The Chant of Savant

Tuesday 8 November 2022

Boresheni na Rekebisheni Jeshi la Polisi na Nchi Nzima

Malalamiko ya ulaji wa rushwa dhidi ya jeshi la polisi, hata kama yana ukweli, ni nyenzo ya kulisaidia taifa letu kujua tatizo na kuboresha na kurekebisha jeshi hili muhimu. Kwanza, tukubali kuwa askari polisi ni watu kama sisi. Pili, tukubali kuwa wana akili timamu kama sisi. Tatu, tukubali kuwa wamekuwa wakaiishi maisha ya kupunjwa mishahara na stahiki nyingine sawa na maeneo mengine. Hata hivyo, tukukiri pia. Mlinzi wa mlangoni anapopunjwa, madhara yake na mbinu anazotumiwa ni tofauti na mpishi aliyeko jikoni. Japo watanzania wengi wa kada mbali mbali ukiondoa wanasiasa na wahubiri feki wa dini, wanaishi maisha ya kupunjwa, wanaishi kwa ‘nguvu au kipato’ vya ziada.
            Kuna usemi kuwa kila mbuzi hula kwa urefu wa kamba yake. Tukizingatia maana ya usemi huu, polisi wanakula kulingana na ulaji uliowazunguka. Mfano, sitegemei polisi malaika ambaye mshahara wake hautoshi hata kwa nusu mwezi, amkamate mhalifu ambaye yuko tayari kumkatia kitu aache kukipokea hata kukiomba. Hii ndiyo hulka ya binadamu yeyote mwenye akili. Huwezi kumkondesha mchungaji anayechunga ng’ombe wanaonyonyesha. Akienda malishoni atawakamua tu taka usitake japo ujifanye kutoliona hili.
            Jeshi letu la polisi sawa na idara nyingine nyingi limekuwa likiishi kijima. Kabla ya Hayati Rais John Pombe Magufuli kuwajengea lau nyumba za kuishi japo si kwa wote, polisi wengi ima walikuwa au wanaendelea kuishi uraiani jambo ambalo pia linawafanya waishi kiraia ili kuepuka madhara ya kuishi kipolisi au kuishi maisha ya hovyo na yasiyo na heshima. Kama haitoshi, polisi, sawa na watumishi walio wengi, wanalipwa mishahara kidogo. Je hapa unategemea nini? Je kwanini polisi wasipokee na kula rushwa na kuongoza katika jinai hii kutokana na ukaribu wao na wahalifu wanaojua madhara ya kufungwa? Kimsingi, watumishi wengi wanapokea na kula rushwa sema wanazidiana kutokana na maeneo yao na ukaribu na mishiko.
            Kama ilivyo kwa mpishi na mlinzi wa mlangoni, uwezekano wa mpishi kupata ulaji mwingi ni mkubwa kuliko mlinzi. Uwezekano wa polisi kupata rushwa kirahisi ni mkubwa kuliko mfagiaji ambaye asipokuwa mjanja kuiba siri za ofisi na kuwauzia waandishi wa habari hasa kwenye ofisi nyeti za umma, hapati kitu. Kama nilivyobainisha hapo juu, polisi ni watu wenye akili na mahitaji kama sisi.  Unategemea nini unapomkondesha yaya wa mtoto wakati anaweza kuyafikia na kuyanywa maziwa ya mwanao au chakula chake? Mbali na hilo, polisi wanajua umuhimu wao katika kuendesha nchi. Wanawalinda walaji wazuri kama vile wanasiasa na wazito wa serikali. Wanaona wanavyopwakia ulaji wakati wao wakiachwa wafe njaa. Je watakubali wafe wakati kuna mazingira wezeshi na rahisi ya kuomba na kupokea rushwa?
            Zamani jeshi la polisi lilikuwa la watu wasiokwenda sana shule. Siku hizi limejaa wasomi tena waliobobea wanaoona namna nchi inavyoliwa au kuuzwa. Wanajua namna siasa inavyotumiwa kupata utajiri wa haraka au kulinda biashara na dili za wakubwa. Kwanini wasipige njuluku? Hapa hoja ni nini? Mosi, tuboreshe si maslahi ya askari bali hata jeshi zima kwa kutoa fursa kwao kuishi sawa na wengine kwa kupata stahiki yao. Tukuze uchumi. Tuchape kazi. Tupambane na matumizi mabaya ya fedha na ofisi za umma, ufisadi, uvivu, kufanya mambo kwa mazoea na kutenda haki kwa wote. Huwezi kumpunja mshahara hakimu au jaji akaacha kupokea rushwa. Huwezi kumpunja mshahara daktari, mkemia, mkunga na muuguzi wakaacha kuiba dawa au kupokea rushwa toka kwa wagonjwa. Huwezi kumpunja mwalimu mshahara akaacha kuuza mitihani na kulazimisha twisheni. Ni rahisi hivyo. Hawa ni binadamu tena wenye akili timamu tu.
            Sipendi rushwa wala siitetei. Pia, sitetei kutotenda haki au kupunja wengine wakati wengine wakila na kusaza kama ilivyo kwa wanasiasa na wakubwa wetu wengi. Tumekuwa tukisoma kwenye taarifa ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali namna nchi inavyopoteza mabilioni ya shilingi kila mwaka wa fedha. Hali ni mbaya hadi watu wanapiga hata magari ya serikali kana kwamba serikali haipo. Je polisi na wanyonge wengine wanaopunjwa mishahara na stahiki zao mnadhani hawajui?  Wanajua tena sana. Wanajua viongozi wanaopiga ulaji sana. Wakubwa wanaoshirikiana na wafanyabiashara kupitisha mambo yao. Wanawajua wakubwa wazembe na wanaotumia vibaya fedha za umma na ofisi. Wanajua wazito wanaosamehe kodi. Wanajua kila kitu. Ni bidamu wenye akili hawa.
            Leo sitadurusu mengi. Kimsingi, tuboreshe jeshi la polisi. Tuboreshe mishahara ya watumishi wote nchini bila kusahau bei za mazao ya wakulima. Viongozi wawajibike na kubana matumizi. Tukuze uchumi. Tufuate katiba inayosema kuwa kila mtanzania anastahiki kutendewa haki na kupata stahiki ya jasho lake. Tupunguze ukubwa na matumizi ya hovyo ya serikali. Tubane matumizi. Tutawalane kwa haki, ukweli, na uwazi. Tuache uzururaji na kuponda raha. Tuache ubabaishaji na uvivu wa kufikiri na roho mbaya na uchoyo vya kimfumo. Kimsingi, tusiboreshe si jeshi la polisi na kada nyingine tu bali nchi nzima kwa ujumla.
Chanzo: Jamhuri leo.

No comments: