Tukio la kusikitisha la kinyamana na kipumbavu lilotokea Oktoba 1, 2016
huko kijijini Iringa Mvumi lilistua na kuchukiza wengi ukiachia mbali kwa
taifa. Wataalamu wawili wa Udongo na
dereva wao toka kwenye kituo cha Seliani mkoani Arusha waliuawa eti kwa
kudhaniwa ni wanyonya damu au mumiani.
Hii maana yake ni kwamba bado tunajenga taifa la watu mbumbumbu,
washirikina na wakatili wanaoweza hata kuondoa uhai bila kujiridhisha kuwa kile
wanachoshuku ni kweli au siyo. Tukio hili lilitangazwa na kulaaniwa nchi nzima
wakati ule. Hata hivyo, baada ya kujitokeza upungufu wa namna hii kwenye uelewa
na imani za wananchi wetu, wahanga walizikwa na huo ukawa ndiyo mwisho wa habari
yao. Hatujui nini kilitokea kwa familia za wahanga kuhusiana na stahiki zao
kama mafao, fidia na mengine kama haya. Leo kwa makusudi mazima, tunajikumbusha
tukio hili la kikatili na kutisha lau kukumbushana kama jamii na taifa ili
kuepuka kurudiwa mahali pengine nchini.
Kwanza, tunajitahidi kuvaa viatu vya wahanga au wapendwa wao kuona nini
tungetaka tufanyiwe baada ya kukumbana na mkasa kama huu ambao bila shaka
mwenye kulaumiwa ni serikali kwa kutowaelimisha watu wake vya kutosha ukiachia
mbali kutokuwa na mfumo wa haraka wa mawasiliano ambao ungeweza kuepusha vifo
hivi vya wataalamu na hasara ambayo taifa lilipata tokana na ujima na upumbavu
huu.
Ni bahati mbaya kuwa wahanga wa kadhi ahii walikuwa wakipambana na kutumia
ujuzi wao kuwasaidia hawa hawa waliowaua kutokana na hisia na imani za
kipumbavu. Ni hasara na unyama kiasi gani? Tunashauri serikali ieleze namna
ambavyo ilizifidia familia za wahanga wa ujinga wa taifa unaotishia
kuliteketeza taifa letu. Kama haijafanya hivyo, tunaandika kuikumbusha wajibu
wake hasa ikizingatiwa kuwa wahanga waliacha wapendwa wao waliokuwa
wakiwategemea.
Inashangaza kuona baadhi ya watu
wetu wakishabikia na kushiriki mauaji ya kujichukulia sheria mikononi kama vile
kuchoma moto vibaka wakati wakiabudia na kuvumilia mibaka mikubwa tu. Lazima
tuseme wazi kuwa kosa hili si la wauaji wa Iringa Mvumi pekee bali taifa kwa
ujumla hasa wale walioteka uhuru wetu na kuwajaza watu wetu ushirikina na
ujinga. Kusema ukweli, tuna mfumo mbovu wa kishirikina na kipumbavu ambapo
matapeli wachache huruhusiwa kuhubiri sumu ima kupitia dini au uganga wa
kienyeji. Rejea mauaji ya mara kwa mara ya watu wenye ulemavu wa ngozi.
Je sasa nini kifanyike? Tutaotoa baadhi ya maangalizo hapa ili kuepusha
kurudiwa kwa aibu na unyama huu ambavyo ni pigo kwa taifa:
Mosi, wataalamu au watu wetu wanaoingia kwenye maeneo mageni ima wapewe
ulinzi wa askari au waruhusiwe kupeperusha bendera ya taifa kwenye magari yao.
Kwani, watu wetu wamezoeshwa kuogopa bendera kama alama ya serikali.
Pili, wananchi wetu waelimishwe namna ya kuheshimu na
kutumia sheria. Inasikitisha kuona kwenye karne ya 21 bado Tanzania ina watu
wasiojua hata namna ya kuripoti matukio au watu wanaowashuku hadi
wanajichukulia sheria mikononi kama ilivyotokea hivi karibuni huko kwenye
kijiji cha Iringa Mvumi mkoani Dodoma. Jambo linaloonyesha kuwa
tumefika pabaya sana kimfumo na kijamii ni ile hali ya serikali kuchukulia
mauaji husika kwa wepesi sana. Kama ingekuwa inachukulia kadhia kama hii kwa
uzito, tungesikia lau bungeni suala kama hili likijadiliwa na wabunge ili
kuangalia nini kifanyike. Wahanga wa Iringa Mvumi wamesahaulika; na hakuna
anayewaongelea ili kuepusha kadhia kama hii kutokea tena nchini.
Sijui kama waziri wa mambo ya ndani analo tena kwenye
kumbukumbu zake hasa wakati huu mauaji mengine kama yanayoendelea Kibiti
yanaposhamiri. Vinginevyo, tungesikia lau wamepewa hata nishani au zawadi za
utumishi bora katika mazingira hatarishi ambayo yaliwagharimu maisha yao. Lazima
wahanga wakumbukwe kwa namna ya pekee. Kwani walikufa kazini wakitekeleza kauli
ya “Hapa Kazi Tu” ya rais John Magufuli ingawa hakuliona hilo. Namuuomba na
kumshauri rais aliangalie hili kwa uzito wa pekee ili kujua namna familia za
marehemu zinavyoendelea.
Mwisho, katika kuwakumbuka wahanga wa Iringa Mvumi,
serikali iangalie namna nyingine ya kukomesha kadhia hii ni kwa serikali
kuwachukulia hatua watendaji wake waliowezesha kujengeka mazingira ya uhasama
na kutoaminiana miongoni mwa wanakijiji uaji ambao inasemekana walishachoshwa
na mauaji yanayodaiwa kutekelezwa kwa maagizo ya mwanakijiji mwenzao aliyekuwa
akilindwa na wakubwa wilayani Chamwino kama gazeti moja la kila siku
lilivyofichua. Hawa walipaswa kuwa korokoroni huku uchunguzi wa kina ukiendelea
ili kupata ufumbuzi wa kudumu. Hii ndiyo namna ya pekee ya
kuwafariji jamaa za marehemu na kuwaenzi marehemu waliokufa kutokana na ujinga
ulioachiwa kutamalaki nchini ukiachia mbali imani za kishirikina ambacho ni
chanzo kizuri cha mauaji haya. Hivi kweli Tanzania bado kuna mumiani katika
karne ya 21? Ni aibu kiasi gani!
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano leo.
No comments:
Post a Comment