How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Tuesday, 9 May 2017

Kijiwe Chataka Vyeti Vya Wanasiasa Vihakikiwe Pia

Image result for photos of profesa paramagamba kabudi
            Baada ya waziri wa Utumikishaji ofisi ya rahis kuja na mpya kuwa zoezi la kuwang’oa vihiyo lilihusu wafanyakazi wa umma tu, Kijiwe kimeona hii si sawa. Ni ubaguzi na uonevu wa wazi. Hivyo, kimekuja na maangalizo kikiwataka wahusika kuacha ufisadi wa kujihudumia huku wakiwaumiza wenzao wakati jinai yao ni moja.
            Msomi Mkatatama anaingia akiwa na gazeti la Danganyika Leo. Analitua kwenye meza baada ya kuamkua na kusema “wasomi wa kweli mmeonaje hii double standard ya watawala kujihudumia kwa kupendeleana kubebana huku wakiwasulubu wachovu vihiyo kama wao tena wenye kulipwa njuluku kiduchu tofauti na mabilioni wanayozamisha kila uchao?”
            Mipawa anajibu ‘mie sishangai hasa nikiona wanavyolindana. Unategemea nini kaya inapokuwa mikononi mwa vihiyo kama Bashite ukiachia mbali wabangaizaji wanaosema hili na kutenda lile? Huwezi kusema kuwa wanasiasa si watumishi wa umma wakati wako kwenye ofisi za umma. Kama alivyosema Tunda Lishu, anayesema hivyo anasema ujinga; naye ni mjinga pia. Kimsingi huu ni ujinga wa kimfumo kuanzia chini hadi juu.”
            Mpemba anaamua kula mic “wallahi hata mie nshangaa sana. Hivi hawa akina Bashite kweli si vihiyo waniopaswa kutupwa lupango kwa kughushi vyeti? Sasa kama twatumia sharia kibaguzi hivi, kweli tutaendeleaje wakati tunichofanya ni haramu na hatari kama kaya?’
            Mgoshi Machungi anamchomekea Mpemba “haya maigizo yamenichefua kwei kwei hadi kuhisi kizhunguzhungu. Hawezekani vihiyo wanaojuikana waendelee kuukata wakati wachovu wakifukuzwa. Hii si haki tate nane. Hakuna kiichonikea kama hawa wanaotibagua kutidanganya kuwa wapo pae kwa kia mwanakaya wakati si kwei.”
            Mipawa aliyekuwa akisoma gazeti anaamua kutia guu “sijui wenzangu mnashangaa nini iwapo mlishaambiwa kuwa mengine ni makaburi ambayo wanene wanaogopa kuyafukua wakashindwa kuyafukia? Mie sishangai hasa nikizingatia kuwa siasa zetu ni za wenye ulaji lakini si za waliwa. Sisi tunakuwa na thamani pale tunapopiga kura ya kula. Baada ya kupiga kura ya kuliwa, wahusika wanajifanyia watakavyo bila kujali wala kusikia vilio vyetu. Inakuwaje wafanyakazi wa umma watakiwe kuwa wasomi wa kweli wakati viongozi wao wakiruhusiwa kuwa vihiyo, kughushi na kufanya kila aina ya upuuzi? Haiwezekani watendaji wasomi walioiva wakakubali kuongozwa na vihiyo ambao sifa yao ni eti kujua kusoma na kuandika. It doesn’t make any sense. Nonsense. Utter nonsense.”
            Kanji aliyekuwa akinong’ona jambo na mheshimiwa Bwege naye anaamua kula mic “mimi iko sangaa sana dugu zangu. Kwanini ongozi iwe Kihiyo na tumishi iwe somi? Kama Hiyo naongoza Somi hapa takuwa gongano sana. Kwa sababu hiyo hapanajua plans za Somi. Kama naruhusu kaya tawaliwa na Hiyo basi dugu yangu kaya taangamia.”
            Mheshimiwa Bwege anaamua kutia guu “Kanji nakuunga mkono. Nadhani ni kutokana na kuongozwa na vihiyo ndiyo maana tumekuwa tukiruhusu wezi waitwao wawekezaji ambao kimsingi ni wachukuaji kutuibia madini kwa kisingizio eti cha kupeleke mchanga nje kuchunguzwa. Kwani unaumwa au ujinga na ukihiyo wetu ndiyo wametumia. Ni kutokana na kuwa na vihiyo wengi wa kisiasa ndiyo maana tulijenga bomba la gesi la bei mbaya tena kwa kuruhusu kila kitu kutoka China. Nadhani ndiyo maana tumejaza magabacholi wanaoishi kayani kinyume cha sheria tena wakiajiriwa wakati vijana wetu wakizidi kuozeana kwa kutokuwa na ajira.” Anapiga chafya na kuendelea “ ningependa tuondoke hapa na azimio la kwenda mjengoni kuwataka wahishimiwa kubadili katiba ili kila mchovu ahakikiwe elimu na mali yake bila kubaguana wala kukoromijiana kama ilivyo. Hatuwezi kuendesha kaya hivi tukawa salama kama alivyosema Kanji.”
            Kabla ya kuendelea Sofia Lion aka Kanungaembe aliyeenguliwa hivi karibuni toka Chama Cha Maulaji anakula mic ‘kaka hapo umenikuna kweli kweli.”
Kabla ya kuendelea Mbwamwitu anamchomekea “Hebu tueleze vizuri, amekukuna wapi na vipi?”
            Sofia anabeua midomo na kusonya na kuendelea “tunajadili mambo ya maana wewe unaleta utani. Basi umekunwa wewe.” Anamgeukia Mbwamwitu na kusema ‘hebu kaka tuache utani. Inauma kweli kweli.”
            Kabla ya kuendelea Mbwamwitu anamchomekea tena huku akicheka “nini inauma hiyo?”
Da Sofia anaendelea “kama haikuumi kuona namna wachovu wanavyofukuzwa kazi kwa kughushi huku wanasiasa tena wenye mavyeo makubwa wakiendelea kutesa pamoja na kujulikana wazi basi huna hisia wewe.”
            Mijjinga aliyekuwa akisikiliza kwa makini anaamua kukatua mic “tuache utani na kupotosha. Kweli inauma sana kama alivyosema da Sofi. Haiwezekani wasomi kama sisi tukose ajira wakati kuna vihiyo kibao kwenye ofisi za umma. Msimamo wangu ni kwamba vihiyo wote wawe watumishi wa umma au wanasiasa wapigwe chini nasi tupate ajira. Hii kaya ni yetu sote kwa usawa. Kama alivyopendekeza mheshimiwa Bwege, lazima tuondoke hapa na azimio la ima kwenda njengoni au ikuu kushinikiza tutendewe haki kwa kuhakiki vyeti vya wanasiasa.”
            Kijiwe kikiwa kinachangamka si likapita shangingi la waziri wa uhakiki wa vyeti. Acha tumtolee mabango kukosoa ubaguzi wake wa kitaaluma. Kwa vile hatukuwa na ubaya naye, tulimpa ofa ya kahawa akanywa na kuondoka akiwa ameelewa na kutuahidi kutofanya uhakiki kijinga bali kiweledi kwa kuhakikisha wanasiasa nao wanahakikiwa na kutimliwa.
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano kesho.

No comments: