Baada ya zoezi la kuhakiki vyeti feti kukumbwa watanzania wanaokaribia 10,000 bila kuhusisha wafanyakazi kwenye taasisi binafsi na viongozi wengine wa kisiasa wa umma, kuna haja ya kujiuliza maswali mengi mazito na magumu. Je kadhia ya kughushi ilianza lini na kwanini? Je nini dawa yake mbali na kufuta kazi walioghushi au kuwapeleka mahakamani. Nadhani kuna haja ya kwenda mbali na kuangalia mfumo wa kisiasa unaoendesha taifa letu hasa baada ya ufisadi na jinai zinazowezesha watu kutajirika haraka kiharamu bila kushughulikiwa kisheria. Nimekuwa mpenzi na mtetezi mkubwa wa kurejesha sheria ya maadili inayoruhusu serikali kukamata mtu na mali yoyote inayoaminiwa kupatikana kinyume cha sheria. Nimekuwa mpenzi wa kutaka kila mtu mwenye utajiri aeleze alivyoupata na si mtu kulala maskini na kuamka tajiri.
Leo nitaongelea kadhia ya vyuo feki ambavyo ima vinatoa elimu feki, shahada feki hata picha mbaya kwa watanzania kiasi cha watu kuacha kujipinda na kusoma badala yake wakategemea kupata shahada za chapchap feki na za ubwete. Namna hii hatuwezi kuendelea kama taifa. Lazima turejeshe Tanzania kwenye miaka ya 70 hadi 90 ambapo elimu ilikuwa ndiyo njia ya uhakika katika maisha bora na mafanikio. Turejeshe Tanzania kwenye nyakati za elimu ni ufunguo badala ya ufunguo kuwa madawa ya kulevya, ufisadi, kughushi na jinai nyingine.
Hivi karibuni nilistuka niliposoma kwenye mtandao kitu kinachoitwa Africa Graduate University ambacho ni chuo kinachoonyesha kila aina ya shaka. Kilichofanya nistuke na kudurusu ni namna chuo husika kinavyofanya mambo tofauti na vyuo vingine na utamaduni wa kitaaluma. Mfano, chuo husika kilikuwa kikitangaza kutoa shahada za juu yaani PhD kama njugu; tena kwa kutumia vigezo vya ajabu kama vile mtu kutunga kitabu au kufanya jambo fulani kwenye jamii na kupewa PhD. Hivi kama mtu anatunga kitabu kimoja hata kiwe cha kitaaluma anapewa PhD, kwa waandishi kama sisi wenye vitabu vingi tu vya kitaaluma na visivyo vya kitaaluma tupewe uprofesa? Kwa kutoa shahada kwa mtu kutunga kitabu ni ushahidi kwa mhusika kuwa hajui maana ya shahada anayotoa na hata anayeipokea kutokana na wote kuwa vihiyo. Huu ni ushahidi kuwa chuo hiki ni cha hovyo na cha kisichojua maana ya kuwa chuo ukiachia mbali kutojua maana na uzito wa PhD. Je kuna biashara inayofanyika nyuma ya pazia kwa wapenda udaktari wa heshima ambao wengi ni wavivu wa kusoma na kusaka elimu? Haiwezekani eti mtu anaendesha NGO ya kawaida anatunukiwa PhD ya heshima (Honoris causa).
Mkuu wa chuo hicho Profesa Steven Nzowa alikaririwa akisema “tunao watunuku tuzo hizi tuzo za heshima ni watu waliokuwa na umri wa miaka 60 ambao wanafanya kazi za kijamii katika nyumba za ibada kwa zaidi ya miaka 15 na kuendelea na wale ambao umri wao ni miaka 40 hadi zaidi na wenye shahada.” Sijawahi kusikia vigezo kama hivi. Kama vingekuwapo akina Kardinali Polycap Pengo wangekuwa na magunia ya shahada.
Mtu anafanya shughuli za NGO za uongo na ukweli; anapewa PhD. Hivi hawa wanajua maana na uzito a PhD au ni ujinga unaowasumbua. Baada ya wamilki wa papermills kama hizi kuzitangaza, nilihisi wana baraka toka serikalini jambo ambalo nalo ni ajabu na hatari kwa mustakabali wa taifa.
Chuo hadi kiwe na hadhi ya kutoa PhD siyo kuwa chuo tu bali lazima kiwe na ithibati na uzoefu na fedha. Kwa waliosoma vyuo vikuu nje ya nchi, kuna vyuo vingi maarufu lakini havina programs za PhD. Kinachoshangaza ni ile hali na vigezo vinavyotumiwa kutoa hizo PhD hata jina la chuo halina maana kitaaluma. Hakuna kituko kilichoniacha hoi kama kusema eti makao makuu ya chuo hiki yako nchini Sierra Leone. Katika tovuti ya chuo hiki kuna yafuatayo:
CURRENT STATUS: A) National: Today, Africa Graduate University-Sierra Leone with 2,300 to 2,500 students comprises three campuses such as: i) The College of Professional Studies Freetown Campus( delivering Certified NCTVA & ICM Certificates, Diplomas and Higher Diplomas) ii) The College of Professional Studies Mile 91 Campus (delivering Certified NCTVA Certificates, Diplomas and Higher Diplomas) iii) The Africa Graduate University College Freetown ( delivering online and on-campus Courses in Graduate and Postgraduate levels. Ukiangalia kwa umakini, ni kwamba chuo husika kinatoa vyeti na stashahada lakini si shahada kamili. Kituko zaidi ni pale chuo kinapodai kinatoa masomo ya uzamili online. Hii ni ajabu sana. Sijawahi kusikia wala kuona PhD ikifanyika online na ikawa na ithibati sawa na zile za kusomea darasani.
Kwanini huko na si hapa? Kwa wanaojua mambo yanayoendelea kwenye baadhi ya mataifa ya Afrika Magharibi, hili pekee litaanza kuamsha mashaka juu ya ithibati ya chuo husika. Kuna haja ya mamlaka zinazohusika na kusajili vyuo nchini kuwa makini na vyuo vyenye kutia shaka ili kuepuka kuigeuza Tanzania kitovu cha shahada chafu na feki almaarufu papermill.
Inashangaza watu wazima kiumri tena wanaojiita watumishi wa Mungu kuchezea kitu muhimu kama elimu. Au ni kwa vile haikuandikwa kwenye vitabu vyao vya dini kuwa kuchezea elimu ni dhambi wasijue kusema uongo ni dhambi iliyoanishwa inayoangukia kwenye hiki wanachofanya. PhD hata kama ni ya heshima ina vigezo vyake; na haitolewi kama pipi kama ilivyo kwa hiki kituko kiitwacho Africa Graduate University.
Tumalizie kwa kuzisihi mamlaka zinazohusika kuchunguza vyuo vya kutia shaka kama hivi ili kuepusha watu wetu kuendelea kutapeliwa na kuamini kuwa wanaweza kupata hadhi ya kitaaluma dezo bila kustahiki wala kuzisotea. Hii nayo ni aina fulani ya kughushi na ufisadi katika elimu. Vyuo vya namna hii vinapaswa kufungwa haraka na wahusika kuchukuliwa hatua kuanzia watoaji na wapokeaji.
Chanzo: Tanzania Daima Jumapili leo.
No comments:
Post a Comment