The Chant of Savant

Wednesday 14 April 2021

HONGERA RAIS SAMIA, MPANGO CHAGUO LA NGUVU

Baada ya kuapishwa na kukalia kiti cha urais, macho ya watanzania walio wengi yalikuwa kwa mheshimiwa rais Samia Suluhu Hassan (SSH). Wengi walitaka kujua nani angemteua kuwa msaidizi wake mkuu yaani makamu wa rais kama alivyokuwa yeye kwa hayati John Magufuli aliyetuondoka hivi karibuni na Mungu ailaze Mahali Pema Peponi. Katika mitandao, majina mengi yalirushwa huku wengine wakitumia fursa hii kupenyeza watu wao wawanadi kama wanaofaa kuteuliwa. Kama ada, Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho kinasifika kwa kuteua wale usiowadhania, kimeendeleza ugwiji wake katika hili. Kwani, pamoja na majina mengi kurushwa kwenye mitandao na vijiwe, lilikuja jina ambalo wala halikutajwa hata mara moja. Nalo ni la Daktari Philip Isidor Mpango, makamu mteule wa rais aliyeteuliwa na SSH hivi karibuni, akiwaacha wengi midomo wazi. 
Pamoja na kwamba Mpango hakutajwa tajwa, ana sifa nyingi. Anafaa kuwa makamu wa rais. Tutagusia sifa chache katika nyingi alizo nazo mheshimiwa Mpango kama ifuatavyo:
Mosi, ni msomi wa kiwango cha juu ambaye amejikita kwenye uchumi kazi ambayo ameifanya vilivyo chini ya awamu mbili mtawalia akijizolea sifa ya kuaminika na kuchapa kazi. Daktari Mpango ana shahada ya Uzamivu (PhD) katika uchumi toka Chuo kikuu cha Lund nchini Sweden. Na historia yake inaonyesha ameutumia vizuri usomi wake hadi kuchomolewa na rais wa awamu ya nne toka aliko kuwa na kumwamini wadhifa mkubwa hadi ilipoingia awamu ya tano ikamtafuta na kumpa nyadhifa nyingine nzito kwa mfuatano hadi anateuliwa mbunge na waziri wa fedha aliyehudumu kipindi chote cha JPM.
Pili, ni muaminifu ambaye¬¬–––katika nchi ambayo kashfa ni sehemu ya maisha–––hajaguswa na kashfa yoyote tuijuayo hadi sasa. Kitendo cha kuhudumu chini ya rais aliyesifika kwa kutumbua–––kama ilivyo kwa rais SSH–––ni ushahidi tosha wa uaminifu wake.
Tatu, sambamba na sifa ya uaminifu, Mpango ni mchapakazi. Ndiyo maana ameweza kuhimili kasi ya uchapazi kazi ya hayati JPM kiasi cha kubakizwa kwenye wizara nyeti ambayo, kimsingi, ndiyo ilikuwa kwenye moyo wa JPM na ndiyo ilikuwa nyenzo yake kubwa ya kukamilisha miradi aliyoweza kuikamilisha kwa muda mfupi huku akianzisha mengine mingi.
Nne, ni mtulivu asiyependa makuu. Wakati wa kupitishwa na bunge, karibu kila mbunge aliyepewa nafasi ya kuchangia, alimueleza Mpango kama waziri ambaye hakuwa na majivuno wala kujikweza. Mmojawapo Joseph Kasheku alisema kuwa, wakati mawaziri wengi huwa hawawajali wabunge, yaani wanaringa kwa maneno mengi, yeye amewahi kupewa lift na Mpango.
Tano, ni msikivu. Usikivu unahitajika sana hasa kwenye nafasi ya umakamu ambapo kazi kubwa ni kumshauri na kumsikiliza mtu ambaye ana mamlaka makubwa ya kuweza kuajiri na kufukuza wakati wowote bila kuulizwa na asiwe ametenda kosa. Hili nalo, kadhalika,  waheshimiwa wabunge wamelithibitisha kuwa–––akiwa waziri wa fedha–––anasifika kwa uwezo wake wa kumsikiliza kila aendaye kwake bila kujali cheo chake. Hata kwa rais aliahidi kumsikiliza, kumtii na kumshauri rais bila ya kumsaliti.
Sita, Mpango si mtu wa kujikomba hasa nyakati hizi ambapo wapo wengi hutegemea kujikomba lau wateuliwe. Hatuzushi. Chini ya awamu iliyopita, tuliona watu wengi wakijikomba hadi JPM akiwakaripia kuwa hataki kusifiwa bali kuchapa kazi. Mfano, yupo waziri mmoja aliyewahi kuwa shabiki wa mmojawapo wa mafahari wawili wakati wa kinyang’anyiro cha kugombea urais mwaka 2015 waliokuwa wakiongoza hadi wakaharibiana na kutoteuliwa kupeperusha bendera ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Aliwahi hata kumponda JPM. Lakini siku chama kilipompitisha JPM na kumtupa mtu wake, wengi walishangaa jamaa huyu alivyogeuka haraka na kuwa kipenzi cha JPM kwa kujikomba kila namna asibanduke karibu naye hadi uchaguzi ulipokwisha akapewa uwaziri wa wizara moja nyeti. Hata hivyo, uzoefu unaonyesha kuwa mtu anayejikomba, mara nyingi, huwa hajiamini, wengine huwa na mapungufu wanayoficha kama vile kughushi au mengine kama hayo na utendaji wake unaweza kutoridhisha. Mtu yeyote anayejiamini, hajikombi bali kujiamini kuwa anatosha. Mpango anatosha kweli kweli. Na rais aliyemteua ameliona hili na atafaidika naye.
Saba, Mpango hajawahi kuonyesha kupenda makuu au kuyatafuta madaraka kwa nguvu. Maana, kila anapoelezea teuzi zake zote huwa anasema kuwa hakuwahi kuotea kufikia ngazi fulani. Huwa haachi kumshukuru Mungu kwa kumkweza. Mtu wa namna hii anaweza kuhimili nafasi ya makamu wa rais ambaye anaweza kumwamini na akamsaidia kama ilivyo kwa bosi wake ambaye wakati wa utawala wa JPM aliweka kichwa chake chini na kumuacha bosi wake afanye mambo aliyoona yanafaa yeye akishauri nyuma ya pazia. Uzoefu unaonyesha kuwa rais anapomteua mtu ambaye ni mtaka madaraka, watakosana kwa vile kila mmoja atakuwa anavutia upande wake.
Nane, Mpango ni mcha Mungu ambaye wengi waliomuongelea bungeni¬¬¬–––kama wanavyomjua–––walishuhudia hili. Mtu wa namna hii hawezi kulaghaiwa au kujiingiza kwenye wizi wa mali ya umma hasa ikizingitiwa kuwa mojawapo na sifa za wacha Mungu ni kutokuwa mafisadi na waroho wanaojilimbikizia mali. Hata nyumba yake kule kijijini kwao–––kama ilivyoonyeshwa kwenye mitandao baada ya kuteuliwa–––ni ya kawaida.
Kwa ufupi, kwa kuangalia baadhi ya sifa tajwa za Mpango, japo si zote, ni mtu anayefaa kumsaidia mheshimiwa rais kutekeleza majukumu yake bila shaka yoyote. Kimsingi, sasa ni wakati wa Mpango kuonyesha ukali wake kama alivyosema wakati akithibitishwa na bunge kuwa yeye si mpole bali mkali hasa kwa majizi ya mali za umma. Hivyo, si vibaya kumpa pongezi rais SSH kwa chaguo bora lisiloleta mgawanyiko wala malalamiko tokanana kutokuwa na makundi.
Chanzo: Raia Mwema leo.

No comments: