Matusi
yaliyoporomoshwa na rais mstaafu mwenye kashfa ya kujitwalia Mgodi wa Makaa ya
Mawe wa Kiwira Benjamin Mkapa hivi karibuni kwenye kufungua kampeni za Chama
Cha Mapinduzi (CCM) yameacha wengi vinywa wazi. Mkapa alikaririwa akiwaita wapinzana malofa na
wapumbavu asijue alikuwa akijichamba asijue? Hatutachambua maneno malofa na
wapumbavu kutokana na urahisi wake kueleweka. Je tukiangalia hawa wapinzani na
Mkapa aliyekwisha achia dola tena kwa aibu ya wizi wa kijinga nani lofa na
mpumbavu? Ngoja tuache wasomaji waamue wenyewe. Kwani hatutaki kumlaumu Mkapa
kwa kurudia alichofanya.
Pili,
kwa rekodi ya Mkapa kisiasa, wengi hawakutarajia kama angepata mshipa achia
mbali jeuri ya kutukana wenzake hadharani tena bila sababu. Wapo wanaoona kama
Mkapa alipaswa abwate ili kuwaridhisha watakaoingia madarakani wamkingie kifua
kama alivyofanya rais anayeondoka Jakaya Kikwete baada ya kubainika yeye
marafiki na familia yake walivyotumia uwekezaji kulihujumu taifa. Ni aibu kiasi
gani kwa mtu anayetegemewa awe mfano wa kuiga anaongea kama wahuni na wapiga
debe wa vijiweni.
Tatu,
kwa hadhi ya Mkapa kama rais wa zamani–hata kama ana madudu na mazabe yake
aliyotenda kutokana na upogo na tamaa–hakupaswa kuwa bingwa wa matusi na
mipasho jambo ambalo linaweza kufanya wenzake wamuite mtu mzima hovyo.
Nne, kwa umri wake alipaswa awe ameishajua
jinsi ya kuchagua maneno ya kuongea na ya kutoongea. Si jambo la maana kwa mzee
tena wa hadhi ya Mkapa kuongea kama watoto wa vijiweni au wale wazee waliokataa
kukua. Sijui kwa matusi ya Mkapa ametufundisha nini kama jamii aliyowahi
kuitawala baada ya kushindwa kuiongoza?
Tano,
Mkapa alipaswa kuchukuliwa hatua za kisheria kwa kutenda makosa ya jinai
mojawapo likiwa ni matusi na kutumia lugha za shari. Sijui Mkapa amekumbwa na
nini? Maana huko nyuma hakuwa hivi! Hata mwl Julius Nyerere aliyempigia kampeni
baada ya kugundua kuwa alikuwa hauziki bila kubebwa, hakutumia lugha za hovyo
na aibu kama hizi anazotumia Mkapa.
Sita,
Mkapa anapaswa aambiwe kuwa lugha aliyotumiwa licha ya kutokuwa saizi yake si
ya kistaarabu wala haina cha maana cha kulifundisha taifa zaidi ya kumvua nguo
na kumuonyesha kama mtu muhuni na mpayukaji asiyejua jinsi ya kuzuia ulimi
wake. Kama hakuwa na la kusema si angejinyamazia kuliko kumwaga upupu.
Saba,
kama Mkapa atataka asiendelee kueleweka vibaya, basi awaombe msamaha wapinzani
aliowatukana na watanzania aliowanyosha utovu wa nidhamu tena hadharani. Hivi kama
ni ulofa na upumbavu, kuna ulofa na upumbavu kama kuingia kwenye mikataba ya
kijambazi ya uwekezaji ambayo haina maslahi kwa taifa? Je kuna ulofa wa kisiasa
kama kutumia matusi na maguvu kama ambavyo inaanza kubainika bila sababu ambapo
wahusika wameishaanza hata kutumia polisi kuwahujumu wapinzani? Ama kweli mzoea
vya kunyonga vya kuchinja haviwezi. Sijui kama wapinzani ni malofa na wapumbavu
kama anavyowaelezea Mkapa wakati wameizidi CCM yake kete wakawasomba mawaziri
wao wakuu wawili kwa mpigo akiwamo mshirika , rafiki na waziri mkuu wa pekee wa
Mkapa Fredrick Sumaye ambaye ameamua kujitenga na dhuluma na kushindwa kusoma
alama za nyakati. Hivi ikitokea
wapinzani wakashinda Mkapa ataweka wapi sura yake? Tulitegemea wazee aina ya
Mkapa wahubiri haki ,upendo, amani, heshima, maadili, haki, kumbe wapi. Badala yake
wanahubiri maangamizi, matusi, uchokozi na vurugu. Tunamshauri Dk John Pombe
Magufuli ajitenge na watu wa namna hii asionekane yu sawa na wao au ni
kikaragosi chao. Hatudhani kama Magufuli ni mchovu hivi kiasi cha kuhitaji
kubebwa na wale waliobebwa.
Namheshimu
sana mzee Mkapa ila kwa hili alilofanya, kwa mapenzi yangu makubwa kwake,
sitamuogopa wala kumdanganya, amechemsha tena vibaya sana. Hata huyu
aliyempigia kampeni kwa lugha za mipasho, kashfa, matusi na ukosefu wa busara
hamsaidii zaidi ya kumuumiza. Badala ya kujifunza kwa Nyerere aliyewahi hata
kuambiwa amebeba kinyago cha mpapure bila kurusha ngumi wala matusi, Mkapa
anazidi kujivua nguo tena hadharani. Hakika hii siyo saizi yake. Hata mzee Jangala kwenye maigizo yake hawezi
kufikia uhovyo kama alioonyesha Mkapa.
Tuamalize
kwa kumtaka Mkapa aombe msamaha yaishe. Maana waingereza wana msemo kuwa
ukiishi kwenye nyumba ya vioo usiwachokoze vichaa. Bado watu wanajua madudu
yake ya NBC, Kiwila, EOTL na mengine mengi. Ashukuru Mungu tuna siasa za
kulindana tokana na wote kuwa waovu. Vinginevyo angepata wapi hiyo jeuri mtu
kama yeye. Wapinzani wanaweza kuamua
kama mbaya mbaya wakamjibu kizembe kama alivyofanya akaumbuka zaidi. Tunawashauri
wasimjibu Mkapa kwa vile lugha aliyotumia siyo saizi yao. Sana sana walipaswa
kwenda mahakamani kuweka katazo Mkapa asishiriki kampeni kwa vile hana udhu
wala uwezo wa kufanya hivyo bila kuvunja sheria.
Chanzo: Dira Agosti 31, 2015.