How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Tuesday, 4 March 2008

Kwa utawala kama huu uchumi kukua ni ndoto

NCHINI China kuna mikakati na mchakato vya kweli vya kupambana na ubadhirifu na wizi wa pesa za umma. Matumizi mabaya ya ofisi za umma hayakubaliki wala kuvumilika. Kila mtu anamchunguza mwenzake kama ilivyokuwa wakati wa utawala wa awamu ya kwanza.

Kwa waliokuwa wakati wa utawala wa awamu ya kwanza watakuwa mashahidi kuwa kuwapo kwa nia na vitendo vya dhati kuzuia ubadhirifu na wizi wa mali za umma, Tanzania ilikuwa ni miongoni mwa nchi chache za kiafrika zilizoweza kutoa huduma za jamii bure kuanzia elimu, tiba na hata mikopo kwa vyama vya ushirika. Tanzania ilipaa kwenye huduma za jamii hadi kufikia kutoa elimu hata kwa watu wazima chini ya falsafa ya “Kisome chenye manufaa”

Ikumbukwe kuwa wakati ule madini kama tanzanite,migodi mipya ya Bulyanhulu, Geita, Kahama na mingine haikuwapo. Wakati ule hapakuwa na gesi ya Songo songo wala sangara wa ziwa Nyanza. Wakati ule hapakuwa na uwekezaji wa aina yoyote toka nje. Lakini pamoja na kutokuwapo haya, tuliweza kupata elimu na tiba bure.

Kwa upande wa pili, wakati ule hapakuwapo na utegemezi kwa wafadhili. Pia hapakuwa na ushufaa wa watawala kutumia magari kama mashangingi ya VX. Badala yake kulikuwa na Land Rover na Volkswagen. Nakumbuka kuna mbunge mmoja kwenye mwishoni mwa miaka ya 1970 alikuwa akitumia Volkswagen tuliyoibatiza mgongo wa chura.

Pia wakati ule hapakuwapo na tabia ya viongozi kupata mishahara zaidi ya mmoja. Badala yake kulikuwa na miiko ya uongozi ambayo kwa sasa imezikwa kutokana na watawala kupenda ukuu,makuu na kujiingiza kwenye jinai zote zinazoonyesha uroho na roho mbaya.

Nchini China kumeanzishwa utaratibu wa aina yake. Huu ni utaratibu wa kupiga marufuku kwa mtumishi au kiongozi wa umma kuwa na nyumba ndogo. Hii ilifikiwa baada ya kugundulika kuwa watu wengi waliokuwa wakifanya ubadhilifu wana utitiri wa nyumba ndogo unaowafanya waibe ili kuuridhisha.

Je, sisi kwetu hatunao watu kama hawa ambao wanafikia hata kuhonga vyeo na nyadhifa? Mimi sijui. Chunguza viongozi wetu waliomo maofisini uangalie uwezo wao kwa kuongoza na jinsi walivyofikia hapo hata bila sifa. Hapa achia mbali kesi za Dodoma za kupeana talaka.

Tukirejea China, kwa mujibu wa gazeti la ‘The Times’, kesi maarufu ya Lin Longfei katibu wa zamani wa chama cha Kikomunisti kwenye jimbo la Fujian ndiyo chanzo cha falsafa hii mpya dhidi ya ubadhilifu na nyumba ndogo.

Lin aliwakaribisha vimada wake wote 22 kwenye hafla na kuwapa zawadi kila mmoja kulingana na alivyotaka. Mwaka 2004 Lin alihukumiwa kunyongwa kutokana na kosa la ubadhirifu. Wakati China wananyonga sisi tunaambizana “Muache fulani ni mwenzetu”!

Nchi jirani ya Zambia, ambayo Rais wake wa zamani, Fredrick Chiluba, alipatikana hivi karibuni na hatia ya kuibia umma jumla ya paundi za Kiingereza milioni 23, nayo ina vituko vyake.

Kwani iligundulika kuwa Chiluba, mpenda makuu, alikuwa akitumia jumla ya paundi 600,000 (karibu zaidi ya shilingi milioni 170), kwa mwaka kununulia mavazi ilhali wananchi wake wakifa kwa utapiamlo na njaa. Chiluba aliweza kujinunulia masuti na majaketi yapatayo 206 kutoka kwa wanamitindo kwa ‘bei mbaya’ Ulaya na mashati 240 kwa kutumia pesa ya walipa kodi maskini wa Zambia!

Tukirejea kwenye suala zima la uchumi, imegundulika kuwa pamoja na chumi nyingi za nchi maskini hasa barani Afrika kuwa hoi, wezi waliomo madarakani hufanikiwa kutokabiliwa na shinikizo la wananchi kuachia madaraka.

Sababu zilizo wazi ni kwamba kuwepo kwa wananchi waishio nje ya afrika kumesababisha wezi hawa kupeta. Kwani ukiunganisha na pesa ya misaada toka kwa nchi fadhili, wananchi walioko nje ya Afrika huingiza pesa nyingi barani afrika kuliko hata wakati mwingine pesa inayoingizwa na wafadhili.

Pesa hii ambayo hutumwa na watu binafsi kwa familia zao, imesaidia sana kuwapumbaza wananchi kiasi cha kutosimama na kukabiliana na wezi walioko maofisini.

Hivyo kuna baadhi ya nchi kama Ethiopia ambayo wananchi wake wengi wamegeuka kuwa kero kwa usalama wa nchi yetu kutokana na kuingia bila hati halali, huwamotisha wananchi wake kukimbilia nchi za nje hasa ulaya na Marekani ili baadaye watume pesa nyumbani kwa ndugu zao na ndugu zao wapumbae wasidai kuubadilisha utawala mchafu.

Pia imegundulika kuwa NGO na serikali barani Afrika ndiyo asasi zinazotumia pesa nyingi kuliko wananchi. Maana NGO zimebadilika. Badala ya kuwa taasisi zisizo za kiserikali za kuwatumikia wananchi maskini zimegeuka kuwa taasisi zisizo za kiserikali za kuwatumia wananchi kama serikali.

Hivyo tukubaliane kuwa pamoja na kupigia kelele matumizi machaufu ya watawala wetu hasa kwenye magari na majumba ya thamani na ziara za mara kwa mara ughaibuni, tusisahu kuwa hivi tunavyoona ni cha mtoto.

Kuna huu upande wa Chiluba uliojificha. Hebu tazama karibu yako. Je rais au mkuu wa wilaya au mkoa wako anatinga kwenye suti kiasi gani ili kuendana na hadhi ya shangingi kama alivyowahi kusema mpumbavu mmoja aliyesoma akakosa kuelimika.

Mtazame mumewe au mkewe anatinga kwenye viwalo vya bei gani. Watazame wabunge wenu wanavaa na kula vipi? Upuuzi wote huu unatokana na pesa ya mlipa kodi maskini na kapuku wa nchi ombaomba! Je hii siyo laana na roho mbaya?


Je pesa inayoharibiwa na mafisadi aina ya Chiluba ingeweza kujenga mashule na hospitali ngapi?


Je tunao akina Lin wangapi nchini mwetu? Je hawapo? Hapa kweli kuna uchumi kukua? China ni nchi yenye uchumi unaokua kwa kiwango cha ajabu duniani. Uchumi wa China kwa miaka zaidi kumi umekuwa ukikua kwa asilimia zaidi ya kumi! Haijawahi kufikiwa na nchi yoyote. Na karibuni China inaweza kuipindua Marekani kwenye nguvu za kiuchumi. Maana tangu mwaka jana China imekuwa ndiyo nchi inayonunua bidhaa nyingi duniani nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Marekani kwa muda mrefu.

Je, wamefikaje hapo? Ni pamoja na kufanya kazi kwa bidii na kupambana na ubadhilifu vilivyo badala ya ngonjera na nifaki. China haitegemei wafadhili pamoja na kuwa na idadi kubwa ya watu duniani. Inachukia uombaomba na utegemezi wa aina yoyote.

Wachina wametumia watu wao na rasilimali zao kufikia hapo walipo.

Nasi tukitaka kufufua na kukuza uchumi wetu lazima tukubali kuchukua hatua za kweli na madhubuti za kupambana na ubadhirifu kuanzia kwa viongozi wa juu badala ya kusafishana kwa kutumia akina Takukuru.

Tusimwamini mtu hata awe rais na tuweke sheria kali kwa watakaopatikana na hatia za ubadhilifu badala ya kuunda tume za kusafishana.



Source: Tanzania Daima Machi 4, 2008.

5 comments:

Anonymous said...

Mhango unasema ukweli. Watawala wetu wanatufanya majuha kwa kutopambana vilivyo na ufisadi kwa vile ni mafisadi.
Mbona Kikwete hasemi chochote kuhusiana na list of shame?
Yapo mengi ingawa amejitahidi kumtundika msalabani Lowassa.
Naye anapaswa kuchunguzwa na kushitakiwa badala ya kumuacha awe hakimu.
Mood Gogo

Anonymous said...

Gogo,
Naungana nawe. Kikwete hafai ni msanii. Tulionywa na Nyerere tukampuuzia sasa yanatukuta.
Mwema Sadik

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Mood Gogo na Mwema Sadik nawashukuruni kwa mawazo yenu.
Tujikomboe kifikra tukizingatia ukweli bila kumuonea mtu.
Na wahusika watie akilini ushauri wa umma wanaoutawala.
Tuzidi kuwasiliana na karibuni tena na tena kwenye blog yenu.
NNMhango

Anonymous said...

Mhango usiwafundishe watu jinsi ya kuelezea kero zao. Kama matusi wanayotutukana watawala wetu huyaoni, unayoandika ni bure.
Hakuna lugha inayowafaa manyang'au hawa wanyonya damu.
Lugha waliyotumia wachangiaji juu ndiyo inayoweza kufikisha ujumbe kwa majambazi hawa waliomo madarakani.
Hivyo wape uhuru wachangiaji wako wawasulubu watawala wao wachafu.
Ngumi

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Ngumi hukunielewa vizuri. Siwezi kuwafundisha watu jinsi ya kueleza kero zao. Lakini lazima, kama mwandishi niwakumbushe umuhimu wa staha na stahamala.
Hivyo isieleweke ushauri wangu ulilenga kuwafundisha watu jinsi ya kujieleza. Isitoshe huu ni uwanja wao wa kujidai. Sitaingilia wala kuzuia ila ningeshauri sana tuzingatie mada badala ya kulumbana juu ya ni lugha gani itumike. Muhimu blog hii ni komavu na kwa ajili ya mawazo komavu.
Karibuni kuchangia.
NNMhango