Kwanza niombe msamaha kwa kutowataarifu wasomaji kuwa nilikuwa na mpango wa kuendeleza makala ya wiki jana juu ya tuhuma za ulaji rushwa wa wazito wa mkoa wa Dar Es Salaam. Vyombo vya habari viliripoti kuwa Kamishina wa kipolisi, Simon Sirro, wa Jiji la Dar Es Salaam na RPC wa Kinondoni, Susan Kaganda wanachunguzwa tokana na tuhuma zilizotolewa dhidi yao na Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam Paul Makonda. Hili ni jambo ambalo ni jema–japo kuchunguzwa watuhumiwa bila kumchunguza Makonda itakuwa si kuwatendea haki makamanda hawa–ukiachia mbaliku kujenga mazingira kuwa kuna watu wasiogusika (untouchables) nchini. Tunasema; Makonda naye achunguzwe. Kwani, alionyesha uzembe na, unaweza kusema, ubabaishaji na kukwepa wajibu wake kama kiongozi wa ngazi ya juu na raia kwa kutoripoti makosa ya jinai yaliyokuwa yakitaka kutendeka kwa kumhushisha. Makonda, kama mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa, kwanini–kama hakuwa na maslahi kwenye kadhia hii–hakuchukua hatua kama vile kuripoti kwa waziri mkuu hata rais na badala yake akaishia kulalamika kama hapakuwa na namna au mvutano? Hili swali linajirudia kuliko mengine ili kumpa picha msomaji afanye tathmini hata hitimisho lake.
Pili, Makonda anapaswa abanwe awataje wahusika ili washughulikiwe na kueleza kwanini hakuwataja awali. Na hapa lazima tuwe wazi. Tusizugwe na watuhumiwa walioripotiwa na vyombo vya habari kukamatwa siku moja tu baada ya vyombo vya habari kuja juu. Kwanini wakamatwe siku moja baada ya tuhuma hizi kufichuliwa kama hakuna namna? Je mamlaka zilikuwa wapi siku zote hizi? Je hapa nani anatuchezea mahepe kati ya Makonda, Sirro na Kaganda? Hii maana yake ni kwamba watatu hawa, kwa sababu wajuazo wenyewe, walikuwa wanawaachia wauza shisha. Je, kama hakuna namna, ilikuwaje wawajibike sasa na si kabla? Maana, vyombo vya habari vimeripoti hivi karibuni kuwa watu watatu wamekamatwa kwa makosa yahusianayo na uuzaji shisha.
Ukiachia maswali hayo mama, kuna mengine:
Mosi, je tutaendelea kufanya kazi kwa namna ya kuzamia na kuchomeana hadi lini?
Pili, je hawa watatu tu waliokamatwa wanatosha; au wahusika wanatafuta kutuliza hasira na shuku za wananchi ili waendelee na business as usual kama ilivyokuwa kabla ya kuchomeana utambi?
Tatu, baada ya Makonda kumshutumu Sirro na mwenzake, je wao wanajitetea vipi lau wananchi wapime na kujua mbivu na mbichi ni ipi?
Nne, je wawili hawa watakwenda mbele ya vyombo vya sheria ili kupata stahiki yao au watanyamaza na kuacha yapite ilhali kunyamaza kunaweza kutafsiriwa kama ukweli wa madai?
Tano, je watatumia njia mbadala za ndani ya serikali na kuutangazia umma kilichofikiwa?
Sita, kwa upande wa mamlaka zilizowateua, zitafanya kama ilivyokuwa kwa marehemu Wilson Kabwe? Yaani kuwawajibisha wahusika bila kusikiliza upande wa pili jambo ambalo litamfanya Makonda aonekane bora kuliko wenzake (better than thou) jambo ambalo si jema kwenye utumishi wa umma ambapo kila mtu ni sawa. Kama wawili hawa watatoa utetezi au maelezo yao, itakuwa vigumu kwa umma na hata wakubwa wao kubaini nani mkweli na nani muongo, nani mtafuta sifa na nani mchapakazi.
Saba, je kuna mengine mengi yaliyofichwa nyuma ya utata huu unaoonekana kukiuka kanuni za utawala hata uongozi kwa kufanya mambo hovyo hovyo bila kufuata taratibu zilizowekwa na zinazojulikana? Hivi karibuni, mwandishi mmoja alishuku mbinu ya Makonda ya kumchafua Sirro kama njama ya kumzuia asiteuliwa IGP. Lisemwalo lipo; kama halipo laja. Hili nalo lapaswa kuchunguzwa.
Nane, je kitendo cha Makonda kumuumbua Sirro na Kaganda hadharani si ushahidi kuwa baadhi ya watendaji wa serikali ya awamu ya tano, ima hawajui mipaka ya madaraka yao au hawajui hata wanachofanya kiasi cha kulimana hadharani tokana na wengine kupewa madaraka makubwa kuliko uwezo wao?
Tisa, je huu si ushahidi kuwa serikali ya awamu ya tano haikushikamana (incohesive) sifa ambayo si nzuri kwa serikali ilijionyesha kuwa makini? Sijui kama akina Makonda wanalijua na kuliona hili hasa wakati huu ambapo wafanyakazi wanalalamikia kunyanyaswa na wateule wa rais.
Kumi, tokana na tabia ya Makonda kuwa kujifanyia mambo atakavyo hata kwa kukiuka kanuni, wapo wanaodhani amepewa madaraka makubwa kuliko uwezo wake. Mfano, hivi karibuni, alionekana akiwadhalilisha baadhi ya watendaji kwa kudai wanaamini ushirikina badala ya kufanya kazi bila ushahidi. Kama haitoshi, alimkalisha kiti moto DMO wa Kigamboni mbele ya umma kana kwamba hakuna mechanisms za kushughulikia tatizo kama hili.
Tuhitimishe kwa kuvitaka vyombo vya dola visimuongope yeyote tokana na cheo au ushawishi wake. Chunguzeni wote; ili ukweli na mengine ambayo yanaweza kuwa yamefichwa vijulikane. Kwani wahusika, licha ya kuwa viongozi wa ngazi ya juu, bado ni wanadamu wenye kila aina ya udhaifu ukiwemo uwezekano wa kushawishika kupokea rushwa hata kukomoana.
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano leo.