Naamini mafyatu wote wazima. Kiza, kupanda gharama za maisha, na vituko walioshitiwa kuregeshwa na wafu kufufuliwa havijawafyatua mkafyatuka. Anyway, waache wafu wazike wafu wenzao. Juzi niliwaza cha kufyatua, si zikaja kumbukumbu za zama za dhahabu nikisomea shahada ya uzamivu katika falsafa za uumbaji na uhuishaji kimazingaombwe na viini mato au abracadabras kisambaa. Ndipo nikarejea kwenye ufyatuzi na ufyatuaji. Leo nawaletea falsafa iliyoanzishwa na gwiji aitwaye Jean-Pierre de Biere Kanyuwaji kwa kisambaa aliyefyatua kitu ambacho wengi walikishangaa, hasa mafyatu walioona vitabu kama mimi ukichia mbali vihiyo na vilaza na wasaka tonge walionoa alipoumba ili kufanana na Mungu japo alikuwa muungu akiitwa hata Mungu. De Biere alitegeneza kiumbe cha ajabu na kidhabu akakiita Bashiti, yaani Binadamu aweje siyo halisi ingawaje tajitia ithibati kama stizahi ya ubonzo, ufyatu, kidhabu ulimbukeni, unyang’au na uzabazabina wa baadhi ya ngurumbili hasa mabashiti.
De Biere, pamoja na utaalamu wake, alisifika kwa ukatili na usanii. Hivyo, alitengeneza kiumbe afriti na cha hovyo aliyemtumia kufanya na kuficha uovu wake ili asilaumiwe. Jamaa, mbali na kuabudiwa, alipenda sana kusifiwa na kupendwa hata kama ilikuwa kwa uongo au kujiridhisha. Alijaliwa kila kitu isipokuwa hekima. Alikuwa bingwa wa kuigiza kiasi cha kuwahadaa wote waliomsujudia na kumwabudu wakidhani muungu kumbe ka mchezo ka paka kutumia ushanga wa vichwa vya dagaa kufanya ibada.
Kwa vile Godi aliumbwa kwa udongo, de Biere aliumba kwa uchafu aliouita UBABE yaani Uchafu badala ya ardhi bora endelevu. Mungu alimuumba Adam akiwa uchiNa de Biere alimuumba Bashiti hivyohivyo. Alimuosha, kupiga utuli, na kumnenepesha ili ngurumbili wamuogope atakapokuwa akifanya kazi chafu za de Biere. Alimvisha nguo za gharama na kuwaambia ngurumbili waliokuwa karibu naye wamsujudie. Tofauti na Mungu, wapo waliomsujudia hasa wachumia tumbo pia, waliokataa shiriki hadi wengi kunusurika au kunyongwa chini ya uangalizi wa hiki kibashiti cha de Biere.
Leo ngurumbili anaweza kuwa hivi kesho vile, usijue hata msimamo wake. Mara nyingi, japo si wote, ngurumbili wafikiriao kwa manonihino na matumbo ni Bashiti. Hivyo, nimeishakupa maana ya bashiti. Je wewe ni bashiti?
Turejee kwa bashiti. Kwa vile muumba wake alikuwa muungu na siyo Godi, alirejesha namba. Walikuwapo wengi waliokwazwa na ufyatu, unaha, upogo, kujikomba, roho mbaya, na uroho wake wasijue yule ni bashiti. Ukiwaenga hutaowadhania achia mbali kuwajua. Waliosherehekea kuwa muungu wa bashiti amekitoa forever walikosea pwenti. Hawakujua sifa moja ya kuwa bashiti ni kubadilika na kuishi kama kinyonga. Anaimba na kucheza kulingana na mlio wa ala. Kadhalika, bashiti kwa sababu ni bushiti wa kwanza, alimaizi na kujua sana sanaa hii ya ukinyonga.
Alipogundua kufa kwa muungu wake kunaweza kuwa mwisho wake, alijibadili kama kinyonga na kuanza kuabudia muungu mwingine uitwao Sahasu kiumbe kingine cha de Biere. De Biere aliuachia muungu huu vitendea kazi vyote. Kwa kujua hili, Bashiti alianza ibada zake za sanamu kimyakimya akingojea kufufuliwa. Wasiojua hili hili, walidhani Bashiti alikuwa amekwisha kifalsafa wasijue Sahasu angemfufua. Haukupita muda ikapigwa tarumbeta kukusanya mafyatu wote na kutangaziwa kufufuliwa kwa Bashiti. Wapo waliozimia huku wengine wasiamini. Ndo ubashiti huu mafyatu wangu. Msijiumize bure. Ngurumbili ni nani na nini wakati yupo kwa muda kama kivuli kabla ya kugeuka vumbi. Kama de Biere, alomfinyanga Bashiti na Sahasu alikitoa forever, nani atabakia?
Kwa vile fyatu anihaririye hunipangia idadi ya maneno, inabidi nifupishe kwa kutoa masomo tuliyopata kwenye kisa hiki cha Bashiti na ubashiti. Kimsingi, tunajivunza kuwa mabashiti hawaaminiki. Pili, kuwa ni vinyonga. Tatu, kuwa lazima tuwaepuke kama ukoma. Nne, tusipoteze muda nao kwani watatoweka siku moja. Tano, tuugope ushirikina, ibada za sanamu, na dhambi nyingine zitokanazo na ubashiti.
Mwisho, lazima, na muhimu kabisa, najua mafyatu wanaweza, watokomeze mabashiti na ubashiti pale inapojitokeza fursa ya kufanya hivyo. You know what I mean. Sifa kubwa ya mabashiti ni kutoshitiana na wakishitiana na kwa muda kuwahadaa ngurumbili waliofyatuliwa
Kumbe nasoma kitabu cha Abunwas!
Chanzo: Mwananchi kesho.
No comments:
Post a Comment