Liberal Peace Conflict, Gender, and Peacebuilding

Liberal Peace Conflict, Gender, and Peacebuilding

Monday 5 August 2024

Epuka au Usiwe, Kuoa au Kuolewa na RST

Tumeumbwa watu kila aina wabaya hata wazuri. Kwa vile ndoa hufungwa na wanadamu, tunaomba tugusie suala nyeti bila kuonekana kama tunabagua au kuwawekea utu ubaya. Hivyo, siyo uzushi kusema dunia ina watu wazuri na wabaya. Leo tutaongelea tutakachokiita RST bi maana ya Roho mbaya, Sura mbaya na Tabia mbaya. Kwanza, tukubaliane. Kuna watu wenye sifa hizi.
Tutaanza na kisa cha kijana mmoja wa kiume mtanashati na handsome (hatuna Kiswahili chake). Kijana huyu alijaliwa elimu na kazi nzuri vilivyompatia kipato mbali na biashara zake. Pamoja na yote, tokana na makuzi yake ya kizazi cha zamani, hakuwahi kuwa kwenye mahusiano tokana na sababu zifuatazo:
        Mosi, malezi yake yalikataza uhuni au uhuria unaoanza kujitokeza kwa kuigiza wazungu ambapo watu wasiooa au kuolewa huanza mambo ya wanandoa. 
        Pili, alichelea kuzaa kabla ya kuoa jambo ambalo hakutaka liwe kikwazo katika ndoa yake. 
        Tatu, hakutaka watoto wenye mama tofauti aka rangi mbili.
        Nne, alikuwe mwenye aibu na mwenye kujitunza vitu viliviyomtenga na mambo ya starehe. 
        Tano, alitunza fedha ili baadaye awe na familia yenye maisha mazuri. Mfano, alijenga nyumba na kununua gari kwa ajili ya shughuli zake za kikazi na kibiashara kabla ya kuoa. 
    Sita, aliogopa kuwakwaza wazazi wake kwa kujiingiza kwenye mambo ambayo, kimila lazima yapate ridhaa yao. Hivyo, alingoja kupata mwenza atakapoamua kuoa.
        Pamoja na kijana yule kutotaka kuoa kabla ya kukamilisha malengo yake na kuheshimu taratibu, hakukosa akina dada waliompenda ima kwa sababu ya u-handsome wake, elimu yake, au fedha. Mwenyewe aliendelea kujijenga ili awe tayari kuanzisha familia yake. Siku ya kutafuta mchumba, alipata taabu sana. Kwanza, alikuwa mwenye aibu na ambaye hakuwa na uzoefu wa kuwa na mawasiliano na akina dada hasa akichelea wangemuingiza majaribuni.
        Kadri siku zilivyokwenda, dada wengi jirani waliomjua walimuona mdenguaji au mwenye tatizo. Hivyo, waliacha kumsumbua na kukosa imani naye. Hapa ndipo tatizo lilipoanza. Akiwa yuko tayari kutafuta mchumba, alijikuta hajui pa kuanzia. Akiwa katika mchakato, aliajiriwa dada mmoja kazini kwake ambaye, licha ya umri kwenda, alikuwa si mwenye sura nzuri na wala hakuwa mechi ya yule kijana si kwa tabia wala sura. Hivyo, tutamuita jimama.
        Tokana na muda kwenda, jimama lilipogundua kuwa yule kijana mtanashati hakuwa na mke wala rafiki wa kike, lilianza kumzoeazoea kiasi cha kuanzisha urafiki wa kawaida. Jimama lilikuwa lilishafanya kila aina ya ufuska, utoaji mimba, uhuni wa kila aina kuchumbiwa hata kuvunjika uchumba kutokana na tabia mbaya. 
        Yule kijana–––tokana na kutokuwa na uzoefu––––si jimama likamzidi ujanja likamshawishi kuanza mahusiano. Haukupita muda, jimama lilimtegeshea mimba. Kabla ya hata kujua la kufanya, jimama lilihamia nyumbani kwake kwa kisingizio cha mimba yake. Kwa vile hakutaka kuzaa bila kuoa, kijana alijikuta akiingia matatizo makubwa kwa kukubali kulioa lile jimama japo hakulipenda toka rohoni.
           Kwa upande wa jimama, lilishinda mambo matatu kwa mpigo. Lilipata mume tena msupu au mhandsome kama wasemavyo wakenya tena mwenye fedha na historia ya kutokuwa mhuni, na mtoto. Ni kama ilikuwa ndoa ya mwewe na njiwa. Alilitambulisha kwa wazazi wake, walistuka na kuhofia kulikuwa kuna namna lakini wasiingilie kwa kuogopa kumvunja moyo mtoto wao au kuingilia chaguo lake. Yule kijana aliamua kulioa hilo jimama.
                Maisha yalianza. Jimama lilokuwa pole kabla ya ndoa, ghafla, lilianza vituko kwa vile lilikuwa limeishaolewa na kumzalia mtoto. Mungu hamfichi mnafiki. Lijisahau. Lilianza kumchuna yule bwana kwa vile lilijua lilivyolazimisha ndoa. Hivyo, lilihofia huenda jamaa angeamka usingizini na kulipiga teke. Hivyo, zile tabia zake asili yaani RST zilianza. Kama tulivyogusia, jimama lilianza kuonyesha uhalisia wake. Lilianza kuwachukia ndugu za mumewe. Lilianza mahusiano na marafiki zake wa zamani wakiwamo hata ndugu wa karibu maana lilitoka kwenye  makabila ya wapenda fedha na ambao huchukuana ndugu kwa ndugu.
         Baada ya mume kustuka na kuanza kuwa mkali, jimama lilikosa kujiamini likaanza kusaka madawa ya mapenzi wa waganga wa kienyeji lisijue hakuna dawa ya mapenzi bali tabia njema, uaminifu, na mapenzi ya kweli. 
        Kufupisha kisa kizima, jimama liliishia kuachika tokana na RST. Hivyo, mnaopanga kuoa hata kuolewa, mjiepushe na RST iwe mke au mume. Tabia njema ni silaha tuliaswa. Kwa waoaji wasio na uzoefu, washirikisheni wazazi wenu yasiwakumbe yaliyomkuta kijana huyu asiye na hatia. Msikurupukie mahusiano bila kujiridhisha kuwa mnaingia kwa kuzingatia uchaguzi wenu. RST ni sawa kilema. Haitibiki. Iepuke. Ni vizuri wanandoa wakaendana kulhali japo wakati mwingine mapenzi hayachagui. Muhimu, tusilazimishe ndoa. Haitadumu. Tusitafute dawa ya mapenzi. Hakuna. Tusiingizane mkenge katika ndoa. Tuwaingizao watakengeuka na kulipiza kisasi.
Chanzo: Mwananchi jana.

No comments: