How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Thursday, 26 October 2023

Kazi ya elimu na siri kali si ajira

Rais Samia na mkwewe Waziri Mohamed Mchengerwa pichani
Si uzushi wala ufyatu kufyatuka kuwa elimu siyo ufunguo tena. Naiona kama kufuli hasa kwa wasiojua namna ya kuifyatua kupambana na taabu za kufyatuliwa na wakoloni na mifumo tuliyorithi kwao tukaridhika na kushindwa kuifyatua kukidhi mahitaji yetu. Huwa nasikia vilio kotekote. Mafyatu wanafyatua na kusomesha vitegemezi, mengine kwa njuluku za ukwapuzi, yakitegemea vipate ajira sirikalini ili kufyatua ukwasi. Ushaambiwa siri kali. Unategemeani? Hujui inawenyewe na kazi yake ni kutunza siri kali tena kwa ukali na achikali?
        Huwa nataabika, kufyatuka, na kuumia. Wakati mwingine hufarijika kuona mafyatu waliosomeshwa intenesho skuli wakisota hasa ambao madingi wao siyo wanene kayani. Mafyatu wanasoma kwelikweli japo hawafikirii sawasawa. Wafyatuapo ung’eng’e, yesi ovukozi una kikohizi kakikoze kiufyatuzi, utadhani kingi Chaz kumbe jobless! Wanazo stashahada, shahada za uzamivu na uzamizi wanaolia ajira. Wengine wamevamia umachinga na utapeli halafu wanaambiwa mambo yanogile. Really?  How? Yananogile kwa nani wakati hata chawa wanatanua kuliko waja?
        Naona yule anatikisa kichwa. Unadhani ufyatu au ukweli tena mtupu? Kama mlisoma muajiriwe, mmenoa na kufyatuliwa sana. Kama wewe siyo mojawapo wa koo fyatu maarufu ziloteka, kufyatua, na kujimilkisha kaya, umeula wa chuya.  Imekula kwako. Siku hizi sifa za kuula na kunenepa uwe mnene ni jina nene: si mavyeti yako uchwara. Kinachoangaliwa si unajua nini bali nani. 
        Bila jina nene, kwako kiza kinene kama mimi niliyefyatua masayansi yote na kufyatuka na distinction ya extinction chuoni nikaishia ukapuku. Mjombangu ana PhD in acrobatic and romantic science lakini ameishia kuwa cha bia. Yeye na kanywaji na kanywaji naye. Ameshindwa kutumia acrobatic romance science kukifyatua kitegemezi cha mnene akapewa uwaziro na kuufyatua kuliko kufyatuliwa kama alivyo!
            Seriously. Kweli lengo la elimu ni kumfyatulia fyatu kibarua kiitwacho ajira kwa lugha ya kiungwana au kumjengea uwezo wa kuyafyatua maisha? Inakuwaje mafyatu wanafyatukia na kushobokea kuajiriwa na si kujiajiri au kufyatua ajira? Ukisikia ukale na ukoloni ndiyo huu. Je kazi ya serikali kweli ni kuajiri au kuhakikisha usalama na ustawi wa wana kaya japo yetu haifanyi hivyo? Mnaohangaika kusaka ajira zisizokuwapo hamuoni nyingine bwerere kama vile ukulima, ufugaji,  biashara, ujasiriamali, na stadi za mikono?
            Msiotaka taabu bali kuufyatua kirahisi, fyatueni vyama vya siasa. Vinalipa ikizingatiwa kuwa unafyatua ruzuku na kufyatua mke mdogo, shangingi la shumbwengu au nyumba ntobhu. Huwezi, fyatua dhehebu na kujipachika cheo kikubwa na kitukufu na kutenda miujiza? Huoni wachunaji wanaofyatua kondoo kupitia uchungaji, utume, unabii na mengine feki wakati nyuma ya pazia, matapeli wa kawaida? Kama si utapeli ni nini kuwauzia mafyatu maji, vitambaa, na upuuzi mwingine? Kama kweli upuuzi huu unaponya, iambieni serikali ifunge mahospitali wao watibu wagonjwa. Ufala na utapeli mwingine, sina namna ya kuueleza. Mafyatu mazima tena masomi, yanafyatuliwa na vihiyo kuliko wao!
         Huwezi, katafute kitegemezi cha mnene chamani au sirikalini ukifyatue au kikufyatue uule. Huu unaitwa uwekezaji wa ndani. Unafyatua au kufyatuliwa na kitegemezi cha mnene mambo mswano. Mungu akupe nini? Unataka akugeuze chawa? Kama huna mashairi na ngonjera ya kufyatua vitegemezi vya wanene, jigeuze chawa ufyatue sifa na mapambio uzawadiwe ulaji uukate kama wengi ninaowajua walioula kwa kuukana ubinadamu na kufyatukia uchawa. Mjini shule. Hujui!?
        Unashindwaje kufyatua dhehebu wakati wavivu wako wengi wanaoamini miujiza uchwara na vitu vya ajabuajabu badala ya kuchapa kazi? Kwani huwaoni? Kuna fyatu mtoto wa mganga wa kienyeji namfahamu. Aliyeogopa umande ameula baada ya kufyatua dhehebu la uongo na ukweli. Japo alichemsha shuleni, amejifyatulia ajira hata kama ni haramu. Ukishindwa uchunaji wa kujipachika si uanze uganga wa kienyeji. Mbona wagonjwa tena wa akili na fikra bweee kayani. Unashindwani kuchukua vitunguu ukachanganya na majani na kuwapa wagonjwa na kuula? Shauri yako. Imezidi sana anzisha NGO ya kutetea hata wezi wa mali na njuluku za mafyatu. Unashindwa kufokafoka matusi huku ukikata makalio, kuvaa hereni, kujitia tatuu, na kupewa majina ya madini na kuula!Hutaki kuitwa tanzanite platinum siyo?
            Walioshindwa hayo hapo juu, waje kwangu niwape dawa ya utajiri. Dawa yangu ni kiboko. Ukiinywa, kila utakachogusa kinageuka madola na unaukata kirahisi.
Nilivyowaka mfukoni, Sijui leo nitakula nini!
Chanzo: Mwananchi jana


No comments: