Liberal Peace Conflict, Gender, and Peacebuilding

Liberal Peace Conflict, Gender, and Peacebuilding

Thursday 29 August 2024

Unapochagua Mchumba Jua na Zingatia Yafuatayo

Kuoa au kuolewa, au kuoana kama wasemavyo siku hizi, si suala la kukurupuka au siku moja kama kununua tiketi ya bahati nasibu au kukodisha taxi. Katika kuchagua mwenza wako (wa maisha au vinginevyo kama hamtafanikiwa), unapaswa uwe makini tena sana. Usikurupuke kuamua kuingia uhusiano ambao una mwanzo lakini hauna mwisho isipokuwa kifo hasa kwa wale wanaofunga ndoa za kikristo (hata walio kwenye ndoa tofauti wangetamani iwe ni ‘kufa na kuzikana). Hivyo, ni muhimu kumjua mwenzako kwa madhaifu na ubora wake. Lazima uwe na orodha ya vitu ambavyo ungependa mwenze wako awe navyo kama vile umri, atokako, tabia, urefu, uwezo wa kufikiri, mvuto, mengine mengi kulingana na utakavyo bila kusahau kama nawe unavyo au unapimwa hivyo. Kama ilivyo kwenye kujenga nyumba au kununua gari, lazima ujue ukubwa hata muundo wa nyumba. Kama ni gari, ungependa kujua aina, ulaji wake mafuta, nguvu (horsepower), rangi, mwaka wa kutengenezwa na hata ubora na udhaifu wake.

            Kwa vile ndoa ni taasisi unaoingia kwa sababu za upendo na uhuru wa kuchagua, siyo sawa na kuzaa watoto au kuzaliwa. Wazazi hawachagui watoto wala watoto hawachagui wazazi kwa sababu hawana uwezo wa kufanya hivyo. Kwa upande wa ndoa, una chaguo huru ambalo likishafanyika, huodoa uhuru huo. Hivyo, unapaswa kuwa makini, mvumilivu, na mwelevu kufikia kusema I do.

            Tofauti na gari na nyumba, ndoa siyo mali yako binafsi. Ni mali ya jamii hasa kwa jamii za Kiafrika ambapo familia za pande mbili huanza machakato na hatua mpya ya uhusiano wa karibu usio na mwisho vinginevyo ivunjike japo si lengo lake. Hivyo, tofautisha kumchagua rafiki mnayeweza kufarakana na kuamua kuvunja urafiki. Ndoa ni zaidi ya urafiki maana, rafiki hana haki kisheria kumrithi au kumrithisha rafiki yake mali zake pale inapotokea kufariki. Tofauti, mwanandoa anakuwa na haki hata zaidi ya wazazi na ndugu kwenye kukumilki wewe na mali zako. Hivyo, huyu si mtu wa mchezo au wa kukwapukia. Siyo mchezo wa pata potea wala kamari bali jitihada makusudi zinazolenga kujenga uhusiano wa karibu katika maisha yenu yote. Hakuna anayefunga ndoa anayeomba au kutegemea ivunjike japo nyingi zinavunjika.

            Katika mila za Kiafrika, ndoa huwahusisha wazazi, ndugu, na jamaa katika kuanza kuijenga, hata wakati mwingine kuimboa na hufanya familia mbili tofauti kuwa moja. Familia mbili uhusisha familia nyingine nyingi ambazo hazikuhusiana kabla kuingia katika uhusiano usio na mwisho japo una mwanzo. Ndiyo maana tuna washenga, makuwadi, na wengine wengi tunawaowahusisha kwenye kuanza msingi wa ndoa ambao, kimsingi, ni watu wa karibu na wanaoaminika walio karibu nawe kwa uhusiano wa damu ambao, mara nyingi, huteuliwa na wazazi wetu tokana na ukaribu na imani yao kwao. Hii ni kutokana na wahusika kuwa na uzoefu wa muda mrefu mbali na ujuzi ambao huchukua miaka mingi kuupata.

Tunadhani utaratibu huu ndiyo uliowawezesha wazazi na mababu na mabibi zetu kutokuwa na talaka kwani ulikuwa siyo shirikishi tu bali wenye umakini zaidi katika kutafuta wahusika wanaofaa na kufaana tokana na walivyowajua. Kwa Waafrika hata neno talaka ni la kigeni litokanalo na lugha ya kiarabu iliyoleta Uislam. Kabla ya hapo, hatujui dhana hii ilivyotafsiriwa. Japo talaka zinatolewa, huwa si jambo la kufurahisha wala kutamani liwepo ukiachia mbali kwenye zile ndoa ambazo ni rahisi kuoa na kuacha kulingana na misingi na taratibu zilizojiwekea.

Kumalizia, bila kuzama zaidi kwenye mada tokana ufinyu wa nafasi. Wanyama hawana send offs, vyeti vya ndoa wala mikataba yanayojulikana kwa binadamu, wana dalili zinazoashiria thamani ya ndoa ikizingatiwa na maarifa ambayo binadamu ameyachota kwao, lina mashiko au ghorofa bila kuangalia kichuguu? Hii ni elimu mwanadamu aliyoipata toka kwa mwalimu mchwa. Kama tukubalivyo kupata ujuzi huu toka kwa mwalimu huyu, kadhalika tukubali na ukweli juu ya taasisi hii ya ndoa toka kwa viumbe mbali mbali waliotuzunguka.

Chanzo: Mwananchi Jumapili iliyopita.


No comments: