The Chant of Savant

Monday 3 March 2008

Mawazo ya Ole Naiko ni ya hatari kwa taifa


GAZETI la Thisday la Februari 26, 2008 lilichapisha malalamiko ya Mkurugenzi wa Taasisi ya Uwekezaji (Tanzania Investment Centre), Emmanuel ole Naiko akidai kuwa kuanguka kwa Edward Lowassa ni mwendelezo wa usafishaji wa kikabila la Wamasai wa Monduli!

Asubuhi ya siku iliyofuata kwenye maoni ya mhariri, Gazeti la Thisday lilimkosoa Ole Naiko kwa msimamo na imani yake ya kikabila.

Kwa mtu anayejua siri ya utangamano na mshikamano wa Tanzania licha ya kushangaa na kusikitika, anaona kama anachokozwa yeye na taifa lake. Hakuna nchi inayojivunia mshikamano usioangalia makabila kama Tanzania katika Afrika.

Ingawa ukabila upo Tanzania, ni kwa kiwango cha chini na wa chini chini ikilinganishwa na nchi kama Kenya, Nigeria, Rwanda, Uganda na nchi nyingine.

Kwanza inashangaza, Ole Naiko kama amefikiria kabla ya kurusha makombora yake yanayomvua nguo na kujenga wasi wasi juu ya uelewa hata elimu yake!

Kwanini Wamasai, tena wa Monduli waanze kusafishwa leo kutoka madarakani na si jana? Mbona wakati Lowassa akiteuliwa tena dhidi ya kelele za kupinga uteuzi wake wa kuwa waziri mkuu, Ole Naiko hakujitokeza kukosoa mfumo mbovu anaoanza kuuona leo tunapoanza kuwaandama mafisadi?

Mbona tulimkubali na kumpenda shujaa Edward Sokoine ambaye kimsingi pengo lake ndilo lililowaibua kina Lowassa?

Na je, tukianza kufuatilia makabila ya watu, hao anaowatetea watanusurika? Mbona kuna uvumi kuwa mtu wake si Mmasai bali Mmeru aliyehamia?

Mawazo haya ya kikabila licha ya kuwa ya kijima, ni hatari kwa taifa ambalo kwa miongo zaidi ya mitano limekuwa likijitahidi kupambana na hisia za ukabila, ujimbo, udini na hali ya kipato cha mtu.

Kwanini Watanzania waanze kuwapiga vita Wamasai, ilhali wanaweza kuwavumilia hata Wahindi ambao wamekuwa kila mara wakihusishwa na kashfa karibu zote zihusuzo mabilioni ya wizi wa pesa ya umma?

Mbona wamewavumilia watu hawa wabaguzi wasiochanganyikana nasi, si kwa ndoa wala dini? Ole Naiko angetafuta sababu nyingine lakini si ukabila wala chuki dhidi ya Wamasai.

Isitoshe, Ole Naiko si msemaji wa Wamasai. Hivyo kama ana ndoto za kuibua chuki miongoni mwa Watanzania aonywe haraka na akiendelea ashughulikiwe. Huu nao ni ufisadi wa kikabila ambao kwa sasa unaitafuna nchi jirani ya Kenya, ambapo Rais wa sasa Mwai Kibaki anaonekana kuendelea kuwa madarakani kwa turufu ya ukabila pogo.

Kwanini Ole Naiko anataka kushabikia dhuluma na hatari inayozidi kutugharimu hapo jirani Kenya?

Au haoni rais ambaye ni mwenyekiti wa AU anavyohangaika kila uchao kusuluhisha mgogoro utokanao na hisia za ukabila uliompa kiburi Kibaki akaiba kura?

Ingawa Tanzania inanuka, hainuki ukabila zaidi ya ufisadi. Hata wezi wetu wanaotuhangaisha kila uchao, ukiwaangalia ni kutoka makabila yote na dini zote na maeneo yote ya Jamhuri.

Hivyo hoja ya ukabila na usafishaji wa Wamasai ni mfu na uchwara. Pia hoja hii inaweza kujengwa na kuaminiwa na mtu aliyefilisika kimawazo na kimsimamo, ukiachia mbali kuwa na mashiko kwa namna yoyote.

Ole Naiko, kwanini leo anajitokeza kuwa msemaji wa Lowassa ambaye hata kwenye utetezi wake kwa wapiga kura wake wa Monduli hakulitaja hili zaidi ya kudai waliomsulubu walikuwa wanataka cheo chake cha uwaziri mkuu, ingawa na hoja hii nayo ni uchwara na mfu?

Mbona Lowassa alisema: aliponzwa na wasaidizi wake, hasa Ibrahim Msabaha kwa kumpa taarifa za uongo, ingawa nayo hoja hii haina mashiko?

Je, kati ya Lowassa na Ole Naiko, nani anasema ukweli? Je, nani kamtuma Ole Naiko kumsemea Lowassa? Je, Ole Naiko anataka kutupandikizia suala jingine zito ili lituvuruge na tuache kuwaandama kina Richmonduli? Kama amelenga hili amenoa sana. Watanzania wa sasa si wale wa mwaka 47, wa kupakia kila uchafu kutoka kwa watu wachafu.

Ni nini kinamsukuma Ole Naiko kutoa madai ya ovyo na hatari kama haya? Nadhani anapaswa kuchunguzwa hata jinsi alivyofika hapo alipo.

Kwa nafasi yake ya kuwahudumia Watanzania wote kama Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji, madai yake yanamvua uhalali wa kuendelea kuwa mkurugenzi.

Leo akiguswa kwa mfano Mkurugenzi wa Tume ya Kuchunguza na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU), Edward Hosea, kutokana na alivyopindisha ukweli kwa sababu azijuazo alipoitetea Richmond, watu wa kabila lake nao waje na upuuzi kuwa anaonewa kutokana na kabila lake? Mbona alipoteuliwa hakuna aliyejitokeza kulalamika kabila lake linapendelewa?

Kama kuna mtu wa kumlaumu kutokana na anguko la Lowassa, wa kwanza ni Lowassa mwenyewe kwa kutokuwa makini na mwaminifu kwa umma.

Na wa pili ni mfumo mchafu wa kujuana na kulipana fadhila uliomuwezesha Lowassa hata Ole Naiko kufikia walipofikia kwa bahati mbaya kwa umma wanaojaribu kuuhujumu kwa kuzusha madai ya kipuuzi ya ukabila.

Tanzania inaelekea kubaya kama watu wa kariba ya Ole Naiko wanaweza kuja na madai ya kitoto kama haya. Hawa hawana tofauti na watabiri na wahubiri wanaohongwa na muathirika wamtetee kuwa atarudi kuongoza kama alivyofanya Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, wasijue kufanya hivyo ni kumdhalilisha Mwinyi na kupoteza muda.

Wanasahau kuwa mazingira ya sakata la kujiuzulu Mwinyi ni tofauti kabisa na kuachia ngazi kwa Lowassa.

Asiyekubali kushindwa si mshindani. Lowassa akubali ameanguka na hatarudi kama anavyoaminishwa na watabiri wake. Isitoshe Tanzania inao vijana wengi safi wanaoweza kuongoza nchi, si lazima awe Lowassa.

Kuna haja ya kumsaidia na kumuelimisha Ole Naiko na wale wote wenye mawazo kama yake, kama wanataka kumsaidia Lowassa basi wamwambie aeleze ukweli kuhusiana na madai ya Richmond.

Na si hayo tu. Ajibu hata tuhuma zilizomuathiri kwa Watanzania zilizotolewa na marehemu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, kuwa alikuwa na utajiri mkubwa alioupata kwa kujilimbikizia mali ambazo hawezi kuzitolea maelezo.

Hivi kweli Wamasai wangekuwa wanapigwa vita, Ole Naiko, angekuwa bado ofisini? Au amehisi kuna uwezekano wa kutimuliwa na sasa anaanza ‘ku-preempt’ ukweli huu?

Je, Ole Naiko anataka kujifichua kama mshirika mkuu wa Lowassa? Maana hata yeye kama Hosea, taasisi yake iliguswa na jinsi ilivyotoa upendeleo kwa Richmond? Je, ni kwanini walifanya hivyo? Je, ni kwa maelekezo ya Lowassa anayetetewa sasa na Ole Naiko? Kuna kitu hapa, si bure.

Tuhitimishe kwa kumshauri Ole Naiko asiendelee na madai yake. Kwani licha ya kumtia aibu, ni hatari kwake na taifa kwa ujumla.

Na ifahamike: kama ni mkakati wa kutaka kujijenga upya, basi umefeli hata kabla ya kuanza.

Maana bila ya kujibu tuhuma kuanzia zile zilizotolewa na Nyerere hadi hizi za kamati teule ya Bunge, kurudi kwa Lowassa ni ndoto.

Source: Tanzania Daima Machi 2, 2008.

5 comments:

Anonymous said...

Ole Naiko kama Lowassa anatapatapa. Kama ulivyosema, ni vizuri akachunguzwa na kuondolewa haraka kwenye wadhifa wake.
Naye ananuka rushwa ndiyo maana anaitetea. Ni stooge wa Lowassa huyu. Maana kwa maneno yake hili liko wazi kabisa.
Kikwete tuondolee mzigo huu wa Lowassa hata kama Lowassa nawe lenu moja.
Mhango nakupongeza kwa makala zako zilizokwenda shule ndugu yangu. Kaza buti kishindo tumekisikia alipogaragara Lowassa.
Kwanini humpi kipigo mfadhili wao Rostam Aziz?
Mshukie nae ingawa anaguswa guswa.
Khalfan

Anonymous said...

Khalfan umenena vyema. Inaonekana Ole Naiko ni mkia au tuseme zigo la Lowassa. Lakini wawili hawa hawatashinda. Hawa ni wezi wanaotaka kuutumia ukabila wao kama ngao dhidi ya uchafu wao unaoonekana wazi.
Mbona hatukumchukia Sokoine?
Lowassa na Ole Naiko hata wafanyeje hawawezi kukwepa wala kuukimbia uchafu wao. Lowassa alinuka tangu enzi za Nyerere.
Kilichofanyika ni kuhitimisha utabiri na ushauri wa Nyerere.
Mwandishi amejitahidi kumpa elimu ya bure. Ni tuisheni bila malipo kama anazo akili.
Ole Naiko kitoe na Lowassa wako nyie ni hasara.
Kafilie mbali. Nani awachukie wakati mlijichukia kwa uchafu wenu?
Ngongomeka Mchopeka
Kizimkazi-Pemba

Anonymous said...

Hei!
Leo naona mmeamua!
Kusema ukweli huwa sina tabia ya kuacha ujumbe kwenye uzi huu, leo sina jinsi.
Huwa nausoma uzi huu na kujiondokea nikiwaza.Leo nimewafuma mmenifuma.
Ole Naiko si wa kulaumu bali kuhurumiwa. Hawa ndiyo watawala wetu wanaotula kama dagaa!
Kama mtu mwenye cheo kama hiki anaweza kuwa na mawazo mfu kama haya hawa wanavijiji watakuwa na mawazo gani?
Kikwete haraka haraka tuondolee hii nuksi. Ondoa hiki kichefu chefu "tusikutapikie" kwa mawe haraka.
Shehe Ahmad Mussa,
Chumbe

Anonymous said...

Kumbe tuko wengi! Ole Naiko ni mshenzi. Angetetea wamasai kugeuka walinzi na kukimbia mavazi yao ningemuelewa kama anataka kuwa kiongozi wao. Hili la Lowassa ni aibu kwake. Hivi asingeuawa Sokoine, Lowassa angekuwa wapi?
Naungana na mwandishi Lowassa siyo mmasai bali mmeru aliyezamia na kujichanganya. Wasituchanganye.
Msemakweli

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Nawashukuruni Khalfan, Ngogomeka, Shehe Mussa na Msemakweli kwa mchango wenu. Zidini kutembelea blog yenu na kuacha ujumbe.
Naamini wahusika watafanyia kazi mchango wenu mzuri.
Ningeshauri tujitenge na matusi hata kama tuna hasira.
Ujumbe wenu, naamini utawafikia walengwa ambao naamini huwa wanapitia blog hii.
Karibu tena kwenye blog yenu na msisahau kuacha ujumbe kila mtembeleapo.
Nafarijika sana kuwasomeni kama mnavyonisoma.
NNMhango