The Chant of Savant

Sunday 4 October 2020

Hawa Nao Kweli Waheshimiwa?


Huwa napata utata na wakati mwingine kinyaa itajwapo heshima sijui cheo cha mheshimiwa! Hushangaa sana hasa nionapo baadhi ya wanaoitwa waheshimiwa. Wengine hawana wala hawastahili heshima. Wananuka ubabaishaji, ufisadi, urongo na uzushi. Ni mafisadi na mafisi hadi kwenye mifupa. Mfano, wanaotembeza uongo mchana wakati huu wa kusikia mengi wanaoendelea kuitwa waheshimiwa. Hivi kweli hawa ni waheshimiwa? Wana heshima gani iwapo wanatenda mambo ya aibu wazi? Wanaotetea wezi wa raslimali zetu nao eti ni waheshimiwa!Makuwadi wa uchukuaji wanaoita uwekezaji au vibaraka wa mabeberu ambao rais John Magufuli amekuwa akimbana nao, kweli nao ni waheshimiwa? Wapo wengi wake kwa waume. Ukiwaona wana sura za binadamu. Lakini ndani ni mafisi watupu.

Je sisi tunaowaita hawa waishiwa waheshimiwa–––wakati tunajua ni majizi–––tunastahiki heshima kweli? Je heshima ni maneno au matendo? Sheria wanasema: mhalifu ni yule aliyetenda kosa la jinai au aliyeshuhudia asiripoti au aliyeshirikiana na aliyelitenda; ni yoyote anayeshiriki kutenda kosa la jinai ima kwa kujua au kutojua hadi atakapobainika vinginevyo. Je hawa wanaotafuta madaraka kwa rafu ni waheshimiwa kweli?  Hebu angalia yafuatayo:

Kwanza, kwa maneno na matendo yao, hawastahili heshima; unapomdharau mtu usitegemee akuheshimu wala ukimdanganya mtu usitegemee akutetee.

Pili, ukiangalia historia zao za utendaji na mazingira hata sera na nia zao, hutahofia wala kusita kuwaita wabangaizaji na wasaka tonge tena wa kukodiwa au kununuliwa. Tunao wengi. Wapo majukwaani, vyamani na kwingineko. Tunao kwa mamia hawa. Wengine wanatafuta madaraka kujitajirisha huku umma ukiendelea kusota. Ukiwaona utawajua. Hupenda kujisifu na kulaumu tu bila kutoa mbadala. Sasa mnawajua; msiseme hatukuonya Ibilisi wa mtu ni mtu.  Aweza kuwa wewe hata mimi. Aweza kuwa mtukufu hata tajiri na msomi. Ibilisi ni ibilisi hata aitwe mchungaji, mheshimiwa, kizito na mfadhili na makando kando mengine mengi.

Tatu, anayetetea ujinga utakaoweza kfuanya watanzania kulanguliwa umeme siyo jizi tena kubwa lao? Na huyu aliyesababisha madini yetu kuwaneemesha wawekezaji ilhali sisi tunazidi kuwa maskini si wa kuogopwa kama ukoma? Vipi kuhusiana na mtu asiye na sera za kutukomboa bali kututumia badala ya kututumikia; anayetaka kuwe watwana naye bwana? Hebu fikiria juu ya mtu anayetoa toa ahadi asitekeleze hata moja. Waswahili husema: Haja ya mja kunena, muungwana vitendo. Je asiyetimiza hili si muongo tu hata akiitwa mheshimiwa? 

Nne, mfikirie anayewadanganya watu. Anasema hili leo kesho lile. Je huyu anayostahiki hata chembe kuitwa mheshimiwa? Mbona uheshimiwa umevamiwa kiasi cha kuwa uishiwa? Mbona uheshimiwa umekosa thamani kiasi cha kutumiwa na wazushi hata wambea?

Tano, kuna watu na heshima zao. Lakini pia wapo wengi waitwao waheshimiwa wasiostahili hata nusu ya heshima. Wapo wenye silka, hulka na tabia za wanyama waitwao waheshimiwa. Kuna watu wanapaswa kuwa gerezani si bungeni wala uraiani. Chukulia, mpotoshaji wa wazi wazi akilenga kuchonganisha watu ili waanzishe vurugu. Hebu fikiria mtu anayewaganywa watu ili awatawale kama yule mshenzi wa kiingereza aitwaye Lugard alivyotufanyia. Fikiri jitu au mijitu inayoeneza chuki za kidini na kikabila. 

Sita firiki zaidi. Hebu jielekeze kwa mtu anayesimama kwenye viwanja kama vile vya Jangwani akatangaza kutenda miujiza iwe ya kisiasa au ya kidini wakati hana lolote bali janja ya kuwaibia wajinga wengi. Je hawa hawapo? Siku moja tulikuwa tunajadili ni kwanini nchi za kiafrika haziendelei ilhali zimekuwa na serikali kwa zaidi ya miaka 50. Tuligundua mdudu mmoja mbaya sana akiziangamiza nchi hizi. Anaitwa ulafu na ubabaishaji na kutegemea miujiza badala ya kuchapa kazi.

Tembelea Afrika kuanzia Kaskazi hadi Kusi, Mashariki na Magharibi. Utakuta watu wanaojifanya wanawapenda watawaliwa waliwa. Watajionyesha kama wapenda maendeleo wakati ni vikwazo vya hayo maendeleo ndoto. Wanaishi maisha ya kifalme wakizungukwa na makapuku wa kunuka. Wao na familia zao, kupitia ujambazi fichi wa kimfumo hawana tofauti na kupe. Wanawanyonya watu maskini kwa kisingizio cha upuuzi uitwao kuchaguliwa!

Wanaficha mabilioni ya fedha Ulaya. Wanachekiwa afya zao na kutibiwa Ulaya. Leo akitokea rais asiyeruhusu uhuni huu anaambwa anaogopa kwenda nje! Kwani kuzurura ni kazi yar ais? Wameua hospitali, zahanati, shule, mashamba, viwanda na kila aina ya mradi. Halafu akitokea mtu akavifufua wanampa kila aina ya majina. Bado majizi hawa wanawahadaa watu wanaweza kuwaletea maendeleo. Kwao watu ni familia na marafiki zao. Wameishiwa kiasi cha kushindwa hata kujitambua. Bahati mbaya na watawaliwa nao wameendelea kuuziwa mbuzi kwenye gunia kana kwamba hawana akili wala macho!

Hata nifungwe au kupigwa mijeledi, sitawaheshimu waheshimwa majambazi waliotamalaki kwenye nchi za kiafrika. Sitaacha kuwaambia kuwa ni majizi na waishiwa.

Kuna haja ya kungalia kwa makini demokrasia yetu inayoanza kugeuka ghasia. Kuna kila sababu ya wasomaji na wananchi kwa ujumla kuanza kutafuta jibu la kejeli na matusi haya kuhusiana na demokrasia na dhana ya uheshimiwa wa wasiostahiki heshima wala kuwa nayo ambayo husakwa kupitia uchaguzi. Mheshimiwa au mwizimiwa?

Leo sisemi sana.

Chanzo: Nipashe Jumamosi leo.


No comments: