The Chant of Savant

Sunday 27 September 2020

Je watanzania watachagua kwa huruma au hekima?

Kabla ya kuzama kwenye mada, lazima niseme wazi. Natabiri kuwa watanzania watachagua sera na si sura; uzoefu na si uanagezi; uhalisia na si hekaya za Abunwas; ustaarabu na si matusi; ukweli, si uongo, uhalisia, si uchochezi na matendo na si nadharia.  Kwani urais si nafasi ya majaribio wala tambo bali serious business kwa kisambaa. Mnajua ninachomaanisha hata kama naongea kilevi. Kwa taarifa yenu, walevi wengi ni wasomi na watu wasio wanafiki. Ukimkosea mlevi, kabla hajawa mbwi, atakugwaya. Akishaweka vitu vyake, jiandae kufurumushiwa ukweli unaouma na kuchukisa kinoma. Hivyo, nisemayo leo, ni matokeo ya kanywaji. Waliozoea vitu vilivyotulia na kwenda shule, leo watanshangaa wakidhani sina akili nzuri wasijue mie ni bonge la daktari tena wa falsafa zote. KTY, hakuna watu wakatili kwenye kutovumilia ghilba kama walevi. Ukitaka kumdanganya mlevi, mnyime kanywaji. Ukitaka ukweliwengi wanaokuficha, mpe mlevi kanywaji.
        Nizame kwenye mada sasa. Yupo mzee mmoja mwalimu wa zamani wa chuo; amekuwa akijinadi kwenye mitandao kuwa ni mchambuzi wa masuala ya kibinadamu na kijamii. Mzee huyu ambaye sitamtaja ili nisimpe ujiko wa bure, amekuwa akisema kuwa uchaguzi huu unaweza kuwa wa aina yake kwa vile wapiga kura watapiga kura kwa huruma badala ya hekima. Nakubaliana naye kuwa uchaguzi huu ni wa aina yake kwa vile umejaa wabangaizaji hata wachochezi wanaojua kuwa watapoteza lakini watapata kiki. 
        Pili, mchambuzi huyu anayetumia uchambuzi kuficha mafungamano na ukereketwa wake wa kisiasa, anatia shaka.  Mfano, anatumia uzoefu wa Nelson Mandela, rais wa kwanza mzalendo wa Bondeni alivyochaguliwa kwa vile alikuwa amefungwa na serikali ya kikaburu kwa jumla ya miaka 27. Anashindwa kuelewa kuwa serikali ya kikaburu ilikuwa haramu tofauti na serikali iliyomaliza muda wake. Anashindwa kuelewa kuwa mateso yatokanayo na kupigania umma ni tofauti na yale yatokanayo na kupigania haki binafsi. Mandela alipigania uhuru. Je hawa jamaa zake wenye ugonjwa uitwao Ukosefu wa Sera, Adabu, Heshima na Adili (USAHA) anasahau kuwa siasa za Afrika Kusini na za kipindi kile ni tofauti na za sasa za Bongo ambapo lazima utumia bongo na si bango, sera na si sura, matokeo halisi na si matarajio.
        Tatu, kwa kuzingatia kile watanzania karibu wote wanahitaji–––wakiwamo hata hawa wanaopiga kelele na kukufuru–––sina shaka. Watachagua rais wao; si kwa kusikiliza ngonjera na vilio bali ukweli mtupu utokanao na mambo yanayoweza kutolewa ushahidi na si vinginevyo. Wataangalia utendaji wenye mashiko na si kudandia mambo yasiyoingia hata kwenye kichwa kidogo cha kuku. Katika yote, maendeleo yatachukua kiti cha mbele kwenye vipaumbele ambayo watanzania wanavyo. Afya, amani, barabara, elimu, miundombinu, nishati, na usalama vitakuwa ni tunu wanazotaka anayetaka kuwaongoza awe na uwezo wa kuwahakikishia ima kutokana dira na ilani yake au mambo ambayo ameishayafanya. Hawatakubali kugeuzwa mabunga wala sehemu ya siasa za majaribio. Huu ni ukweli ambao unaweza kuuapia hata bila kupata kanywaji. We are now going practical as opposed to theoretical. Kwa wasiojua kisukuma, nisameheni. Sina haja ya kutafsiri. Kwa kimakonde ni kwamba sasa tunaangalia vitendo na si ngonjera na mashairi. Kwa kijita ni chikerebe, cha kwa akina Pius Msekwa, ni kwamba kapira bwacha sugu si salamu bali kanuni ya sayansi.
        Amini usiamini. Watanzania wa sasa si wa jana. Wanataka mambo yanayowekana na si hadithi za Paukwa Pakawa. Siasa siyo hadithi ya mapenzi. Ni uwanja ya maslahi tena mapana na mengi. Ukitekeleza nilichokutuma na ulichoahidi, nani akuondoe? waliokuwa wakitaka maji wakayapata watamchagua aliyewezesha; kadhalika kwa barabara, umeme na mengine. Waliochukia ufisadi watachagua aliyeuangamiza; ukwepaji kodi na wizi wa raslimali zao watachagua aliyekomesha kadhia hii. Je huyu ni nani? Si kazi yangu kutamka. Msiseme amenihonga kanywaji. Mwenye macho haambiwi tazama; mwenye masikio sikia. Kila kitu kiko wazi kama usiku na mchana. Nani ni usiku na nani mchana? Usiku ni kiza kitupu. Hujui wala kuona uelekeako zaidi ya kelele za wadudu na vyura. Mchana, kila kitu kiko wazi. Hata ukifumba macho utaona tu.
        Ikifika siku ya uchaguzi, chagua uwezekano na si matarajio na ahadi za urongo zisizo na rekodi yoyote ya utendaji. Chagua maendeleo na si maneno matupu. Kwani maneno matupu yanaliwa? Narudia. Mwenye mato haambwi tazama; na mwenye maninga haambwi tazama. See you.
        Tumalize, japo ni haki kuwa mawazo na ushawishi wake, mhusika katika kutetea chama chake, kwa wanaojua maana ya kufaa katika kutumikia watu, wapiga kura huangalia mambo mengi na si kumuonea huruma mgombea ima kwa vile alifungwa au alinusurika kuliwa na simba au kufa ajalini na mambo mengine kama haya. Wapiga kura si mama au baba huruma.
Chanzo: Nipashe Jumapili leo.


2 comments:

Unknown said...

Mwandishi ana ladha ua ukibaraka na khofu ya mabwana. Ogopa sana waandishi dizaini hii. Wako tayari kuona wananchi wanakufa au wanauliwa lakini wao mitumbo inavimba. Kitu ethic wao hawakijui

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Usemayo ni kweli. Hasa ikizingatiwa kuwa ni maoni yako. Fichua jina tukujue. Hakuna ukibaraka hapo. Upinzani ndiyo vibaraka ulioshindwa kutuletea mgombea mmoja. Kwa mambo ambayo CCM chini ya Magufuli imefanya, kwa sasa tukubali ukweli. Hakuna wa kumshinda Magufuli. Hapa hakuna cha kuhongwa. Ni bahati mbaya kuwa wewe na wenye mawazo na agenda kama zako hamtaki kuuona na kuukubali ukweli. Ngojeni matokeo yatawaamsha toka kwenye ndoto za mchana. Kama hili limewachoma, nadhani mwaka huu mtakata roho. Maana huu ndo mwanzo tu.