How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Wednesday, 26 March 2008

Mpayukaji nakwenda Butiama kumwambia Mwalimu hivi


MAMA Kidume jana kanipa taabu kweli. Analalamika nafuja pesa ya familia ipatikanayo kwa dhiki kukamilisha mpango wangu kabambe. Nakuibia kidogo. Ngoja niseme kwa sauti ya chini CCM wasinisikie wakadhani nakwenda kuwachongea kwa Mwalimu. Baada ya kuibiwa nyuzi kuwa CCM watakutana Butiama kufanya vikao vya Halmashauri Kubwa na Kamati Kubwa, nimeamua niende huko huko ili kijulikane. Siendi kuwachongea kwa wapenzi wa chama kama kina Butuku. Wanajua madudu yote yanayofanyika. Wamesema hadi makoo yamewakauka. Sijui watafanya nini kuona mpendwa wetu na wao marehemu Baba wa Taifa anafanyiwa unyama huu? Nilipanga kujinyonga nikagundua siyo jibu. Kimsingi nakwenda kuwaambia waheshimiwa wasio heshima: wamwambie Mwalimu yafuatayo. Nataka nisisikie gazetini wala kuona radioni. Nataka nishuhudie mwenyewe ili nije niwajuze wana Kijiwe chetu. Kwanza wamwambie Mwalimu kuwa kazi yao ya kuyafufua yote mema aliyopigania na kuyafia imekaribia kukamilika. Najua Mwalimu ni mwelewa atawakubalia hasa wakimpa sababu zenye mashiko. Naenda kuwatambulisha wafanyabiashara maarufu wanaopenda chama chake ambao wako tayari kukichangia hata kwenye uchaguzi kinapoonekana kuelemewa na wapingaji hasa kwa njia ya takrima. Nimeishawasiliana na mgosi wa Nk’oogwe amkaribishe Mjasiriamali, mkewe mama pochi, mwanae anayeonekana kurithi damu ya ujasiriamali ya baba na mama na rafiki yao mkubwa Jona. Nakwenda kuzitambulisha rasmi kwa Mwalimu ANBEN, Tanpower, Fosnik, Kagoda na Deep Green Finance. Nakwenda kumuonyesha Mwalimu kuwa uchumi wa nchi yake umekua kiasi cha kuwa na mashangingi kwa kila mjumbe mkubwa na mdogo. Pia nakwenda kutoa taarifa rasmi kuwa hata wafanyabiashara sasa wanakipenda chama chake kiasi cha kukipaisha kama dege la Lowassa. Pia nakwenda kuwasilisha ripoti ya kazi nzuri iliyofanywa na Benki Kuu chini ya mpango wa EPA au Economic Profligacy for Authorized-corsairs, ambapo karibu madeni yote ya nje ya benki na sheria yamelipwa bila wasi wasi. Pia sitasahau kumpa taarifa jinsi rafiki yake toka umasaini Ole Mmeru Ewassa, aliyemshauri asipoteze muda kujipaka uchafu kuwania uongozi alivyochafuka na kupigwa kibuti, tena kwa aibu na kibuhuti huku Bi mkubwa wake akimwaga michozi utadhani darling wake alikuwa ndiyo ananyotoka roho! Hapa lazima nimshike mkono Daktari Mwakiembe na kumtambulisha kwa Mwalimu. Najua atafurahi na kumpa nasaha moja, mbili. Sitaacha kumpa taarifa, hata kama ni za aibu, kuwa kile kizee kilichojidanganya kingevaa viatu vyake chamani kiliboa na kuanza kuropoka na kupayuka kama mimi kiasi cha umma kukizomea. Nitamueleza jinsi zile mvi za kile kibabu zilivyoishia kuwa hovyo. Hayo tuyaache. Ni yangu na Mwalimu. Pia nitautambulisha rasmi ule mradi wa bi mkubwa wa hiki kibabu pale Ubungo kituo kikuu cha mabasi. Pia nitampa Mwalimu habari njema kuwa kwa sasa nchi yake inajiandaa kutoa mabilionea kwenye jarida maarufu la Forbes watakaopambana na akina Warren G Buffet Carlos Salem na Bill Gates. Kwa mara ya kwanza Bongo itatoa bilionea wa kwanza mwanamke, Bi Nonihino Clean Ben wa Makapi. Kitu kingine nitamjulisha Mwalimu kuwa maadili ya uongozi siku hizi yamerejerewa vilivyo. Viongozi wana maadili na madili kweli kweli. Wakifanya uchafu wanasafishwa na TAKUKURU ili wasichafuke na kukiuka miiko ya uongozi. Hapa nitampa salamu za rafiki yake Ole Mmeru Ewassa na yaliyomfika alipopuuza ushauri na utabiri wake. Kadhalika nitampa taarifa ya mafanikio ya Net Group ambapo tumefanikiwa kupandisha bei ya umeme kwa zaidi ya asilimia 240 ili kuondoa tabia ya watu kupenda starehe za kutumia umeme hovyo. Pia nitamtaarifu Mwalimu kuwa chama chake kimeanzisha utaratibu wa kisayansi na kiteknolojia wa kutumia mitandao badala ya matawi ya chama ambayo ni rahisi kukatika hasa kutokana na ukame. Nitawatambulisha wabunifu wa mitandao ya kisasa katika chama ambayo imeanza kuleta matunda kwa kushindana kiasi cha kukipaisha chama. Kitu kingine nitakachomwambia Mwalimu ni suala zima la muafaka kule visiwani. Nitamtaarifu: ule muafaka aliodhani ungekuwa ni baina ya vyama umeboreka kiasi cha kugeuka kuwa suala la viongozi wa vyama. Juzi nilimuona jamaa mwenye midevu kama Osa… sorry Mpayukaji akicheka na mjomba’ake Mgosi tuliyedhani walikuwa maadui kumbe wa ubani! Pia nitampa taarifa Mwalimu kuwa siku hizi chama kimeanza kuzingatia urithi hasa wa nasaba. Kimegundua kuwa kumbe alikosea kuwazuia watoto wake na mkewe kushika nyadhifa chamani. Kufanya hivyo kulikinyima chama damu safi kama yake. Hivyo siku hizi ruksa kwa yeyote kugombea na kushika madaraka chamani bila kujali ni mke au mtoto wa mwenyekiti au rais. Hihuu! Atafurahi najua akisikia hili. Kitu kingine nitakachomwambia Mwalimu ni kuzuka kwa imani ndani ya nchi na chama, hasa ya kuabudiwa pesa na walio nazo. Kwani wataalamu chini ya ugonjwa uitwao metastasis kitaalamu, wamegundua kuwa bila pesa hakuna madaraka na bila madaraka hakuna pesa. Hivyo kuepuka nchi kusikinika, tumeanzisha ibada za namna hii ili kukuza uchumi na kuwa na viongozi wajasiriamali. Pia nitamfahamisha kuwa siku hizi, ili kukuza uchumi, ni lazima kufanyia biashara Ikulu. Hii ni kutaka uchumi uendeshe nchi badala ya siasa. Nitamkosoa kwa kushindwa kuchukua mikopo ya mamilioni ya dola alivyokuwa madarakani. Maana kutofanya hivyo kumefanya aonekane mchovu ilhali kijana wake sasa ana majumba na miradi minono. Ahitaji kujengewa kibanda kama cha Mwalimu na jeshi wala polisi. Akitaka anaweza kupigwa tafu na mkewe au wafanyabiashara marafiki zake. Pia nitamwambia jinsi wachonga maneno na peni walivyozibuka. Nitamwambia walivyoshika bango eti kijana wake Ben afikishwe kwa pilato wasijue ujasiriamali ndiyo siasa za kisasa za kimataifa! Walipozidi mkuu aliwaonya waache umbea na kutishia amani na mshikamano wa taifa kwa kutaka kuwabughudhi wakubwa wanapokuwa wanafaidi matunda ya kustaafu. Enhee! Kitu kingine. Nitamwambia Mwalimu jinsi watawala wetu wanavyojua kuchapa kazi na kuchangamkia tenda. Nitampa kisa cha lijamaa Nshomile lilivyochangamkia tenda hata kwenye hoteli kule kwa Kwini. Jamaa lilikuwa shapu na tayari kuwafuata wawekezaji hata kule Calgary, London na hotelini! Mwisho nitamfahamisha Mwalimu jinsi yale madini aliyokuwa ametunza kwa ajili ya vizazi vijavyo yanavyoingiza mabilioni baada ya vizazi vijavyo kuja kwa kasi mpya ari mpya na nguvu mpya. Madini haya yameifanya nchi kuwa na matajiri wa kutosha na kutisha hata kuchusha kiasi cha kuita hata wengine waje kutoka India wakiwa maskini lakini wayatumie kuwa mabilionia na kuiletea nchi sifa. Naamini atafurahia mafanikio tuliyopata kwenye EPA na miradi mingine kabambe. Na mwisho nitampa hongera kwa kuona mbali hasa pale aliposema tunapochagua rais tusifanye hivyo kama tunachagua mchumba. Tumeishaona na kuelewa alichomaanisha. Sasa bila kuwachosha, ni kwamba mama Kidume hataki kusikia nasafiri. Kwanza anahofia nitapata fursa ya kutanua na ‘nyumba ntobhu’ zangu ukiachia mbali kufuja pesa. Mwanamke kidhabu huyu! Yaani anajua pesa ya kusafiria nimepewa hisani na rafiki yangu Kanji lakini bado anashupalia utadhani nimechomoa kwenye akiba yake ya chakula! Inaonekana mama huyu hajui jinsi siasa za kisasa zinavyofanywa. Anataka kila siku nikae Bongo kwenye joto na tishio la migawo mwishowe mandata wanitokee wanikate mitama. Ashindwe na washindwe na kulegea. Naona kichaa mwenyewe mshirika wa bedroom, Mama Kidume, anakuja akiwa amekunja uso. Wacha nikitoe asije akanivisha gagulo na kunipigisha deki.

mpayukaji@yahoo.com


source:Tanzania Daima, Machi 25, 2008

No comments: