Wengi wa wapenda demokrasia, haki na usawa nchini watakuwa wameshangazwa na
hata kuchukizwa na yaliyojiri hivi karibuni. Ni kuhusiana na sakata la
kughushi; mbali na la uvamizi wa vituo ya Clouds. Hii ni baada ya
kuachishwa kazi kwa aliyekuwa waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo,
Nape Nnauye. Hata hivyo, kosa lake halikuwekwa wazi ukiachia mbali kujengeka
hisia kuwa kadhia hii ilitokana na Nape kuunda tume ya kuchunguza uvamizi wa
vituo tajwa hapo juu. Japo rais hapaswi kuingiliwa kwenye mamlaka yake ya
uteuzi au utenguzi, kuna haja umma kujulishwa hasa, ikizingatiwa mhusika
alikuwa ameshikilia madaraka ya umma. Je kweli kosa la Nape ni kuunda tume
kuwachunguza wateule wasioguswa?
Japo ni haki na mamlaka ya
rais kuteua na kutengua, kuna haja, wadau yaani wananchi, kujulishwa
kinachoendelea jikoni; kuepuka kujengeka dhana ya udikteta, upendeleo na
upatilizaji kwa wenye mawazo tofauti. Umma unapaswa kujulishwa nani wanapaswa
kuguswa na nani hawapaswi kuguswa hata watende makosa makubwa kiasi gani.
Tanzania ni nchi ya kidemokrasia inayopaswa kuendeshwa kwa haki, kanuni, sheria
na usawa bila kusahau katiba inayotamka wazi kuwa watanzania wote ni sawa na
wana haki sawa.
Mengine yaliyoibuka kwenye
kadhia tajwa ni matumizi mabaya ya vyombo vya dola. Inakuwaje mtu mmoja, tena
asiye na stahiki kisheria kutumia vyombo hivi kwa maslahi binafsi na katika
mambo binafsi kama ilivyokariri taarifa ya uvamizi wa Clouds? Mbali na hili,
inakuwaje, kama taifa, tunaanza kuminya na kutishia vyombo vya habari ambavyo
viko kikatiba na si kwa mapenzi ya mtu hata awe na mamlaka kiasi gani?
Inakuwaje; wahusika wanashindwa kujua vyombo vya habari ni sauti ya wasio na
sauti au voice of voiceless dhana nyepesi kabisa kujua? Rejea namna rais
alivyokaripia na kutishia vyombo vya habari kuwa kama vinadhani vina uhuru, it
is not to that extent au si kwa kiwango hicho. Haya si maneno ya rais
anayefuata na kulinda katiba wala kuheshimu uhuru wa kiraia.
Katika kutishia na kuonya
vyombo vya habari, rais alisikika akijigamba kuwa yeye ni rais anayejiamini na
ambaye utawala wake hautokani na ushauri, usaidizi wala ushirika wa mtu yeyote.
Kwani alipokwenda kuchukua fomu za kugombea urais, licha ya kutoshauriwa na
yeyote, alikwenda peke yake. Hii ni kweli; japo sijui kama alijipigia kura na
kushinda. Isitoshe, rais wa nchi anapaswa kuwa rais wa wananchi wote bila
kujali tofauti zao. Hili, hakika, ndilo ambalo rais amekuwa akilihubiri; japo
anaonekana kutolitenda. Kwa maneno ya rais, ni kwamba utawala wake ni
wake binafsi. Je inawezekana taasisi kubwa na muhimu katika taifa ikadhibitiwa
na mtu mmoja hata awe mjuaji kiasi gani? Urais kama, taasisi ni mkusanyiko wa
vyombo vingi. Hivyo, unahitaji maelfu ya wananchi ili uweze kufanikisha malengo
uliyokabidhiwa na wananchi. Hata wafalme huwa hawatawali peke yao pamoja na
ufalme kuwa sawa na mali ya familia.
Japo simuonei huruma Nape
kwa yaliyompata hasa ikizingatiwa alichangia kikubwa kuyaunda, nampongeza kwa
kufia ukweli. Socrates (469 B.C. to 399 B.C), mwanafalsafa wa zamani wa
Kigiriki aliyesifika kwa kupenda ukweli aliwahi kunena “do not be angry with
me if I tell you the truth” yaani usinichukie ninapokwambia ukweli. Yesu
naye alisema ‘tuitafute kweli; kwani itatuweka huru.’ Hii maana yake ni kwamba
mtu anayechukia na asiyependa kweli si huru. Anahitaji uhuru hata kama ana
uhuru wa kisiasa. Je hatuhitaji uhuru utokanao na kweli hata kama unawaudhi
wenzetu tena wenye madaraka? Je kadhia inayomkabila mkuu wa Mkoa wa Dar Es
Salaam, Paul Makonda ya kughushi vyeti vya kitaaluma na kuvamia Clouds si
ukweli tunaoutaka kama jamii ili, licha ya kutendeana haki kwa usawa, utuweke
huru? Nani huyu mtumwa asiyependa kujua kweli imuweke huru? Je tunaweza
kushindana na kweli na kuishinda tukawa salama kama jamii na taifa? Leo
tutakwenda na falsafa ya Socrates tokana na mfano bora alioacha wa kuitafuta kweli
hata kwa gharama ya maisha yake kama ilivyomtokea pale aliposhitakiwa kuwa
alikuwa akiwaharibu vijana kwa mafunzo yake. Baada ya kuhukumiwa kunywa sumu
aina ya Hemlock au Conium maculatum, Socrate alisema “yapo
maarifa ya kweli na katika kujua hili hujui kitu.”
Tukirejea kadhia zetu hapo
juu, nani hajui kuwa mengi yaliyojitokeza ni ya kweli? Nani hajui kuwa tumeanza
kujenga taifa la watakatifu wasiokosea, wanaojua kila kitu na taifa la wasio na
haki wala maarifa ukiachia mbali stahiki na haki ya kueleza mawazo yao? Nani
huyu fedhuli anaweza kufunga mawazo? Je inawezekana? Ukijua hili jua hujui na
kama hujui kuwa hujui basi hujui na utajua,
Tumalizie kwa mfano wa
Socrates kuwa tusiogope kusema ukweli kwa kuhofia kufukuzwa, kunyamazishwa au
kutishwa. Ukweli utabaki kuwa ukweli kuwa mambo yanavyokwenda, licha ya kuwa
tofauti na mategemeo yetu, sivyo ndivyo. Uhuru wetu kama wana jamii una thamani
na gharama ambavyo hakuna anayeweza kuvipoka huku nasi tukiangalia. Ama!
Tanzania imefikia hapa!
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano leo.