The Chant of Savant

Thursday 6 March 2008

Kijiwe na mauza uza ya Mkuu

Juzi baada ya Mkuu kuja na mvinyo wa zamani kwenye chupa mpya, na Kijiwe kimefanya mabadiliko ya uongozi. Hii ni baada ya waziri mkuu wa Kijiwe, Muathirika Mbwamwitu kugundulika kushirikiana na yule Kanji tuliyemnyuka siku zilizopita kuiba pesa ya Kijiwe na kununua kahawa mbovu.

Kwanza Kijiwe kilivyomsulubu mshirika wangu sina hamu. Yaani utadhani Bwana Yesu! Maana kabla ya kuzama jua walimchukua wakamleta mbele ya makutano wakamfungulia mashtaka ya ufisadi kwenye kijiwe. Wanakijwe walioonekana kumchukia kutokana na majivuno yake mara walihanikiza’ "Asulubiwe, atimuliwe,, adhalilishwe. Ndipo yule pilato aitwaye 666 akatoa amri askari wa Kijiwe wamshushe toka kwenye ukuu. Akashushwa toka kwenye ukuu huku mshirika wake wa bedroom akilia.

Ufisadi na mafisadi hawapo huko tu. Nasi kwenye Kijiwe tunao na hatuwalei, kuwalinda wala kuwaficha. Tunawapa disipilini kama kawa.


Wasomaji kwanza msihofu rais bado ni mimi Mpayuakaji Msemahovyo bingwa wa kucheka na kutabasamu. Mna habari, pamoja na kufanya badiliko hili, wanakijiwe wanazidi kunizodoa kuwa wanahisi nilishirikiana na Mbwamwitu? Eti wamekumbuka nilivyowatembezea takrima ya vikombe vya kahawa na kashata wakati hata kibarua sina! Hii ni wakati wa kunichagua.

Kijiwe kiliunda tume ya kuchunguza ujambazi huu chini ya mwanakijiwe maarufu kama Mwakapende ambaye kusema ukweli alimvua nguo Mbwamwitu sina hamu. Hata hivyo wanakijiwe wanasema wananihesabia siku. Wanataka nami nijiwajibishe kabla hawajanitolea uvivu! Walevi hawa hawana adabu kabisa. Wamelewa kama mimi.

Pamoja na kumsimamisha ulaji Mbwamwitu, niseme ukweli sina sura mpya za watu wanaofaa kutumika kwenye serikali mpya ya Kijiwe.

Kwa mfano yupo huyu Enderea Chenga. Kijamaa kijizi sina hamu. Eti nilipokipendekeza kiendelee kuwa kwenye baraza la Kijiwe nusu watu wazimie kwa mstuko. Si ndipo bomu liliponilipukia kumbe letu moja!

Mie nilikuwa nimewazidi kete kweli kweli. Niliamua nimtoe sadaka Mbwamwitu ili mambo yaishe kumbe naota! Mungu mwenyewe ndiye ataninusuru na balaa hili ambalo nikiri lilisababishwa na upofu, tamaa ya ukuu, na usanii.

Tofauti na Mkuu wa sehemu sehemu ambaye wanakaya wake wanaonekana kuuingia mkenge wake, wangu wameshupaa kiasi cha pressure ya shinikizo la damu kunipanda. Mara nihisi BP.Mara SHELL. Na hata Caltex!

Lazima kwanza nikiri. Mzee Ndomo ambaye wanakijiwe walizoea kumuita Kingungo Mwehu kutokana na uzee na kupayuka hovyo hovyo, Mzee Maneno maarufu kama Mramba kashata na wengine waliozoea kuitwa wanasesere wangu au vinyago vya mpapure nimewapiga chini ili kuwazuga wanakijiwe.

Kwanza niseme tena kwa sauti ya chini ili wanakijiwe wasisikie. Nilichofanya ni kuwapuga lakini tunajuana nyuma ya pazia. Si unajua watoto wa Bongo!



Kuna mpango mwingine mchafu unaendeshwa na baadhi ya wanakijiwe. Eti wanataka nivunje chama changu cha UNM au Ulaji, Ngonjera na Mapozi. Eti wamekibatiza jina la Ufisadi, Ngonjera na Madhambi! Hawana adabu kabisa. Si juzi nilimsikia mbea mmoja eti naye mwandishi wa habari. Anasema Kijiwe chetu ni CCM yaani Chui, chatu na Mafisi! Halafu anasema eti kitendo changu cha kumtoa sadaka Mbwamwitu ni sawa na kumsulubisha Yuda mbele ya Lusifa akichekacheka na kuwa hakimu! Mshenzi mkubwa. Alitaka nimtoe kafara mshirika wangu wa BD! Yaani nimtoe yeye nijiache kwenye baridi! Thubutu yako!

Hawa wanadhani bila chama Kijiwe kitaongozeka? Mbona nasikia akina Msomi, Mgosi Machungi na Makengeza eti nao wana vyama vyao vya mfukoni. Mbona wao nao wanawaburuza wanachama wao? Sijawahi kusikia wamewaita kuwaelezea wanavyotumia ruzuku tunayowapa kutokana na kuuza kahawa?

Kwanza najua siwezi kuangushwa na watu wenye njaa kama wao. Juzi walinikuna saaana. Eti Mbwamwitu alipopatikana na hatia yake kiasi cha kudondoka, badala ya kushinikiza wote tuwajibike, wakawa wanashabikia nani nitamtema na nani nitamrudisha! Hivi hawajui kuwa Kambale wote wana masharubu! Hawajui kuwa hata anayeonekana kusimama aliishaanguka zamani?

Mie baada ya kuona wananiandama nilitia mkwara: atakayeendelea kuchonga nawanyang’anya malipo ya kahawa za bure na nauli za dala dala wanazopewa na Kijiwe.

Kwanza niliwapiga mkwara kuwa tangu sasa wachague kuhudhuria vikao vya Kijiwe au wafanye umachinga wa kuuza chupi na pipi mikononi.


Mijitu mingine eti inataka nitangaze mali zangu na watu wangu! Yaani inaniona mie juha nijivue nguo mwenyewe! Nasema sitangazi na atakayeendelea kushikilia hili naziba masikio tuone itakuwaje.

Kwanza mali ya umma wa wanakijiwe inawahusu nini? Hivi hii minoko haijui mali ya umma ni ya kuuma tena kwa uma tena ukishirikiana na umma wa washikaji wako hata watoto wako? Mbona yenyewe inawaibia washirika wao wa bedroom? We ngoja tu. Nitaiuliza hii mizabazabina inapopata uchache wa kupatia moja joto na moja baridi au ya kuzipa nyumba ndogo zao?

Lakini mijamaa ina hoja. Kama siyo nayo kuridhika na usanii wangu, ina kila sababu ya kunipiga chini. Ila walevi nawajua. Watashikia bango jambo. Baada ya muda kila mlevi anajichimbia kwenye upuuzi na umachinga wake Mkuu wa Kijiwe nazidi kutesa.

Tokana na hawa makenge kustukia dili la kununua kahawa mbovu la Mbwamwitu, inabidi nijiandae kufunika lile dili jingine la kulangua kashata na kuiba pesa kwenye akiba ya Kijiwe.

Mungu naapa wakistukia hili nimekwisha. Maana tuliponyoa njuluku nyingi. Na wangejua kuwa Kijiwe sasa hivi ni maskini wa kutupa! Ee Mungu, sijui siku wakijua itakuwaje? Kwa vile muda wa kuwa Mkuu wa Kijiwe umebakia kidogo, nitazidi kujipanga na kuwapanga vizuri angalau nimalize ngwe hii salama.

Kuna hili la kushikilia eti washikaji zangu pamoja na Mbwamwitu tuwashitaki! Mwe! Nao wakichoka ubangusilo wakaamua kunitaja itakuwaje? Hapa lazima niwapige dana dana hadi wasahau au nimalize ngwe yangu niishie na mishiko yangu. Ila nayo hii choo siku hizi. Maana anaweza kuja nirithi fyatu akanifanyia kweli.

Sasa hivi ninawabana akina Kanji na Mbwa mwitu na mipapure yao warudishe njuluku za kijiwe kisiri siri. Wapo machizi wanasema huu nao ni wizi. Kwanini warejeshe bila kwenda kwa pilato?

Hawajui tuliponyoa pamoja na isitoshe wanaorudisha siyo sisi wazito bali wale vidagaa wepesi ambao tuliwashikisha kimisheni kufanikisha misheni zetu. Hata Mbwa mwitu kwa taarifa yenu hajaondoka. Ameondoka ofisini lakini ulaji kama kawa. Si unajua katiba feki viraka ya Kijiwe. Unaibia Kijiwe halafu unamwagiwa mamilioni ya Kijiwe kwa kustaafu kuwaibia. Ukiugua na mshirika wako huna haja ya kutumia ile pesa uliyowaponyoa. Kijiwe tena kinawaibia walevi na kukugharimia hata kupima mafua kwenye hospitali aghali. Sisi hatulazwi watatu kule Mwanamanyala na Kemete wala Ilaila. Upo hapo? Walevi ndiyo waliwao.


Kuna kamchezo kengine nimeanzisha. Nako ni kujifanya nawasikiliza walevi ilhali nawadharau na kuwapuuzia. Wanasema hata kuandika mengi. Mie natabasamu na kucheka cheka hata kutoa makaripio kwa wenzangu. Lakini vitendo usiniulize. Mie sikuchaguliwa kutenda bali kuhomoa. Wao walikula takrima yangu nasi tunakula mali zao na kunywa jasho na damu yao. upo hapo mlevi? Acha ulevi tutawamaliza.

We simba we. Unaninyemelea eti unile kama ninavyowala wanakijiwe!

Aaa kumbe naota!

Source: Tanzania Daima Machi 5, 2008.

No comments: