The Chant of Savant

Tuesday 27 April 2021

Kodi ya Uzalendo Ianze Sasa kwa Wabunge Wetu

Kwenye kikao cha bunge kinachoendelea, Mbunge wa Ilala, mheshimiwa Musa Azzan Zungu (CCM) alitoa wazo zuri la namna ya kukuza wigo wa kodi kwa ajili ya mapato ya taifa. Alipendekeza kuanzishwa kwa kodi ya uzalendo ambapo kila mtumia simu anapaswa kutozwa angalau shilingi mia. Hili wazo, kama nilivyosema hapo juu ni zuri. Ila katika utekelezaji wake tunapaswa kuwabana wale wanaopata fedha nyingi kama mishahara au marupurupu. Hivyo, kuanzia, tuanzie na wabunge ambao mishahara na marupurupu yao ni makubwa ukiachia mbali kutokatwa kodi. Kama tutalenga kweli kupanua wigo wa mapato, basi waheshimiwa wabunge wakatwe kodi kwenye mishahara na marupurupu yao ambavyo ni vikubwa ikilinganishwa na wale wanaosema wanawawakilisha.
Natoa pendekezo hili la kuanza na wabunge kutokana na sababu zifuatazo:
Kwanza, wanapata mishahara mikubwa na marupurupu makubwa ikilinganishwa na wananchi wa kawaida wanaowawakilisha. Kwanini wawakilishwa wakatwe kodi lakini watumishi wao ambao ni wabunge wasikatwe kodi?
        Pili, wabunge––––ambao ni kioo cha jamii kama viongozi na wawakilisha wa umma kama kweli wanauwakilisha na siyo kujiwakilisha–––wanapaswa kuonyesha mfano mzuri wa kuchangia kupanua wigo wa mapato kwa taifa lao kwa ajili ya maendeleo na ufanisi wa waajiri wao na taifa kwa ujumla.
        Tatu, wabunge wetu ni wengi kuliko idadi inayohitajika kulingana na uwezo wetu wa kiuchumi kama taifa. Kimsingi, majimbo yetu mengi yameanzishwa kisiasa na si kiuchumi wala kiuhalisia. Hata baadhi ya mikoa nayo kadhalika imeanzishwa kisiasa hasa tukizingatia kuwa tokana na kuwa na miundo mbinu mizuri kwa sasa, tuna haja ya kuipunguza.  Hivyo, sehemu nyingine ya kupanua wigo wa mapato ya serikali ni kubana matumizi ambapo mojawapo ya njia inanaweza kuwa kupunguza majimbo ya uchaguzi. Mfano, ukiangalia wabunge watokao visiwani na idadi ya watu wanaowakilisha, unashangaa mantiki ya jumla ya kufanya hivi. Katiba ya Tanzania inatamka wazi kuwa watanzania wote ni sawa. Je ni usawa gani iwapo wabunge mfano, toka Visiwani wanawakilisha idadi ndogo ya wapiga kura na wananchi wakati watokao Bara wanawakilisha idadi kubwa? Lazima tukiri. Hapa kuna tatizo la kimfumo ambalo lisiposhughulikiwa, linaweza kuleta malalamiko baadaye.
        Nne, kama ilivyodokezwa hapo juu, mishahara na marupurupu ya wabunge ni makubwa. Kwanini wananchi wenye mishahara kiduchu–––tena ambayo haijapandishwa kwa miaka mingi–––wakatwe kodi lakini wabunge wasikatwe kodi wala kuwa na mishahara inayolinga au kufanana au kukaribia na ile ya wale wanaowawakilisha? Kazi ya serikali siyo kuhudumiwa wanasiasa huku ikiwaminya wananchi wa kawaida.
        Ukiachia mbali na kuwakata kodi wabunge–––na hata ikiwezekana kupunguza marupurupu yao na hata majimbo–––kuna haja ya kubana matumizi kwa kupunguza nafasi za kisiasa zisizo na ulazima zaidi ya kuwapo kwa sababu za kisiasa kama utititiri wa majimbo. Kwa kumbukumbu ni kwamba Hayati John Pombe Magufuli alipunguza mshahara wake na ile ya wakurugenzi waliokuwa wakipata mishahara mikubwa kuliko hata rais na mawaziri ili kuleta uwiano wa kipato na usawa. Je kwanini mantiki haya yasitumike hata kwa wabunge ambao kimsingi, ni matajiri ikilinganishwa na wananchi wa kawaida wanaodai kuwawakilisha. Ukitaka kujua kuwa ubunge ni sehemu ya kutajirikia, angalia namna watu wanavyoacha hata taaluma zao na kujiunga na siasa ili kupata hii fedha na kutajirika haraka. Watu wako tayari kutoa hata rushwa ili waupate ubunge kwa vile unalipa sana. Wengine wanaacha hata makanisa yao ili kwenda kuchuma fedha hii kubwa inayowafanya si wawe matajiri tu bali hata wawe na ushawishi katika jamii. Hivyo, njia mojawapo inayoweza kuongeza mapato ya serikali ni ku-decolonise ubunge na nafasi nyingine za kisiasa ambazo zinatoa mishahara mikubwa isiyolingana uhalisia wa taifa kiuchumi.
Suala jingine ni kuachana na mfumo wa kikoloni ambapo uchumi ulitumikia siasa badala ya siasa kutumikia uchumi. Tangu tupate uhuru, tulishindwa kuliona hili. Tulisahau kuwa wakoloni walikuwa wakipeana mishahara mikubwa kama njia ya kutudhoofisha ili waendelee kutunyonya na kutusikinisha ili tuwategemee kama ilivyo sasa. Sioni mantiki ya mbunge ambaye, kimsingi, hana ulazima wala hatoi huduma inayohitajika sana kuwa na mshahara mkubwa kuliko daktari au profesa. Ubunge hausomewi wala hauna ulazima wa kujieleza mambo yanapokwenda mrama sawa na watumishi wa umma na wana taaluma. Tokana na ubovu huu wa kimfumo, hata vijana wetu siku hizi hawana motisha wa kusoma. Badala yake wanaona usanii, siasa, uhubiri na mambo kama hayo ni muhimu kwa vile vinawaingizia fedha kuliko usomi.
Eneo jingine linaloweza kutozwa kodi kubwa ni masuala yote ya starehe. Kwa mfano, mabaa, kumbi za muziki, wanamuziki na wasanii kwa ujumla, wanapaswa kutozwa kodi ya kutosha kwa vile huduma zao ni za upili na siyo za kwanza kwa maisha ya binadamu. Ili nisionekane nawakandamiza baadhi ya watu wetu, inakuwaje, mfano, mwanamuziki awe na fedha nyingi kuliko daktari au mtunzi wa vitabu ya kiada kama siyo mfumo mbovu wa kuangalia nini tunataka kama binadamu na taifa? Katika hali ile ile, inakuwaje mazao ya mkulima yawe na bei ya chini kuliko hata muziki ambao hauliwi wala kuhitajika sawa na chakula? Jibu ni ni wazi kuwa tulirithi mfumo wa kijambazi na kikoloni ambapo watu wachache wananeemeka kwa mgongo wa maskini walio wengi. Kimsingi, mfumo huu hauna tofauti na mfumo wa sasa ambapo mtu anaamka asubuhi na kuanzisha kanisa lake na kuanza kuwanyonya maskini na wajinga waliokata tamaa na kulala tajiri bila hata kutozwa kodi huku serikali ikiangalia na kulalamika haina vyanzo vya kupanulia wigo wa kodi kwa ajili ya mapato ya serikali. Hii ndiyo siri ya utitiri wa makanisa kila sehemu kwa vile ni biashara inayoingiza fedha nyingi bila kukatwa kodi sawa na siasa.
            Japo binadamu anahitaji huduma za kiroho na kisiasa, si kwa ulazima sawa na huduma kama afya, elimu, chakula, mavazi, maji na hata uzoaji taka mijini ambavyo umuhimu wake ni wa kwanza na wajuu kuliko miziki, maigizo, nyimbo, mpira, siasa, dini na mengine kama hayo.
        Naomba niwasilishe kwa kutoa mchango wangu wa namna ya kupanua wigo wa mapato kwa kuangalia mambo ambayo hatukuyaona au kuyarekebisha kama tulivyoachiwa na wakoloni nasi tukayashikilia na kuyaendeleza hata baada ya kupata uhuru. Mfano mdogo, hapa Kanada, mambo yasiyo ya ulazima wa kwanza katika maisha ya binadamu yanatozwa kodi ya juu kiasi cha kutisha ili kupata fedha ya kugharimia huduma za msingi na siyo za upili. Mfano, wabunge hapa wanajiendesha. Hakuna serikali kuwalipia fedha za madereva, wasaidizi na mengine kama hayo. Hivi tukiondoa madereva wa wakuu wa idara, mawaziri, wabunge, makatibu wakuu wa wizara, makatibu wakuu wasaidizi, manaibu wa mawaziri, wakuu wa wilaya na mikoa, wakurugenzi wa kada mbali mbali na wengine wengi wanaoweza kujiendeshea magari yao tutaokoa mabilioni mangapi? Je hao  madereva na wasaidizi wengine wadogo wanahitajika? Hakuna haja ya kulalamika wala kuwabana walalahoi bure. Hivi ni vyanzo vikubwa na vizuri vya mapato. Basi waheshimiwa wabunge waonyeshe mfano kwa kuanza kubana matumizi yao na kutozwa kodi ili umma ufuatie.
Chanzo: Raia Mwema kesho.


No comments: