Baada ya baadhi ya wagombea urahis kuwa wanatoa ahadi kama njugu, kijiwe kimestuka kiasi cha kukaa kama kamati ya ukombozi kujadili janja hii.
Leo Mheshimiwa Mijjinga ndiye analianzisha, “Waheshimiwa wanakijiwe hivi mnaonaje hili changa la macho ambapo wagombeaji urahis hata uishiwa wanamwaga ahadi kama njugu?”
Kapende anakula mic, “Usikumbushe hii aina mpya ya utapeli kama nilioshuhudia hivi karibuni nilipokuwa Lindi kabla ya kurejea Bongo na kukumbana na kadhia hii. Kweli watu wanamwaga ahadi utadhani wamesahau ya 2005.”
“Mgosi unashangaa hii ya kutoa ahadi wakati Njaa Kaya anaendeea kumwaga vyeo kwa washikaji zake kama hana akii nzui! Hakuna aiponiacha hoi kama kumteua Amos Makaa kuwa mkuu wa nkoa ukiachia kuteua mabaozi wakati huu wa lala saama ambapo aipaswa kuwa anafunga viago na kuishia,” anajibu Mgosi Machungi huku akibusu kipisi chake cha sigaa kai.
Msomi Mkatatamaa anaamua kuingia mapema leo, “Nadhani tunapaswa kulaumu mfumo wa kipuuzi unaotoa madaraka makubwa kwa ngurumbili usijue atayafuja. Hii kutoa ahadi si chochote si lolote bali utapeli wa kisiasa ambao unafanywa na wagombea wote tishio. Kimsingi, tusiposhupaa ikarejeshwa katiba mpya, upuuzi kama huu utaendelea kurudiwa kila baada ya miaka mitano au kumi. Yako wapi Maisha Bora kwa Wote Apechealolo (MBWA)? When you have an imperial president you must expect such things become norms.”
Kabla ya kuendelea mzee Maneno anamuonya Msomi akisema, “Msomi angalia lugha. Maana maneno mengine yanatua nje akina sie.”
Mpemba anakula mic, “Wallahi hata mie nshangaa mtu kutoa ahadi kwa mfano ya kuwapa vyeo tena vikubwa waloshindwa utadhani vyeo hivyo mali ya mama yake. Wengine wadai watatoe ilmu bure bila kueleza wanivyopanga kutafuta fedha ukiachia wengine kuahidi vitu visivoingia akilini wallahi.”
Sofia Lion aka Kanungaembe anakwanyua mic, “Kama wanaoahidiwa wanaridhishwa na ahadi husika hakuna haja ya kulaumu watoa ahadi. Kwani wanalazimishwa kuzikubali zaidi ya kushawishiwa wapige kura?”
Kanji anakamua mic, “Mimi ona kila gombea tongoza piga kura. Kama tafanya kosa natoa basi taumia sana.”
Mbwamwitu anamchomekea Kanji, “Kanji acha uhuni. Eti wanatongozwa watoe na wakitoa wataumia! Sasa hapa tumlaumu nani zaidi ya kuwa ubwege wa wahusika? Nawashauri wasikubali kutongozwa wala kutoa kura ili wengine wale.”
Mipawa anakatua mic, “Hapa mrume umenena. Kama watajirahisisha wakatoa kura watamlaumu nani wakati walishaliwa sana tena si mara moja wala mbili? Inaonekana wengi wamesahau ahadi kibao kama kupambana na ufisadi, kufumua mikataba ya uchukuaji unaoitwa uwekezaji, kupambana na wauza bwimbwi vitu ambavyo vinazidi kuhalalishwa huku wakuu wakichukua cha juu. Kimsingi, nakubaliana na Msomi na Mbwamwitu. Kama watajiachia wataliwa tu.”
Mgosi anaamua kurejea, “Hei waiwe wao wasisababishe kaya yetu kuiwa na kubakwa kama ambavyo imekuwa ikifanyiwa kwa muda muefu. Yaani imefikia hata wanyama wetu wanatooshwa na hakuna anayejai ukiachia mbai kuendeea kufanya usanii eti watapambana na ushwa na ufisadi.”
“Hivi jamani mmegundua kuwa baadhi ya wagombea hawapendi kuongelea ufisadi kabisa? Wengine wanauongelea kama suala la mtu binafsi wasijue ni suala la kaya nzima. Nashauri muwashauri walio karibu yenu wastukie huu usanii wa kuahidiwa pepo wakaishia kusweka motoni kama ilivyotokea tangu kuahidiwa maisha bora kwa wote yakaishia kuwa mateso makali kwa wote. Ziko wapi ajira, kukuza uchumi na kupambana na ufisadi? Sana sana kilichokuzwa ni deni la kaya na kuzidi kuumka kwa vitendo vya kifisadi na rushwa. Watu wanafikia mahali hata kughushi shahada na bado wanapewa nafasi za juu zinazohitaji maarifa, busara na elimu ya kutosha! Wanatupeleka wapi hawa? Watu wameua hata Katiba kiasi cha kutuacha tukiendeshwa kama kundi la mbuzi tena linalochungwa na fisi na mbwamwitu.” Msomi anashuka kama hana akili nzuri.
Mbwamwitu anachomekea, “Msomi angalia.”
Msomi anaendelea, “Simaani mheshimiwa wewe. Hii ndiyo bahati mbaya ya kupeana majina ya wanyama. Nimaanishacho ni kwamba, hali itakuwa mbaya sana baada ya uchakachuaji huu. Yeyote atakayechaguliwa atavuruga kutokana na mfumo kutompa mamlaka na nyenzo za kuondoa kadhia za wachovu. Uongozi ni taasisi na si mtu binafsi hata angekuwa genius kiasi gani. Waulize wanaosifiwa ziko wapi nyumba za wachovu?”
Kapende anachomekea, “Aulizwe Denjaman Dugong Makapi na baraza lake la mawaziri. Hamkumsikia akituita wote wapumbavu baada ya kutuita wavivu wa kufikiri. Wakati mwingine alikuwa sawa kwa vile jinsi alivyotuibia na hawara yake Ana Tamaa asingekuwa uraiani zaidi ya kuwa lupango. Nashangaa hata waliomruhusu kusimama kwenye majukwaa na kutoa pumba na upupu wake sijui anawasaidiaje! Sioni tofauti yake na Jose Gwajumaa.”
Mheshimiwa Bwege aliyekuwa akisoma gazeti anakula mic, “Mie nadhani tunapaswa kutahadharisha kuwa huu msimu ni wa kuliwa, kulana na kula. Wachovu wasipokuwa makini, wataliwa hadi wanaingia makaburini. Nadhani hapa lazima tulaumu ubwege na usahaulifu wa watakaotoa kura ya kula na kujirahisisha kiasi cha kuliwa kila msimu wasistuke wala kuchukia. Sijui washikwe wapi wastuke?”
Kijiwe kikiwa kinanoga si ikapita misafara ya watoa ahadi hewa. Acha tuwazomee!
Chanzo: Tanzania Daima Sept., 23, 2015.
No comments:
Post a Comment