The Chant of Savant

Sunday 6 September 2020

TUNATAKA KAMPENI ZA KISASA SI ZA KISASI

 

Mwaka huu ni msimu wa uchaguzi mkuu nchini. Bila shaka, watanzania, wanasiasa na wasio wanasiasa, wapiga na wapigiwa kura wako tayari kuushiriki kikamilifu kujipatia viongozi bora watakaowaletea maendeleo. Kabla ya kuzama kwenye mada ya leo, tuwakumbushe wasomaji wetu wa siku nyingi: tumerejea kwa kishindo baada ya miaka kama minne ya kutokuwa hewani. Pia si vibaya kutoa salamu za rambirambi kwa taifa na familia ya rais mstaafu Benjamin William Mkapa aliyetutoka ghafla hapo tarehe 23 Julai, 2020 na kuzikwa kijijini kwake Lupaso, Masasi, Mtwara tarehe 30 Julai, 2020. Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi, Amina.

            Tuingie kwenye mada yenyewe. Uchaguzi mkuu wa mwaka huu ni tofauti sana na chaguzi zote ambazo taifa letu limewahi kushiriki. Kwani:

 Kwanza, uchaguzi unafanyika wakati dunia ikiendelea kupambana na janga la gonjwa la Covid-19 ambalo limesababisha madhira makubwa kwa mataifa karibu yote duniani. Pili uchaguzi mkuu unafanyika kwenye kipindi ambacho Tanzania imeshangaza wengi kuweza kuwa nchi ya uchumi wa kati kabla ya muda uliokadiriwa ukiachia mbali wakati mugumu wa janga la Covid-19. Tuchukue fursa hii kuwapongeza watanzania wote kwa michango yao katika kufikia hatua hii adhimu na muhimu. Kwa upekee, tunaipongeza serikali ya awamu ya tano na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho ni chama tawala na ambacho sera zake zimetuwezesha kufikia hatua hii kwa umahiri wao katika kusimamia uchumi hasa kipindi hiki kigumu baada ya kusimamiwa vizuri.

            Pili, uchaguzi mkuu ni tukio kubwa na muhimu katika nchi ambapo wananchi hupata fursa––kila baada ya miaka mitano––kutumia na kufaidi haki yao ya kikatiba na kidemokrasia kuchagua viongozi wao watakaoongoza na kusimamia uendeshaji wa shughuli za kitaifa kwa miaka mitano ijayo. Hili si jambo dogo. Ni jambo linalohitaji maadalizi na utayari mkubwa kulishiriki na kulifanikisha kwa mustakabali wa taifa na watu wake. Wapo wanaosema kuwa kampeni haijaanza kisheria, wapo ambao wameishaanza kampeni kabla ya kampeni kuanza jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

            Yafuatayo ni mambo muhimu tunayopaswa kuzingatia kama wananchi na wadau wa demokrasia na uendeshaji wa mambo yetu kama jamii, taifa na watu. Hivyo, lazima tuzingatie yafuatayo:

            Mosi, kufanya kampeni na uchaguzi vya kistaarabu vitakavyohusisha sera na si matusi wala uzushi. Tunataka kampeni za kisasa na si za kisasi. Tunataka sera si shari. Tunajua; huu ni wakati wa kusema na kusikia mengi. Hata hivyo, mengi haya yatakayosemwa au kusikika yawe yana tija na si hadithi wala kelele za kupoteza fursa, muda na fedha za wananchi wanaogharimia zoezi hili adhimu na la bei mbaya kwa taifa. Hili ni muhimu; si kwa matokeo yanayokubalika na kukidhi haja bali kwa amani na usalama wa taifa. Kampeni za matusi na uzushi zipingwe na kupiga maarufuku kwa nguvu zote ili kulinda tunu za taifa tulizorithi kwa waanzilishi wake. Kujenga amani ni sawa na kujenga nyumba. Ni vigumu kujenga nyumba lakini rahisi kuibomoa. Gharama na muda wa kubomoa ni rahisi kuliko za kujenga.

            Pili, katika uchaguzi mkuu, kama taifa tujiepushe matumizi mabaya ya uhuru wetu wa maoni kwa kujiepusha na kutishia amani na usalama wa taifa. Hivyo, hakuna haja ya kutishana wala kuminyana. Tujipe nafasi ya kunadi sera zetu na si matusi wala uzushi. Hakika tukifanya hivi, tutakuwa tumejihakikishia uchaguzi bora na mfano kwa wengine. Kwani, ni wakti kama huu nchi nyingi huingia kwenye mtego wa maadui wa kuvuruga amani, utangamano na usalama wake bila kujua madhara yake. Tupingane kwa hoja na sera na si matusi na uzushi. Kwani, taifa litakuwapo baada ya––kama ambavyo limekuwa kabla ya uchaguzi mkuu. Uchaguzi na wagombea huja na kupita. Lakini taifa litakuwapo siku zote.

            Tatu, tuhakikishe haki inatendekea kwa wagombea wote. Wapewe nafasi sawa ya kunadi sera zao bila vikwazo wala vitisho ilmradi wote wazingatie sheria za uchaguzi na za nchi. Hivyo, katika kunadi sera zetu, hakuna haja ya kusingiziana, kuzushiana, kuchukiana wala kudanganyana. Isitoshe ni ukweli usiopingika kuwa tutampata rais, wabunge na madiwani watakaokubaliwa na wale wanaotaka wawakilishe katika serikali yake. Pia wapo, tena wengi, ambao watashindwa. Kwani maana halisi ya uchaguzi, licha ya kuwa zoezi la kidemokrasia na kistaarabu, ni mchujo ambapo wengi huitwa na wachache huchukuliwa. Hivyo, kushinda na kushindwa ni matokeo halali ya uchaguzi ilmradi yafikiwe kihalali na kisheria.

            Nne na mwisho, tujiepushe na vitendo vya rushwa na laghai na siasa rahisi rahisi za majitaka zenye kila dalili za takataka na uchakavu kulhali. Tufanye kampeni na siasa za uadilifu na uaminifu kwa ajili yetu na taifa letu kwa ujumla. Hapa lazima tuseme kuwa pande zote lazima kuwa makini kweli kweli katika matamshi na mipango yao. Wapiga kura nao lazima wapime sera, sifa na ahadi za wagombea wanaojitokeza mbele yao kuwashawishi. Maana wasipokuwa makini, watakuwa wamejitengenezea tatizo la miaka mitano ijayo. Hii ni kutokana na ukweli kuwa mfumo wa demokrasia hii ya kimagharibi unaelezea namna ya kuwachagua wagombea bila kutoa maelekezo ya namna ya kuwaachisha kabla ya kufikia ukomo wa kipindi chao cha miaka mitano. Watakaopokea rushwa ya wagombea wajue wanauza haki zao kwa miaka mitano ijayo ya maisha yao ambacho si kipindi kifupi kama maisha ya binadamu. Wanachotoa ni kikubwa kuliko wanachopata. Pia wagombea wajitenge na vitendo vya rushwa na ahadi za uongo, maana, mwisho wa siku, watateseka pia kutokana na ahadi zao mbovu. Kwani kufanya hivyo, licha ya kutukana na kutapeli demokrasia, wanawanyima wananchi fursa ya kuwa na viongozi wanaowafaa kwa miaka mitano ijayo. Kimsingi, demokrasia ya kweli hutaka wagombea kufanya ushawishi kwa wapiga kura wao kwa kutumia sera na hoja zenye mashiko na si uchochezi, visingizio na matushi wala uzushi. Hili tutaliongelea sana kwenye makala zijazo tutakapokuwa tukidurusu matamshi ya baadhi wagombea ambayo tutaona yanakiuka kanuni za mchezo na uhalisia wa mambo. Hivyo, watakaoongopa, kuzua, kucheza rafu wajiandae au kukiuka maadili kwa ujumla kujikuta hapa ugani wakianikwa bila huruma wala upendeleo.

            Kwa leo, tunaishia hapa. Tuonane wiki ijayo panapo majaaliwa.

Chanzo: Nipashe Jumapili leo.

No comments: