The Chant of Savant

Sunday 20 September 2020

KWA WENZETU KULIPA KODI NI SAWA NA KIFO HAIEPUKIKI

Baada ya serikali ya rais Magufuli kubana matumizi na kuimarisha ukusanyaji kodi, huwa napata malalamiko ya baadhi ya marafiki zangu kuhusu kodi. Huwa nashangaa ikizingatiwa kuwa mazuri yote ambayo nchi yetu imeyafanya na kuyafikia haraka yangekuwa ndoto kama ukusanyaji kodi usingefanyika vilivyo. Hata hivyo, sishangai sana. Malalamiko hutokana na ukweli kuwa wengi hawakuwa wamezoea kulipa kodi vilivyo ima kutokana na mfumo wa kijamaa tulianza nao au kutojua umuhimu wa kufanya hivyo kwa faida ya nchi na wananchi wake. Sababu nyingine ni uzembe wa serikali kuhimiza kukusanya kodi. Hapa Kanada, kulipa kodi ni sehemu ya ustaarabu na utaratibu wa kawaida. Si kulipa kodi tu bali hata kujaza taarifa za mwaka za kodi kwa kila mwananchi na mkazi ambaye si mwananchi wa hapa. Kulipa kodi hapa kunafanyika kwa njia ya kukatwa pesa moja kwa moja toka kwenye kila unachonunua. Ukiingia dukani, utakuta bei ya kila kitu imeandikwa. Kama maandishi yanasema bei ni kiasi fulani, ukikubali kulipa, utaongezewa kodi ya serikali. Hivyo, bei huongezeka tofauti na ile iliyoandikwa. 
             Kitu kingine, kila unapolipia manunuzi lazima upewe risiti tena siyo lazima uiombe. Hata usipopewa, kwa wale wasiotaka kudai baadhi ya fedha zirejeshwazo kwenye manunuzi yao, muuzaji huchapisha ile risiti na kuitupa kwenye jalala. Lazima ichapishwe kwenye mashine ya manunuzi ya kielektoniki, EFD.
                    Hapa kila kipato lazima kitozwe kodi bila kujali ukubwa hata udogo wake. Malaya, watoa simu za umalaya, wacheza uchi, watengeneza matoi ya ngono, waendeshaji klabu za maonyesho ya utupu na waigizaji ngono hawawanatozwa kodi kama watu waliojiajiri.  Malaya akipata mchepuko–––hata kama anafanya hivyo kinyume cha sheria–––anapaswa kutoza kodi na kuhakikisha anatoa risiti ili mteja aamue mwenyewe kwa wanaotaka kurejeshewa fedha za manunuzi au kutunza kumbukumbu. Kisheria, mabaya haya huitwa malum in se (baya lenyewe) au malum prohibitum (baya likatazwalo). David Rotfleisch wa kampuni ya Rotfleisch & Samulovitch P.C anasema kuwa malaya huruhusiwa kudai baadhi ya marejesho ya kodi yatokanayo na maandilizi ya biashara kama vile matangazo, vitendea kazi na kadhalika.
             Wenye tamaa huko Bongo, je utachana risiti au kuiweka ili udai wakati wa kujaza kodi? Utajali fedha unayodai au hatari unayotengeza hasa bi Mkubwa akiifuma? Msikonde. Huku mke na mume hufichana siri zao. Kwetu najua, umalaya ni haramu; msikonde. Hamtatozwa njuluku. Sheria husema: chochote kitokanacho na haramu ni haramu. Siwahimizi wenye michepuko kuchepuka. Bado ngoma inaua japo wap wanaojifanya kusahau. Wanagwaya Covid-19 wakati miwaya inawaramba kama haina akili nzuri.
            Japo uchangu hauwezi kuruhusiwa Bongo, hata ukiruhusiwa, wanaodai risiti watakuwa wachache au hamna. Fikiri. Unakuta: mzee aliposafiri kikazi alilipia huduma ya ngono au mwanao anayesoma chuo au sekondari ametumia njuluku unayojinyima kumwezesha, kulipia ngono. Kwa kuangalia hili, hakika, hakuna haja ya kuhalalisha umalaya. Kwani, licha ya kukinzana na maadili yetu, serikali itapoteza fedha nyingi. Vyangu watapenda pesa yao isikatwe kodi. Wateja watagwaya kudai risiti. Maana, baadhi ya maduka huku huchukua taarifa za mteja kama vile anwani, nambari za simu hata baruapepe. Hivyo, machangupaka wasingependa taarifa zao zijulikane. Hawawezi kujua lini machangu yatapiga simu nyumbani. Hiyo, tuiache. Muhimu ni kuelewa: kulipa kodi ni wajibu si wa raia tu bali hata mkazi wa nchi yeyote. Kwa Tanzania ambapo wageni inakuwa vigumu kuwapata–––kama hakuna utaratibu wa kukata kodi moja kwa moja kwenye bidhaa na huduma–––anzisheni utaratibu wa kutoza kodi kwenye bidhaa badala ya kuhimiza watu binafsi walipe kodi.
Eneo jingine ambalo lazima mhusika alipe au kusamehewa kodi ni kuhusiana na kutoa huduma fulani kwa jamii au kutoa zawadi. Ukitoa huduma kwa jamii, serikali inakupunguzia kodi. Ila ukitoa zawadi au kununua kitu ambacho si muhimu au cha anasa kama sigara au pombe na magari na matoi ya bei mbaya, kodi huwa kubwa kweli kweli. Mfano hapa ninapoishi, kopo moja la bia yenye ujazo wa juu kidogo ya nusu lita inauzwa zaidi ya dola 3.5 za hapa ambazo ni sawa na takribani shilingi za kitanzania 6,000 na ushei kutegemeana na kupanda na kushuka kwa shilingi yetu. 
        Kulipa kodi, licha ya kuwa wajibu wa mwananchi, hutuhakikishia huduma za pamoja toka serikalini. Unapolipa kodi, una haki ya kudai huduma za pamoja kama elimu, ulinzi, miundombinu na mengine kama hayo toka serikalini. Ndiyo maana rais John Pombe Magufuli amekuwa akiwaambia watanzania kuwa miradi mikubwa mikubwa aliyofanikisha, imefanikishwa na watanzania wenyewe kupitia kodi zao. Hivyo, kwa mtu yoyote anayetaka maendeleo katika nchi yake, lazima alipe kodi bila kushurutishwa. Wamarekani wanao usemi kuwa vitu viwili haviepukiki kwa binadamu yaani kifo na kulipa kodi.
Chanzo: Nipashe Jumapili leo.

No comments: