How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Saturday, 17 October 2020

BARUA KWA MWALIMU NYERERE



Baba wa taifa Mwl Julius K Nyerere (RIP).
Shikamoo baba. Ni miaka 21 ya machungu na upweke, kama watu na taifa, tangu ututoke. Japo ulitutoka kimwili,kiroho na kiakili bado tuko nawe kama ambavyo tutakuwa nawe hadi tutakapokutana huko uliko. Katika maadhimisho ya kuondoka kwako baba, leo nina machache ya kukueleza kama ifuatavyo kwa ufupi tokana na mhariri kutonipa nafasi ya kutanua sana:
        Mosi, tangu uondoke, taifa letu limebadilika sana. Nakumbuka wakati ukitutoka, ulimuacha kijana wako, ambaye naye amekufuata ghafla mwaka huu, Benjamin. W. Mkapa. Baada yake, alikuja kijana mwingine Jakaya Kikwete ambaye sasa ni mzee na mstaafu pamoja na mrithi wako mzee Ali .H. Mwinyi ambaye bado anadunda. Muhimu, baada ya Kikwete kuondoka, alichaguliwa kijana mwingine machachari aitwaye John Pombe Magufuli. Kijana huyu, amefanya maajabu hasa kutekeleza yale ambayo ulitaka yatekelezwe. Je unaweza kuamini kuwa makao makuu ya chama na nchi yalishahamia Dodoma huku Dar es Salaam ikirembeshwa utadhani Ulaya. Wale waliokuwa wakililia kwenda kuona maajabu ulaya sasa wanakwenda Dar.
            Pili, kama haitoshi, lile shirika la ndege uliloanzisha mafisi, mafisadi na wezi wakalifilisi sasa linadunda. Mwaka jana Magufuli alinunua ndege 11 mpya na nane kati ya hizo zimo zinapaa nje na ndani ya nchi. Bila kungoja, kwa sasa kuna meli kibao zinatengenezwa hadi moja kubwa ya kwenda Comoro. Cha mno, ule mradi mkubwa wa umeme wa mto Rufiji sasa umo mbioni kujengwa. Kwa heshima na kumbukizi lako, umepewa jina lako sambaba na daraja la kuunganisha Feri na Kigamboni.Mambo ya kukatika  na migao ya umeme sasa historia. Kama haitoshi, je wajua kuwa kwa sasa tupo tunajenga reli mpya ya kisasa ya kutumia umeme ya SGR toka Dar hadi Kigali? Reli za zamani, viwanja vya ndege na madaraja vikikarabitiwa ukiachia mbali ujenzi wa barabara kibao nchini. Siku hizi, kwa mfano, kwenda Kusini kuliko kuwa kumeshindikana ni kama unalia.
            Mwalimu, kabla ya kusahau, rafiki yako Nelson Mandela alishaondoka kadhalika Robert Mugabe pia huku mama Maria akiendelea kudunda japo umri unasogea. Kwa upande wa watoto wako, bado wanaishi maisha ya kawaida saw ana sisi wengine.
            Tatu, mwalimu unaweza kuamini kuwa ule wizi ma mali zetu chini ya ujambazi uitwao uwekezaji umeishakomeshwa? Madini yaliyokuwa yakitoroshwa usiku na mchana sasa yananufaisha taifa kiasi cha kujenga miradi hiyo tajwa bila kukopa kopa, kuomba omba wala kujidhalilisha kama ilivyo kwa mataifa mengi ya Kiswahili. Kule Mererani yanakopatikana madini ya tanzanite sasa hali ni shwari baada ya eneo lote la machimbo kuzungushiwa ukuta huku makampuni nyonyaji ya kigeni yachimbayo madini yakiingia mikataba upya. Kabla sijasahau, siku hizi mashirika na makampuni yanalipa mrahaba wa serikali kama hayana akili nzuri.
            Nne, mwalimu unajua kuwa lugha ya Kiswahili sasa imekuzwa kiasi cha mataifa ya nje kuanza kuitumia na kuionea fahari. Kwa taarifa yako, sasa Kiswahili kinatumika kwenye SADC na Umoja wa Afrika.
            Nne, kama ilivyokuwa wakati wa utawala wako adhimu, kwa sasa, afya na elimu hutolewa bure kwa watanzania wote bila kubagua chama wala dini. Kama haitoshi, ukusanyaji kodi umeongezeka kiasi cha taifa kuwa na fedha yake ya kutekeleza miradi mikubwa kama nilivyokutajia hapo juu na kutoa huduma za kijamii bure ukiachia mbali kujenga hospitali, zahanati na kukarabati miundo mbinu ya zamani.
            Tano, wale waliozoea kughushi au kuajiri watumishi na wanafunzi hewa walishafyekwa zamani. Kijana Magufuli amebana matumizi hadi wasioelewa somo kulia kuwa vyuma vimebana. Ule wakati wa mchovu kulala maskini na kuamka tajiri ushapita zamani. Kila mtu anakula jasho lake na kuheshimu jasho la wenzake. Wale waliozoea kuibia umma sasa wanalia na ni apeche alolo yaani hawana majivuno ya ukwasi kama zama zile za kiza.
            Sita, cha mno, chama chako kipenzi cha Mapinduzi kilichokuwa kimeanza kugeuka chama cha ulaji sasa kimenyooshwa kweli kweli. Mali zake zimerejeshwa mikononi mwa chama na kinaendelea kukua na kuadilika hakuna mfano. Mambo ya kugombea na kushinda kutegemea mfuko wa mtu yalishafyekwa na kugeuka historia chafu ya chama. Siku hizi mtu anayetaka kupeperusha bendera yake anachujwa kwa kuangalia uadilifu na utendaji wake wa kazi bila kusahau uzalendo. Kwa upande wa upinzani, bado upo japo kwa kiasi Fulani unasuasua.  Kabla ya kusahau, watanzania wameongezeka kiasi cha kufikia milioni 50 na ushei huku Muungano ukizidi kuimarika na kulindwa kwa nguvu zote. Je wajua kuwa hivi karibu mtoto wa Mwinyi ameteuliwa kugombea urais Visiwani?
            Mwalimu, barua hii haitaleta maana kama itaisha bila kukufahamisha kuwa Tanzania sasa ni imara kijamii, kisiasa na kiuchumi kuliko wakati wote wa uhai wake. Misingi uliyoweka sasa inatumika kujenga uchumi hadi kuingia uchumi wa kati mwaka huu miaka mitano kabla ya wakati uliokuwa umekadiriwa. Watu wanachapa kazi kama hawana akili nzuri na kauli mbiu ya sasa ni HAPA KAZI TU. Na ni kweli. Ni kazi kweli kweli.
Mwalimu, naomba nisikuchoshe. Kwa leo, ni hayo tu japo yapo mengi ya kufurahisha. Pumzika mahali pema peponi Mwalimu.
Chanzo: Nipashe Jumapili leo.

No comments: