Kwa waliobahatika kusikiliza mahubiri ya wiki iliyopita ya “mchungaji” Josephat Gwajima, walishangaa sana. Pamoja na kujulikana namna anavyojitahidi kutumia madhabahu kufanyia siasa, alichosema kwenye mahubiri ya wiki iliyopita–kama vyombo vya usalama havitayafanyia kazi–basi taifa letu linapelekwa pabaya. Mahubiri haya yamo kwenye yutube kwenye kiunganishi hiki https://www.youtube.com/watch?v=UFnUdPzMvHU
Katika mahubiri haya Gwajima anasikika kuwa kuna watu wana nia mbaya na Tanzania wanaolenga kumuua waziri mkuu mstaafu Edward Lowassa. Anaendelea kusema kuwa hao anaowajua Gwajima wakishafanikiwa kumuua Lowassa, wapenzi wake watasema aliyefanya hivyo ni Magufuli. Hivyo, wapenzi na marafiki wa Lowassa watamuua Magufuli. Kwanza, ukiangalia dhana nzima unapata shaka na uhalisia na ukweli wake.
Kwanza, unajiuliza, inakuwaje Gwajima ajue mpango huu tena unaohusu kuondoa maisha ya kiongozi wa nchi asipeleke kwenye vyombo vya usalama mara moja kabla ya kutangaza na kuwastua wahusika kama kweli madai yake ni ya kweli?
Pili, kwa wanaojua namna Gwajima alivyotatanishi hasa kujulikana wazi alivyomuunga mkono Lowassa halafu akajitahidi bila mafanikio kumuepuka, anaweza kusema hata kuzua lolote ilmradi apate hadhira na kujiweka karibu na watawala.
Tatu, kwa waliofuatilia vita yake na mkuu wa mkoa wa Dar Es Salaam, watakubaliana nasi kuwa Gwajima amekuwa akijitahidi kusema maneno yanayolenga kumpendeza rais bila mafanikio. Amejitahidi kujionyesha kama mtu anayelipenda taifa lakini akashindwa kuonyesha kwa vitendo hasa ikizingatiwa kuwa kazi ya kuhubiri anayofanya imejaa utata kama madai ya kufufua watu, au yeye kupooza na kupona kwa maombi akionyesha alivyo na nguvu za ki-Mungu ingawa kitendo chake cha kuzungukwa na mabaunsa na kuwa na bundiki kinakinzana kabisa na anacholenga kuiaminisha jamii.
Nne, tangu atuhumiwe kujihusisha na biashara ya mihadarati, Gwajima amejitokeza kama mtu anayejitahidi kumshauri rais kiasi cha kutia shaka kuwa kuna kitu nyuma ya pazia kinachomhangaisha kiasi cha kutaka apate sikio la rais.
Tano, kuna swali moja kubwa la pili licha ya lile kwanini Gwajima hakuripoti kwenye vyombo vya usalama juu ya hatari dhidi ya uhai na maisha ya kiongozi wan chi ambalo ni je tumpuuze Gwajima au tujiulize imekuwaje ajiamini kama hajui kitu? Je Gwajima ni mshirika katika mipango hii michafu dhidi ya viongozi wa nchi? hata hivyo, Gwajima ana bahati. Kwani, ni Tanzania pekee ambapo mtu anaweza kutoa madai makubwa kama haya akaendelea kuwa uraiani akipanga mengine.
Sita, kama nilivyoeleza hapo juu, Gwajima anajitahidi kufanya siasa kwa mgongo wa madhabahu jambo ambalo ni kinyume na mazoea na sheria za Tanzania vinavyokataza kuchanganya dini na siasa ingawa watawala wanafanya hivyo, kwanini hakemewi au kuna wanaomtuma ili kuongeza umaarufu kama si kuiondoa jamii na hadhira kwenye mambo muhimu kama vile kashfa iliyofichuliwa na Mkaguzi na Mdhibiti wa Fedha za Serikali (CAG) inayowagusa wakubwa? Je kuna anayemtuma Gwajima au anajituma; ili iweje na kwanini na nini matokeo ya mchezo huu wenye kukera na kila aina ya uchafu?
Je Gwajima ana mizigo inayomsumbua ukiachia mbali kutuhumiwa kujihusisha na mihadarati kama vile kumilki mali zisizo na maelezo zilivyopatikana? Kuna haja ya serikali kuwapa wananchi maelezo juu ya watu wanaoamka na kutoa madai makubwa na ya ajabu ambayo yanaweza kuyumbisha taifa.
Katika kumtambulisha Gwajima tumeweka mabano kwenye cheo cha mchungaji kwa makusudi mazima hasa ikizingatiwa kuwa cheo chake ni cha kujipachika, jambo linalomnyima uhalali wa kutumia cheo hicho. Tumalizie kwa kumshauri Gwajima yafuatayo:
Kwanza, kama madai yake ni ya kweli, aeleze ni kwanini hakutoa taarifa kunakohusika tena haraka alipogundua huo mpango mchafu kama ni kweli na upo.
Pili, aache kumdhihaki rais wala kumhusisha kwenye harakati zake za kutaka umaarafu.
Tatu, achunguzwe si akili tu dhamira ya kutoa madai kama haya kama hatayatolea ushahidi unaoingia akilini huku akieleza ni kwanini hakutoa taarifa kwenye vyombo na taasisi husika.
Nne, achague moja kati ya kuhubiri dini au kufanya siasa ili ajulikane yuko upande gani. na hili kwake ni rahisi. Ana wafuasi tayari na fedha. Hivyo, anaweza kuunda chama badala ili aone mikiki ya siasa badala ya kujificha nyuma ya majoho.
Nne, afahamu kuwa, kwa nafasi yake yenye kutia tata, hawezi kuheshimiwa na jamii na watawala sawa na wale waliopata uongozi wa kiroho kama vile shehe mkuu na muashamu kardinali na viongozi wengine wa madhehebu yanayoheshika ambao mara nyingi hujitenga na siasa na wanapotoa matamko huwa na mashiko.
Mwisho, tunaiasa serikali isikali kimya madai mazito yenye kuhusisha viongozi wazito wa taifa kama haya. Hivyo, Gwajima abanwe aeleze anachojua, alikijua lini na nini uhusika wake. Kama ni gea ya kutafutia mlo na umaarufu vile vile ijulikana ili aonywe au kufunguliwa mashitaka ya jinai kwa kutaka kuyumbisha taifa na kuvuruga amani na mshikamano wa kitaifa. Pia achunguzwe kama sifa za kutenda miujiza anazodai kuwa nazo anazo kweli. Na kama hana, leseni yake ya kuhubiri ifutwe kutokana na kupotosha umma.
Chanzo: Tanzania Daima Jumapili leo.
No comments:
Post a Comment