Baada ya taarifa za kufumka kashfa ya ufisadi wa kutisha
ambapo mhalifu fulani wa Tume ya Kupamba na Kueneza Rushua, sorry Kupambana na
Kuzuia Rushua (TAKUKURU) kukutikana akimiliki mimali yenye utata ya mabilioni,
Kijiwe kinataka kuisaidia sirikali kuanza kuwafichua wote wenye utajiri wa
kutia shaka tena ambao wanajulikana hata kwa kunguru.
Mpemba ndiye analianzisha leo. Baada ya kuamkua anakula
mic “yakhe mmesikia hii skandali ya mkubwa wa kuzuwia rushua kukutwa na ukwasi
mkubwa utokanao na kadhia aloajiriwa kupambana nayo akaishia kuishirika na
kuipamba?”
Kapende anajibu “nimeyasikia haya japo sijashangaa. Hakuna
jipya hapo. Hao mbona wengi na wamefanya kaya yetu iwe maskini kwa kupewa cha
juu na kuacha ihujumiwe na magabachori na sasa wachukuaji waitwao wawekezaji
ukiachia mbali wazungu wa unga? Mbona wanajulikana na kila mtu hata ndege na
wadudu? Hapa nadhani suala si kuongelea kutokea kwa hili bali namna ya
kupambana nalo; au vipi?”
Mgoshi Machungi anachomekea “nakubaiana nawe. Hapa lazima
tianzishe utaatibu wa kia mwanakaya kutangaza, kukaguliwa na kueeza namna
aivyochuma ukwasi wake ii tisiendee kuibiana kama iivyo sasa ambapo mbuua
wachache wanaendee kugeuza kaya yetu shamba la chizi. Tena katika kutangaza
ukwasi wetu tiepuke mambo ya kibashitebashite kama iivyo sasa ambapo kaisai
ameonyesha wazi kumbeba habithi huyu hata aiposhutumiwa kuwa na mimai kibai
yenye kutia shaka.”
Mijjinga anakula mic “hata nami nakubaliana na wazo la
kuamua kuwatolea uvivu wezi wetu ambao wengi wao wanatukoga utadhani wamechuma
kwa stahiki au ujanja wao. Hapa, kama kijiwe, tuanze kuzitambua mali husika,
ziko wapi, ni kiasi gani, zinamilkiwa na nani, halafu tuzivujishe kwenye vyombo
vya habari. Nashangaa hata vyombo vyetu vya habari vimeshikilia siasa badala ya
kufanya uchunguzi wa majambazi kama hawa ili watiwe adabu na kurejesha njuluku
zetu.”
Kapende anakula mic “Mijjinga hapa umemena bro. lazima
tufanye utambuzi kwanza ili tuanze ukamataji au uvujishaji wa mali husika. Ni
rahisi kuwatambua wezi wetu waliotumia ofisi zetu kujineemesha. Mfano, unakuta
kijana kamaliza shule mwaka juzi tu lakini ghafla bin vu anatokea kuwa tajiri
wa kutisha. Hapa lazima tuanze kuhoji wote kuanzia zama za mzee Ruksa ili
kuwatendea wachovu haki. Haiwezekani tukaendelea kuhubiriwa na watawala kuwa
wana nia ya kupambana na ufisadi wakati wakiwafumbia macho mafisadi na wezi
kama hawa wanaotumia ofisi za umma kujineemesha na kuhujumu kaya. Mie nawajua
mia kidogo; na niko tayari kuwataja ili washughulikiwe vilivyo.”
Msomi Mkatatamaa anatia guu “ni kweli; mali za wizi na
waliojilimbikiza wanajulikana. Hata ndege wanajua zilipo na ni kiasi gani na ni
za nani na anafanya kazi ofisi gani. Nadhani kinachowasaidia wezi hawa
kuendelea kutuibia na kufaidi mali zetu ni ile hali ya jamii yetu kugeuka ya
kuabudia vitu badala ya haki na utu. Wengi wa wezi hawa ni wenzetu, wanetu,
ndugu zetu na marafiki zetu. Hata hivyo, kama sirikali ikiendelea kuwadekeza
tutakwenda kuzimakamata kama noma na iwe noma; au vipi?”
Kanji naye hajivungi. Anakwanyua mic “mimi iko sikia vatu
nalalamika naonewa sana na Kufuli. Kama nasikia vanalalamika tadhani vameonewa.
Sasa kama naibia kaya nategemea ipewe sada ya ua au iweke pango naonja joto ya
jiwe kama jusi. Kama nasema Kapenda, unakuta toto dogo bila juzi vovote naanza
kazi leo. Keso nakubwa bilionea. Naangusa jengo kuba kuba, natongoza bibi
kubakuba, nakula kwa hoteli kubakuba, naendesha gari kubakuba, nahonga toto na malaya
gari kubakuba ya bei baya. Hii kama siyo chori napata vapi hii feza nachezea
kama jugu?”
Mheshimiwa Bwege anaamua kula mic “mimi nina mawazo
tofauti nanyi. Kwanini tusitunge sheria ya kuwakamata wahusika na kuwanyonga na
kurejesha mali zetu ili wezi wengine waogope kama wanavyofanya China. Ukikamatwa
umekula njuluku ya kaya China wanakunyongelea mbali bila kujali cheo, chama,
dini wala ukaribu wako na wanene kama ilivyo hapa ambapo mmeongelea kashfa ya
Bashite ambaye anatuhumiwa kukwanyua njuluku kibao lakini dingi anafanya gozi
gozi kumtumbua. Nakubaliana na wanaosema tuwasake hawa wezi. Tukiwakamata tuwafanyie
kama vibaka ili kuepuka kupelekwa lupango wakahonga na kurejea Uswazini
kumalizia mali zetu huku wakitukoga hata kuwahonga wake zetu.”
Da Sofia Lion aka Kanungaembe anakula mic “tatizo si
kuhonga wake zenu. Tatizo ni kutuibia na
kutenda vitendo vya kishenzi. Hata wangechuma kihalali, hawapaswi kuwahonga
wake zetu wala binti zenu. Mbona mnawadhalilisha wanawake; kwani hakuna wanaume
wanaoohongwa na hawa hawa wenye nazo yaani mashuga ladies siyo?”
Mipawa aliyerejea toka Morogoro kumzika mkewe anaamua
kula mic “kusema ukweli hali hii ya wachache kuiba mali za umma kwa kutumia
ofisi za umma inasikitisha sana. Juzi nilipopata msiba wa mke wangu kipenzi,
nilijua maana ya kutokuwa na kitu. Kusafirisha maiti ilikuwa ngoma usipime. Sasa
inakuwa uchungu zaidi pale unapoteseka kwa ukapa na ukata wakati kuna majambazi
wachache wakiibia kaya yako. Naunga mkono pendekezo la kuwachoma moto mibaka
hawa wakubwa. Kwanini tuwe na uwezo wa kuwachoma vibaka tushindwe mibaka
tunayoijua na kuishi nayo?”
Kijiwe kikiwa kinanoga si likapita shangingi la kijana
mmoja anayefanya kazi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa mzee Mchonga. Acha tumtoe
mkuku ili kwenda kumripoti TAKUKURU akanyang’anywe mimali aliyotuibia!
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano leo.
No comments:
Post a Comment