Vassanji ambaye alikulia Dar es Salaam na anaishi Canada alitembelea Tanzania, akafika hadi Mbeya. Ni chombo kipi cha habari Tanzania kilirepoti kuwepo kwake? Ngugi wa Thiong'o alipokuwa nchini mwake Kenya hivi karibuni, alipokewa hata na Rais. Sisi Tanzania mwandishi wetu maarufu hawezi kutegemea hayo.
Kaka Mbele nakubaliana nawe kwa pointi zako tatu. Nimekaa Kenya kwa miaka mitatu na kuizunguka ile nchi. Ni kweli utamaduni wa wakenya kuhusiana na vitabu na elimu ni tofauti sana na watanzania. Wakenya hawapendi udaku wakilinganishwa na watanzania. Siku moja nikiwa Nairobi nilishuhudia mshike mshike wakati kampuni moja ilipoweka tangazo lenye kuvunja maadili mtaani. Wananchi walilivamia lile bango na kuliangusha na kutawanyika huku vyombo vya habari vikilipoti tukio hilo. Nikijikumbusha mabango ya uchafu na matangazo ya redio na runinga ya kuchefua yanayorushwa Tanzania huwa napata hasira ajuaye Mungu. Hata investments za Kenya ni tofauti na Tanzania. Wakati wakenya wakiwekeza kwenye mashule na vyuo, watanzania wanasifika kwa kuwekeza kwenye mabaa, nyumba za wageni, mahoteli na upuuzi mwingine. Hata usanii wa hovyo hovyo kama maigizo yanayokopi toka Nigeria Kenya hawana.
Kwa ufupi ni kwamba itachukua miaka mingi kubadili mfumo wa hovyo wa Tanzania wa kushabikia mambo ya hovyo na kugeuza mambo ya maana kuwa ya hovyo. Tumekuwa taifa la kisanii linalotawaliwa na wasanii. Nadhani ndiyo maana wasanii hawa wanathaminiana kuliko kuthamini watu wengine muhimu. Juzi nilipotoa Kitabu changu kipya cha Soul on Sale, African Executive Magazine (Think tank) walitoa sehemu na kuichapisha huku wakiniandikia kunipongeza. Kwa Tanzania hata nilipomtumia mhariri mmoja wa gazeti la kiingereza ninalochambulia kila wiki a-serialize hakunipa hata jibu.
Post a Comment