Kwenye kitabu chao "The heart of the soul", Gary Zukav na Linda Francis wanasema "....safari ndefu katika maisha utakayofanya ni kutoka kichwani mwako hadi moyoni mwako" (Tafsiri yangu).
Katibu wa itikadi na uenezi wa Chama Cha Mapinduzi, Waziri na mbunge John Chiligati alikaririwa hivi karibuni akiupotosha umma kwa kudai wanasiasa wanapotosha umma na kutumia kashfa ya wizi katika akaunti ya madeni ya nje (EPA).
Aliendelea kudai kuwa wanafanya hivyo ili kumdhoofisha rais Jakaya Kikwete ambaye kimsingi anajidhoofisha mwenyewe!
Kinachotisha na kutisha ni ile hali ya Chiligati kuamua kupotosha huku akiona wenzie ndio wanapotosha! Alichofanya ni kama kumzuia mtu asivute sigara wewe ukavuta bangi!
Hebu angalia maneno yake:"Katika hali hii, CCM tunayo kila sababu ya kuamini kwamba kashfa ya EPA imeanza kutumiwa kwa malengo ya kisiasa, ya kudhoofisha kazi nzuri inayofanywa na rais katika kushughulikia ufisadi na mafisadi… na kumdhoofisha rais aonekane hajafanya jambo lolote la maana. Njama hizi siyo za kiungwana na ni mchezo mchafu," John Chiligati.
Hivi Chiligati anaishi Tanzania kweli? Je anajua anachosema na anaowaambia? Hata kama ni kutetea kitumbua, huku siyo bali kujivua nguo kiasi cha kuwafanya watu wenye akili kushuku hata uelewa wa huyu Bwana. Kama na rais Jakaya Kikwete na Chama chake, nao wataufakamia upuuzi huu, basi huku ni kufilisika alikowahi kuonya Marehemu Horrace Kolimba; aliyekuwa katibu mkuu wa chama hicho.
Chiligati anasema: kashfa ya EPA inatumika kutimiza malengo ya kisiasa. Ebo! Ukiishi kwa upanga utakufa kwa upanga. Kwani pesa iliyochotwa BoT kwenye fuko la EPA ilitumika kufanya nini zaidi ya kukamilisha malengo ya kisiasa ya Kikwete na chama chake? Kwao kuuibia umma na kufanikisha malengo yao kisiasa ni halali lakini haramu kusema :walifanya hivyo! Hiyo ndiyo kazi nzuri ya CCM na Kikwete anayotaka watanzania tujivunie na kushangilia kama yeye anayenufaika nayo?
Nani hajui kuwa CCM ni mtuhumiwa mkuu katika jinai hii ambapo kampuni lake la Deep Green Finance linatajwa sana? Yaani Chiligati bado hajui kuwa watanzania wanajua mchezo mzima na anayecheza mchezo mchafu na safi? Ajiulize kwanini serikali yenye kila zana na nyenzo za kupambana na uharifu imeshindwa kuwanasa wezi walioko nyuma ya EPA. Jibu ni rahisi. Hawakamatiki wezi wa EPA kwa sababu wao ndiyo wakamataji. Kama Chiligati atanipa sababu hata moja ya serikali na chama kusua sua na kushindwa ktk sakata la kuwakamata watuhumiwa wa EPA, niko tayari kuachana na kazi ya uchambuzi. Chiligati angekuwa anajua anachosema,angewalaumu hata wana-CCM kama akina Joseph Butiku wanaokemea kila uchao hadi kufikia kusema nchi sasa ina ombwe la uongozi na ukosefu wa watu wenye visheni na ithibati.
Yaani Chiligati anadhani watu bado ni mbumbumbu kiasi hiki! Hebu angalia maneno yake mengine:"Ni lazima wananchi wakatae njama na hila hizi zinazoendeshwa na baadhi ya wanasiasa wa vyama vya upinzani," alisisitiza Chiligati.
Upuuzi. Hivi akina Butiku nao ni wapinzani? Hata yeye Chiligati kama siyo tumbo, haamini anayosema. Huu ndio uoza na ufisadi mkubwa wa CCM-kuhadaana na kujihadaa.
Kunya anye kuku asingiziwe bata! Chiligati anasema wapinzani wanataka kumkatisha tamaa na kukwamisha kazi nzuri anayofanya Kikwete! Kazi gani nzuri? Kuachia fedha na raslimali vya umma vikiibiwa na mafisi kila uchao! Namtaka Chiligati anionyeshe kazi nzuri aliyofanya Kikwete, nitamuomba msamaha Kikwete hata yeye Chiligati tena ukurasa wa mbele.Wakati akifanya hivyo ajikumbushe ahadi alizotoa bosi wake zikafanya tumchafue.
Anasema CCM wanaamini kinachofanyika ni njama ya wanasiasa na vyama vyao kumchafua Kikwete! Hakuna aliyemchafua Kikwete kama Kikwete mwenyewe na chama chake na wapambe wake. Kikwete hana usafi hata chembe. Alichafuka zamani kiasi cha kunuka. Chiligati inabidi aukubali ukweli huu hata kama ni shubiri kumeza.
Kinachochekesha sana ni ile hali ya Chiligati eti kuonya wanasiasa waache mchezo huu mchafu. Anayepaswa kuonywa na kukemewa ni yeye Chiligati na chama chake kwa kuhadaa umma na kulinda uchafu. Kinachopaswa kufanywa na CCM na Kikwete hata Chiligati siyo kuonya wala kutishana bali kujisafisha haraka iwezekanavyo.Wana bahati wananchi hawajawatokea mitaani kudai haki zao zinazochezewa chini ya Chama kilichofilisika kwa kila namna.
Tumpe marejeo Chiligati. Anaweza kuueleza umma ni kwanini rais Kikwete hajawahi kukanusha wala kutolea maelezo ya shutuma kuwa ni fisadi mkubwa yaliyotolewa na wapinzani mwaka jana chini ya kinachojulikana kama List of Shame.
Si Kikwete peke yake. Hata CCM imekuwa ikizigeuza zile shutuma-- zinazoanza kuonekana kuwa kweli-- kuwa suala la kisiasa badala ya kisheria! Hivi Chiligati anaweza kunipa sababu za ni kwanini CCM imeshindwa hata kuwafukuza au kuwaadhibu hata wabunge wake na makada wake wanaokabiliwa na tuhuma chafu kama kughushi vyeti, kutoa rushwa, kuiba pesa ya umma. Hebu nimpe majina. Edward Lowassa, Nazir Karamagi, Ibrahim Msabaha, Rostam Aziz, Gray Mgonja na wengine ni makada wazuri wa CCM. Wameguswa wazi wazi kwenye kashfa ya Richmond hadi wakafukuzwa kwenye cabinet. Je CCM na Kikwete kama siyo washirika wao wamewachukulia hatua gani wahusika kichama?
Samuel Mchele Chitaliro (Busega-CCM), Gozibert Begumisa Blandes (Karagwe-CCM), Michael Lekule Laizer ( Longido-CCM) na Elisa David Mollel ( Arumeru Magharibi-CCM). Hawa wabunge pamoja na kubainika kwa jinai waliyotenda, bado wako bungeni tena wakilindwa na chama! Kinachofanyika ni kupiga dana dana ili muda uende wamalize ngwe zao au umma usahau. Kuna uchafu kama huu?
Makala hii haiwezi bila kumtaja mwenyekiti mstaafu wa chama, rais mstaafu, Benjamin Mkapa na mkewe na watoto hata marafiki wanaotuhumiwa kujipatia mabilioni ya shilingi kiharifu kwa kutumia ofisi ya rais. Wana makampuni. Ni ANBEN, Tanpower, na Fosnik kwa uchache. CCM ingekuwa na mwelekeo na udhu angalau ingewaonya hata kuwashughulikia. Ndiyo kila uchao wanampongeza na kuzidi kumlamba miguu! Chiligati tueleze CCM na Kikwete wamewachukulia hatua gani waharifu hawa wanaojificha nyuma ya madaraka? Kuna uchafu kama huu? Kuna ufisadi na jinai kama hii ndugu Chiligati? Yaani tunaanza kubariki na kukubali hata ufisadi wa kimawazo! Jamii iliyoharibikiwa ni ile ambayo hutumia tumbo kufikiri badala ya ubongo. Hii ni jamii ya hayawani wakiongozwa na kuku.
Tumalizie na kituko cha Chiligati na CCM yake. Eti wanasema mafisadi walaaniwe na kurejesha pesa waliyoiba EPA! Wakati kidole chao kimoja cha shahada kikiwasota mafisadi, vinne vyote vilivyobakia hata vya miguuni vinaielekea CCM na Kikwete na Chiligati. Ni mafisadi walaaniwe na kurejesha au mlaaniwe na mrejeshe? Naomba kutoa hoja nikiamini Chiligati na CCM hata Kikwete watanipa maelezo kama wanataka umma uwaelewe. Hakika darasa analoweza kufanya na kutoa Chiligati hata Kikwete na CCM ni safari ya kuanzia vichwani mwao hadi nyoyoni mwao.
No comments:
Post a Comment