Kwa wanaokumbuka maneno makali ya waziri mkuu wa zamani Fredrick Sumaye aliyejiungua toka Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kujiunga na Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kuelekea kilele cha kumpata mgombea wa urais wa CCM, watakubaliana nami kuwa mchango wake kwenye upinzani unaweza kuwa mdogo kuliko inavyodhaniwa.
Katika kuelekea kupitisha wagombea watano (tano bora) Sumaye alitishia CCM kuwa kama wangemchagua fisadi (Edward Lowassa) angehama chama. Baada ya CCM kutomteua Lowassa kupeperusha bendera yake, wengi walidhani Sumaye angeendelea kukaa CCM lakini wapi.
Kwa kauli hii ambayo aliipinga mwenyewe kwa kumfuata yule aliyetahadharisha chama chake kisimpitishe tokana na rekodi yake (mbaya) inamfanya Sumaye aonekane kigeugeu na muongo (kama baadhi ya makada wa CCM walivyosema kwenye ufunguzi wa kampeni za CCM). Kwa kumbukumbu, mgombea aliyeshindwa kupenya Charles Makongoro Nyerere akisikika akimnanga Sumaye kwa kuwa mnafiki na muongo aliposema kuwa anashangaa alitahadharisha chama kisimkumbatie fisadi lakini yeye akaishia kumkumbatia fisadi huyo huyo!
Kwa wataalamu wa mikakati, maneno ya Sumaye yanamfanya awe soft target kwa wapinzani wake na upande wake. Hivyo, uwezekano wa Sumaye kuleta matunda na faida vilivyotegemewa ni mdogo sana kiasi cha kumfanya awe mzigo (liability) badala ya faida (asset). Ifahamike kuwa lengo la makala hii siyo kumshambulia Sumaye wala kupigia debe CCM. Tunajaribu kudurusu udhaifu na ubora wa Sumaye ili kuona kama atausaidia upinzani.
Kwanza, Sumaye ni mmojawapo wa waliowezesha mfumo wa rushwa anaopambana nao kwa sasa tena akiwa kiongozi wa juu kwa miaka kumi. Rejea ukweli kuwa Sumaye alikuwa waziri mkuu aliyehudumu kwenye ngazi hiyo kwa muda mrefu kuliko wengine wote.
Pili, chini ya uwaziri mkuu wa Sumaye–japo yeye hajahusishwa na uchafu wowote–ulifanyika uwekezaji wa hovyo na wa kifisadi ulioingiza taifa kwenye matatizo makubwa kiuchumi. Rejea kugawiwa kwa iliyokuwa Benki ya Biashara (NBC) kwa makaburu hadi marehemu baba wa taifa kupinga ufisadi huu wa mchana. Rejea kuuzwa kwa nyumba za umma kwa mafisadi. Rejea kuasisiwa na kutekelezwa kwa kashfa ya EPA iliyogharimu taifa mabilioni ya shilingi bila kusahau kashfa nyingine kama vile Meremeta, Mwananchi Gold, SUKITA na nyingine nyingi.
Tatu, Sumaye anajitahidi kuukosoa mfumo uliomfinyanga na kumlea hadi akafikia hapo alipo sawa na swahiba yake mpya Lowassa. Japo haiwezekani kupata kiongozi yoyote nje ya CCM kutokana na kuwa Tanzania ilikuwa chini ya mfumo wa chama kimoja ambapo kila mtanzania alilazimika kuwa mwanachama tawala, Sumaye alipaswa kuwa wa mwisho kutupa madogo kwa wenzake. Naona kama CCM ni wenzake Sumaye zaidi ya upinzani ambao amejiung anao kutaka kulipiza kisasi kwa kunyimwa kuingia hata kwenye tano bora jambo ambalo licha ya kumshusha, limemuudhi na kumfedhehesha ukiachia mbali kumchanganya.
Nne, kwa kujiunga na upinzani ili kulipiza kisasi, Sumaye anaonekana kama mtu anayetafuta maslahi binafsi na si ya taifa.
Tano, CCM watatumia maneno ya Sumaye kuukaanga upinzani. Tuseme watawakaanga samaki wawili mapapa yaani Sumaye na Lowassa kwa mafuta yao yaani maneno na matendo yao.
Hakuna ubishi kuwa Sumaye ni mmoja wa viongozi safi na wachapakazi. Rejea kutohusishwa kwenye ufisadi wowote hata alipokuwa chini ya serikali fisadi kwa miaka kumi. Hii ni tofauti na bosi wake Benjamin Mkapa aliyeingizwa madarakani na marehemu baba wa taifa Mwl Nyerere akiwa Mr. Clean akaondoka akiwa Mr. Filth baada ya yeye, familia yake na marafiki zake kujitwalia mgodi wa Makaa ya Mawe wa Kiwira kinyume cha sharia.
Pili, Sumaye ana uwezo mkubwa wa kujenga na kubomoa hoja kiasi cha kuwa kivutio kwa wasikilizaji kama ilivyotokea hivi karibuni kule Mbeya. Pamoja na hayo, wenye akili wakichambua maneno yake ya sasa na yale aliyotoa kuelekea kumalizika mchakato ndani ya CCM wanashindwa kumuelewa. Na kama wanamuelewa, wanamuona kama mtu asiyeweza kuaminika tena.
Ukiachia hili, Sumaye amesema wazi kuwa anapambana na mfumo mbovu jambo ambalo ni kweli na la dhati ingawa hata uko aliko anauunga mkono mfumo mzuri wenye kupendekeza mtu mbovu. Hapa ngoma ni droo. CCM ina mfumo mbaya wenye mgombea safi tofauti na UKAWA yenye mfumo bora lakini yenye mgombea mbovu.
Tumalizie kwa kuuliza: Je ujio wa Sumaye kwenye upinzani utaleta faida au kuishia kuwa soft target kwa CCM kuubomolea upinzani? Je wapiga kura watasikiliza yapi kati ya yale aliyosema Sumaye kabla ya kujiunga na upinzani na haya anayosema kwa sasa?
Chanzo: Dira Sept., 3, 2015.
No comments:
Post a Comment