The Chant of Savant

Tuesday 6 April 2021

RAIS SSH ANAWEZA KUWA RAIS BAADA YA 2025 AKIWASOMA AKINA BANDA


Japo siasa za mataifa jirani ya Malawi na  Zambia ni tofauti na za Tanzania, zina somo kwa Tanzania. Kwa wanaokumbuka namna mwanamama Joyce Banda alivyokuwa rais wa Malawi (7 Aprili, 2012 – 31 Mei, 2014) baada ya kufa kwa rais Bingu wa Mutharika au Rupiah (19 Agosti, 2008 – 23 Septemba, 2011) baada baada ya kufa kwa Levy Mwanawasa, watakubaliana nasi kuwa–––kama wangekuwa amejiandaa–––wangeweza kuendelea kuwa marais hata baada ya kumaliza kipindi cha watangulizi wao. Hata hivyo, hawakufanikiwa kuwa marais japo waliutaka urais. Kuna mambo mengi yalichangia kushindwa kuendelea na urais. Mosi, walishindwa kwenye uchaguzi uliofanyika baada ya kumaliza ngwe ya mtangulizi wake.
Pili, uongozi wao hakuwaridhisha wamalawi na wazambia tokana na sababu mbali mbali nyingi zikitokana na ufisadi na namna walivyotumia madaraka yao. Tutaanza na Joyce Banda ambaye alishindwa urais tokana na kuhujumiwa na kambi ya mdogo wa marehemu Mutharika, Peter Mutharika aliyemshinda na kuwa rais miaka michache tu baada ya kaka yake. Ndiyo maana, tumesema kuwa siasa za Malawi na Tanzania ni tofauti. 
Mbali na kuhujumiwa au kuzuiwa na kambi ya Mutharika, Banda alikabiliwa na kashfa ya wizi wa mabilioni ya shilingi ya fedha za umma kwenye kashfa iliyojulikana kama cashgate ambapo ilidaiwa kuwa aliuza ndege ya rais baada ya kuishusha thamani yake kwa kiasi cha dola za kimarekani milioni15 ambapo  milioni 1.5 zilikwenda kwenye ununuzi wa mahindi huku zilizobaki zikiyeyuka bila kubakiza unyayo. Kwa taifa maskini kama Malawi fedha hii si ndogo hata kidogo. Hivyo, tunaweza kusema kuwa ubadhirifu na kushindwa kusimamia fedha ya umma kulimkosesha Banda urais mbali na kuhujumiwa na makundi yaliyomuunga mkono Mutharika. Baada ya kushindwa kwenye uchaguzi, Banda alikwenda ukimbizini kuepuka kukamatwa kwa miaka minne tangu 2014 hadi 2018. Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Uingereza (BBC, 27 January, 2014), chini ya utawala wa Banda, Malawi ilipoteza yapata dola milioni 250 tokana na malipo huduma hewa.
Kwa upande wa Rupiah Banda aliyeshindwa na Michael Sata, hakuna sababu kubwa iliyofanya ashindwe kama kutuhumiwa kuibia taifa $11 milioni ndani ya kipindi cha miaka mitatu aliyoongoza Zambia. Kashfa hii ilitokana na Banda kununua mafuta toka Nigeria ambapo hata mwanae Henry, mfanyabiashara mwenye makazi yake nchini Afrika Kusini naye alituhumiwa kuhusika na kashfa hii ya ununuzi wa mafuta toka Nigeria iliyomlazimisha kuishi ugenini kuepuka kukamatwa. Mwaka 2013, Banda alikamatwa kuhusiana na kashfa hii ya mafuta iliyolenga kunufaisha familia yake. Mbali na kashfa hii, Rupiah alikabiliwa na mashtaka ya matumizi mabaya ya madaraka jambo ambalo alilikanusha.
Hivyo, basi, somo la kwanza kwa rais SSH toka kwa marais Banda ni kupambana na ufisadi vilivyo na kusimamia fedha na mali za umma vizuri ili kukubalika kwa wapiga kura na wananchi kwa ujumla. Somo la pili ni kuepusha familia kujiingiza kwenye utawala wake ili kuepuka vishawishi. Kwani, wanafamilia hawawezi kujua dhamana, maana na ukubwa wa mzigo alio nao rais wan chi. Hivyo, wanaweza kujiingiza kwenye ufisadi kwa mgongo wa ndugu yao wasijue hatari wanayomsababishia na taifa kwa ujumla kama inavyoonekana kwenye kesi hizo mbili juu zinazowahusisha akina Banda ambao waliukosa urais tokana na kutokuwa makini na wadhifa huu.
Somo la tatu ni kwamba hata mhusika asipojihusisha binafsi kwenye ufisadi, anapaswa kuwaangalia walio chini yake. Kwa mfano, pamoja na mashtaka dhidi yake binafsi, Joyce Banda anatuhumiwa kuzembea kuwabana wa chini yake kiasi cha kusababisha hasara ya dola za kimarekani milioni 15-¬––250 kwa nchi yake; jambo ambalo liliwakasirisha sana wapiga kura na wamalawi kwa ujumla na kumtupa nje ya uringo wa kisiasa hadi akakimbia nchi yake kwa muda wa miaka minne. Ili kuweza kunusurika na kifungo, Banda alijiunga na upinzani wenye nguvu chini ya rais wa sasa Lazarus Chakwera. Hivyo, kunusurika tokana na kitendo hiki.
Somo la nne ni kwamba wananchi wanaona kila kinachofanyika. Hivyo, wanapopata nafasi ya kutoa hukumu, wanafanya hivyo kwa ukali sana kama ilivyotokea kwa marais wawili tajwa. Hivyo, rais SSH ana darasa zuri toka kwa maisha ya marais tajwa ambao waliutaka urais baada ya kumaliza kipindi cha mpito lakini wakaukosa. 
Kwa ufupi ni kwamba wahusika walikwamishwa na ufisadi na usimamizi mbaya wa fedha na mali za umma na matumizi mabaya ya madaraka yao. Hilo ndilo somo la msingi katika yote. Kama tulivyosema hapo juu, siasa za Malawi na Zambia ni tofauti na za Tanzania tokana na nchi hizi kuwa na upinzani makini na ulioshikamana. Hata hivyo, hili lisitudanganye kuwa hali ya kisiasa nchini haiwezi kubadilika. Upinzani unaweza kuimarika, kuungana na kufanya maajabu tokana na hali itakavyokuwa baada ya rais SSH kuonyesha staili yake ya utawala. Kama atayaelewa na kuyatia maanani masomo tajwa hapo juu, hana haja ya kuogopa chochote bali kujimbia ofisini na kuweza kugombea na kushinda–––jambo ambalo tunajua ana uwezo wa kufanya bila wasi wasi wala upungufu wowote. Isitoshe, mtaji aliorithi ni mkubwa kiasi cha kumwezesha kufanikiwa haraka na kirahisi. Kwa mtaji wa uchakazi na uwezeshaji ulioachwa na hayati Dk John Magufuli, SSH ana kila sababu ya kuwa mojawapo ya vigogo wa siasa nchini kama ataweza kushinda uchaguzi ujao. Hata hivyo, mwanzo wake unaanza kuonyesha hili hata kabla ya visa tajwa ambavyo naamini anavijua. Tunachofanya ni kumkumbushia tu.
Chanzo: Raia Mwema kesho.

No comments: