Kabla ya kuanza kuishi hapa Kanada, nilizoea aina kuu tatu za ubaguzi. Mosi, ule rangi ambao ulikuwa ukifanyika nchini Afrika Kusini na Marekani. Hata hivyo, sikuwa nikiuhisi sawa na wahanga wake. Pili, ni ubaguzi wa baadhi ya ndugu zetu wa kiasia walioletwa na wakoloni kuwawaidia kututawala na kutunyonya ambao waliachwa nyuma, na kutokana na ukarimu wa Kiafrika, tuliwapa uraia siku tulipopata Uhuru. Ubaguzi niliuihisi tokana na tabia yao ya kujitenga nasi n ahata kutengana wao kwa wao tokana na mfumo wa mchafu wa caste. Nakumbuka kabla ya Hayati Christopher Mtikila, tena peke yake, kushupalia na kuukemea wazi wazi ubaguzi huu, wenzetu walikuwa wakijitenga nasi kwa kila kitu isipokuwa maduka yao tuliyojaa na kuwajaza utajiri wakati huko walikotoka tunabaguliwa wazi wazi na kitu kama hiki kisingetokea. Hata hivyo, kilichofanyika ni kupunguza ubaguzi lakini siyo kuacha.
Tatu, ni ule wa kujibagua na kubaguana sisi kwa sisi kikabila au kidini ambapo utawasikia mfano kabila fulani likisema wao ni bora kuliko mengine au dini fulani wakiwaita wengine majina ya hovyo kama vile makafiri, wenye dhambi na upuuzi mwingine.
Baada ya kuweka kila kitu kwenye muktadha, sasa tuangalie ni namna gani wabaguzi na wahanga wote wanashiriki dhambi hii hata kama ni kwa sababu na viwango tofauti?
Kwanza, nikiri kuwa ubaguzi wa aina yoyote ni matokeo ya ugonjwa fichi wa akili. Huwa najiuliza hapa Kanada ambapo kusema nyeusi ni kama dhambi nionapo watu wana majibwa meusi lakini wasiyabague ila wawabague wengine wasio kama wao. Je hawa watu si wagonjwa? Ninapotoa mfano wa Kanada nisieleweke kuwa Wakanada wote ni wabaguzi. La hasha. Hata wazungu wote si wabaguzi japo mifumo yao yote ni ya kibaguzi. Ninachotaka kuonyesha ni namna gani wabaguzi walivyo wagonjwa wa akili.
Pili, ubaguzi ni matokeo ya ujinga. Kwani, hata ukitumia mfano wa juu, utaliona hili fika. Kama siyo ujinga, inakuwaje tubaguane kwa misingi ya rangi lakini wakati tunafanana kwa vitu vingi muhimu kama damu, mahitaji na viungo? Nani huyu mjanja aliyemwandikia barua muumba kumuumba ‘bora’ kuliko wengine?
Je ugonjwa wa akili fichi unawakumba wabaguzi tu au hata wahanga wa ubaguzi? Naweza kusema kuwa pamoja na ujinga, vinawakabili wote. Mfano, nashangaa namna tunavyoweza kunyamazia au kuvulimilia ubaguzi wa wazi kama nilivyoonyesha hapo juu. Nashangaa namna ambavyo wahanga, tokana na athari ima za kidini au kikoloni wanaweza kupapatikia na kupwakia tabia ya ubaguzi kama vile kujitenga au kujiona bora wakati wote tu sawa. Je licha ya kuwavumilia na kuwanyamazia wanaotubagua tena kwenye nchi zetu, hatu hatuwapapatikii kiasi cha baadhi ya ndugu zetu kupoteza fedha nyingi wakinunua kansa ya ngozi wakiusaka ‘weupe’ feki?
Kama nilivyoonyesha, tunaweza kuuhisi ubaguzi kwa viwango tofauti. Wakati tukiwapapatikia wale wanaotubagua kwa misingi ya rangi zao huku tukiwaita weupe wakati wakija huku nao wanaitwa watu wa rangi (people of colour) sawa nasi ili wasiuchafue weupe ambao nao ukiuangalia unaushangaa kwa vile vyeupe ni chokaa, mifupa mikavu na theluji lakini siyo wao ambao kimsingi ni pinki, wakija huku wanayong’onyea kuliko sie Waswahili ambao tushazoea ubaguzi japo ubaya hauzoeleki.
Kuna aina mpya ya ubaguzi ambao hapo awali sikuujua. Ni ule ubaguzi tena wa kunuka zaidi unaoandamana na unyama kama ule unaofanyika huko Mashariki ya Kati ambapo watumishi wengi wa ndani wa Kiafrika wameuawa na wengine hata kuuzwa utumwanni kwenye nchi za Maghreb huku Waswahili na serikali zetu tukijikanyaga badala ya kutoa onyo kuwa nasi tunaweza kufanya jino kwa jino japo siyo sawa.
Ubaguzi mwingine ni wa kisiasa ambapo mataifa ya Magharibi huyaona mataifa mengine kama hafifu nayo yakijiona bora. Jiulize. Inakuwaje wao wanapotaka kuingia Afrika ni rahisi kuliko sisi kuingia kwao? Pia, kilichotokea ilipofumka vita ya Urusi na Ukraina inaweza kukupa picha ya ninachomaanisha kuhusiana na mfumo wa kibaguzi wa kimagharibi. Wakimbizi toka Ukraina walipokelewa kila mahali huku nchi yao ikimiminiwa mabilioni ya dola wakati mataifa kama DRC na Sudan ya Kusini ambayo yamekuwa na vita tangu kuanzishwa yakikodolewa macho mbali na kulaumiwa.
Sasa nini kifanyike?
Tujitambue kwa kuelimishana na kukataa kubaguliwa kwa namna yoyote. Tuweke msimamo wetu wazi kuanzia kwenye mifumo yetu. Mfano, naweza kuutoa kwa Hayati Shehe Abeid Aman Karume, Rais kwa kwanza wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar aliyepiga marufu ubaguzi kwa vitendo akihimiza Waswahili waliozoea kuonekana kama watumwa kuoleana na wamanga waliozoea kujiona mabwana. Nadhani, kama Hayati Karume angetawala hata kwa miaka 24 kama Hayati baba wa taifa, Mwl Julius Nyerere, kusingekuwa na uPemba na uZanzibari visiwani ambao nao umejenga aina fulani ya ubaguzi ambao ni muendelezo wa aina hiyo kwa upande wa bara ambapo wamanga huwa wanawaoa mabinti wa Kiswahili huku wao wakigoma kuwaozesha mabinti zao kwa Waswahili. Ndugu zangu wa Pwani wanalijua sana.
Pia, tuambiane ukweli hata kama unauma ili pande mbili ziwe tayari kujifunza na kufundishana namna ya kuishi pamoja kutokana na ukweli kuwa wote tunategemeana.
Kwa leo naona nihitimishe hapa nikizidi kusisitiza umuhimu wa kujiamini, kujielimisha, kuelimishana na kujitambua mbali na ithibati katika kutetea ukweli ambao uko wazi.
Chanzo: Jamhuri leo.
No comments:
Post a Comment