The Chant of Savant

Monday 5 December 2022

Waombeni Mababu na si Kakakuona

Babu Yangu Mzee Busara aliwahi kunambia Kitu Kimoja ambacho sitakisahau. Alizoea kusema kuwa Ujinga si Mzigo bali ni Balaa. Maana, Mizigo Mingine ni Mali. Hebu fikiria ukitwishwa Mzigo wa Almas ukaishia Nao. Si unaishia kuwa Kibopa Ghafla bin Vuu? Na Mzigo Wenyewe kama ni Totoz tamu kama Embe Dodo unadhani utasikia Uzito au? Nikiwa ndo natoka kuupiga Mma kwa Mama Nkuzi si nikafika Nyumbani na kumkuta Bi Mkubwa Nesaa amesinyaa huku amesujudu Mbele ya Runinga. Niliuliza kulikoni? Bila Ajizi alijibu “huoni kwenye TV watu wanavyosujudu kumuomba kakakuona awabadilishie maisha yao?!” 
        Bila hata aibu kuwa mie ni mlevi msomi na mjuaji alisema “Njoo upige magoti tututoe maombi yetu.” Pamoja na maulevi yangu nilifikicha macho na kuangalia kituko ambacho sikutegemea kingehusisha walevi wenye akili timamu. Runinga ilionyesha walevi kule Morogorogoro wakisujudu mbele ya kakakuona eti wakiwasilisha maombi yao. Nilisonya na kusema “senzi kabisa. Huyo mdudu anaweza kuwasaidia nini kama siyo wendawazimu wa mchana?”
         Hetu tuache utani. Nani angeamini kwenye karne ya 21 kungekuwapo bado waja ambao wangepoteza juhudi na muda wao na kufanya kila walichoweza kumsujudia na kumsumbua kwa kumuomba mnyama na tena asiyejua wanachofanya achia mbali kuwa na uwezo wa kuwapa walichokuwa wakitafuta? Nilijisemea kilevi “wajinga wa wakubwa tena wa mwisho.” Bi Mkubwa hakunijibu. Maana, kilichofuata nikieleza nitachekwa na kuonekana kama si mrume kitu. Hata kama nilipewa adhabu ya kudeki nyumba nzima, wewe inakuhusu au kukusaidia nini? Hayo tuyaache.
        Naomba tufikiri pamoja tena kilevi. Je inakuwaje watu wanaojiita wazima na timamu kuamini upuuzi wa dada, sorry kakakuona kama siyo kufilisika kiakili? Eti mtu anaombea amani kwa kakakuona. Amani hailetwi na kaka wala dadakuona. Amani inaletwa na kujenga tabia ya amani na kutenda haki na kujitenga na dhuluma. Mwingine eti anaomba umeme kwa kakakuona utadhani kakakuona ni TANESCO! Sasa kama kakakuona anaweza kuleta umeme, TANESCO ya kazi gani? Yupo aliyeomba TANESCO kuacha ubangaizaji asijue kuwa kuwawajibisha ndiyo njia sahihi ya kuachana na kamchezo hako.
        Mwingine eti anaomba fedha kwa kakakuona. Sijui kama kakakuona anaijua hata hiyo fedha ukiachia mbali kuwa haiwezi kupatikana bila kuchapa kazi na kutumia akili vilivyo.
Hakuna kilichoniacha hoi kusikia eti wengine wakiomba wachumba toka kwa kakakuona. Unashindwa kuwasikiliza wazazi na kuwa na tabia njema na kutegemea mchumba aletwe na kakakuona au wale wahubiri uchwara kama wale wa kisulisuli ambao walikuwa manunga! Huwezi kupata mchumba toka kwa kakakuona zaidi ya majaliwa na jitihada zako. Mwingine aliomba mvua kwa kakakuona kana kwamba yeye ni wingu. Mvua hailetwi na kakakuona bali hali wezeshi kama vile kutunza mazingira na majira.
        Yupo aliyeomba upendo kana kwamba kakakuona ni msuluhishi. Unamchukia jirani au ndugu yako halafu unategemea kakakuona alete upendo. Upendo huanzia moyoni na siyo nje ndugu zanguni. Huwezi ukapanda chuki ukategemea kuvuna upendo. Mwingine aliomba amani asijue kakakuona mwenyewe haijui kutokana na kukaribia kutoweka tokana na ushirikina wa wanadamu! Usipande ujinga ukategemea kupata maarifa wala kupanda ubangaizaji ukategemea utajiri. Huwezi ukatumia njia feki ukategemea kupata majibu sahihi. Ubangaizaji huzaa ubangaizaji. Uvivu kadhalika huzaa uvivu ukiachia mbali ujinga kuzaa ujinga na maangamizi.
        Hebu tufikiri pamoja tena kilevi. Je anajua Kiswahili au kiluguru? Je mlipomuomba mlipata majibu ya maombi yenu zaidi ya kujihadaa kwa ujinga na uvivu wenu wa kufikiri? Tangu lini kakakuona akabadili mambo wakati yeye anajiishia kama alivyojaliwa? Heri mngemuomba sungura maana tunaaminishwa kuwa ana akili kuliko wanyama wote? Sidhani kama wanyama wanawaamini nyinyi wajinga. Watawaamini vipi wakati hamjiamini? 
Ukiangalia hata maombi yaliyoombwa ni tofauti na shida za wahusika. Sikuona aliyeomba kuacha uzinzi, uvivu, ngono muwawana na mambo mengine kama hayo. Sikusikia hata mmoja akiomba kuondokana na mtima nyongo, roho mbaya, uchoyo, ulafi, ubabaishaji, ufisadi, wizi, ujambazi, rushwa na majungu, urongo na ushirikina.
        Sasa kama mnaumuomba kiumbe maskini anayekaribia kutoweka kama kakakuona tokana na ujinga, uroho, upogo, na ushirikina wenu, hao mababu zetu watafanya kazi gani? Maana mmeomba miungu yenu imeshindikana. Mmewageukia wanyama. Itashindikana. Basi wageukie mababu zetu waliowanunia baada ya kufundishwa kuwadhalilisha, kuwakana na kuwatukana kwa kupwakia dini za watu msijue ni ukoloni mtupu. Naona yule anasonya huku akitikisa kichwa. Kwani nazusha? Mbona mlikana lugha hata majina yao ukiachia mbali mitambiko yako mkapwakia mitambiko ya kigeni iliyogeuzwa majina? Jaribu kufikiri kabla ya kunihukumu hata kama naongea kwa nguvu ya kanywaji.
Tumalizie kwa kuwaomba na kuwashauri walevi na wale wote wanaojifanya hamnazo kuacha ujinga na hata ukumbaff wa kuabudia vitu visivyo na faida wala uwezo wa kuwasaidia kutatua matatizo yao ambayo wameshindwa kuyatatua tokana na uchizani wao. Kama mmeishiwa hivi, basi ombeni mababu zenu lau wanaweza kuwasaidia. Tukutane wiki ijayo.
Chanzo: Jamhuri Kesho.

No comments: