The Chant of Savant

Monday 6 May 2019

Barua kwa Reginald Mengi (Marehemu)


Image result for photos of reginald mengi

Bwana Reginald Mengi,
Salamu huko kwenye maisha yako mapya.  Sina haja ya kukuuliza kama hujambo au la hasa nikizingatia na hali ya uliko kwa sasa ambako ni safari yetu sote. Kwa heshima niruhusu nikujulishe yafuatayo:
Mosi, tangu ulipoanga dunia hapo usiku wa kuamikia tarehe 2 Mei, umegeuzwa malaika. Wengi wanaimba sifa zako bila kutaja kasoro zako lau wakutendee haki. Wengi wanaogopa kusema ukweli juu yako ili wasilaumiwe au kuonekana wabaya wakati binadamu ana sifa zote ubaya na uzuri. Hakuna mwenye sifa nzuri wala mbaya pekee; wala hakuna binadamu malaika wala shetani. Hata katili wa kutisha kama vile Adolf Hitler, Augusto Pinochet, Pol Pot, Nikita Khrushchev, Nicolae Ceausescu, Samuel Kanyon Doe, Joseph Stalin na wengine wengi walikuwa na ubaya na uzuri wao. Hayo ndiyo maumbile yetu binadamu. Hivyo ninapoandika ninayoandika haimaanishi kuwa nakuchukia wala kukuzushia.
Pili, naomba ufahamu kuwa waraka wangu ni mwakilishi wa wale ambao ima kwa kutojua au vinginevyo uliwakwaza hasa waandishi na wachangiaji kwenye vyombo vyako vya habari. Mimi ni mmojawapo ambaye umeondoka na deni langu baada ya kuandikia magazeti yako ya Nipashe Jumamosi na the Guardian on Sunday kwa miaka mitatu bila malipo. Niliwasilisha madai yangu kwa wahasibu na wahariri wako bila majibu ukiachia mbali kukumbushia mara kwa mara kupitia blog hii.
Tatu, fahamu kuwa umeondoka si na deni let utu bali pia kutokutulipa hasa wale wanaotegemea malipo haya ni mateso kwa familia zetu. Hivyo, wanaokusifia, japo kwa kujua wakafanya makusudi au kutojua, wanapaswa kulijua hili ili liwe somo kwao wanaopenda kusifia watu huku wakifunika mapungufu yao.
Bwana Mengi,
Umeondoka kwenye dunia hii ya kimwili. Mojawapo ya urathi wako pamoja na kusifika kusaidia wanyonge, kuna wengine wanyonge tena waliomwaga jasho lao kukutumikia hukuwatendea haki. Wapo watakaokusamehe na wapo ambao hawatakusamehe ukiachia mbali kuwafikisha mahakamani warithi wako.
Mie naandika kama binadamu nikiwasiliana nawe kama binadamu ili kuondoa mazoea mabaya na unafiki wa kusifia waliokufa na kuwaumiza walioumizwa nao. Nataka niwe mkweli na muwazi kama alivyowahi kuwa rais John Pombe Magufuli kwenye msiba wa mtu mmoja aliyekuwa ameacha wake wengi lakini kwenye msiba akatambulishwa mmoja kiasi cha kumlazimisha rais kuondoa unafiki na kusema alimjua marehemu kama mtu mwenye wake Zaidi ya mmoja. Nawe kama Binadamu wapo uliowakwaza na wapo waliokukwaza pia. Hivyo, huu ni wakati wa kusameheana na kuombeana toba.
Hivyo, rais alitaka wake wengine na watoto wao wasidhulumiwe. Nami nataka kuwaambia wanao na watakaokurithi wasiwadhulumu waliochangia kwenye vyombo vya habari bila kulipwa haki zao na kuachwa na unyonge wao. Maana haiwezekani mtu uwe na uwezo wa kuwajengea watu majumba na hata zahanati na kutoa mikopo kama tunavyosikia mashuhuda wako ushindwe kuwalipa watu waliomwaga jasho lao wakitumikia makampuni yako kama sisi tuliochangia kwenye vyombo vya habari ambao wanawakilishwa na waraka huu.
Hivyo, sitaki niseme mengi. Nakutakia safari njema ambayo ni yetu sote japo kwa muda tofauti. Nasisitiza kusema kuwa nimejitahidi kujitenga na woga hata unafiki wa kukusifia bila kueleza upande wa pili. Huenda kwa nafasi yako kama mtu Tajiri na mkubwa kuna mengi walitenda wa chini yako kwa kuwadhulumu wanyonge na kuziba nafasi ya kukuona. Kwa ulipo sasa ungetamani haya uyajue mapema ili usiondoke na deni. 
Mwisho, wamejitokeza vizabazabina na wapenda sifa waliotunga hadithi chafu na za kunuka kuhusiana na msiba wako hata kumhusisha mkeo. Wapo watasingizia mengi. Hata hivyo, kwa mahali ulipo, wote wanazidi kujichumia dhambi na kujipalia mkaa.
Pumzika mahali pema peponi Reginald Abraham Mengi.

No comments: