How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Monday 3 March 2008

Lowassa kujilinganisha na Mwinyi ni kumdhalilisha

JAPO tumekuwa na mazoea ya kipuuzi ya kuwaamini waganga njaa tunaowapa vyeo vikubwa kama mtabiri maarufu au dokta fulani wakati hata darasa la saba walimaliza kwa taabu, tusifanye kosa kuruhusu wachumia tumbo hawa watuelekeze la kufanya tunapokuwa na matatizo makubwa ya kitaifa.

Juzi, nilishangaa kuona kauli babaishi na okotezi za anayeitwa mtabiri mkuu Afrika Mashariki na Kati, Sheikh Yahaya Hussein, kuhusu kuja kurejea tena kwa Edward Lowassa kwenye hatamu za uongozi!

Kwanza siamini utabiri, hasa unaofanywa na binadamu. Nieleze wazi kabisa kuwa hakuna binadamu chini ya jua anayeweza kutabiri kitu chochote. Hata watabiri wa hali ya hewa huwa wanatumia neno ‘approximately’, ‘likely’ na kadhalika. Maana hawana uhakika na wanachotabiri.

Kwa mtu mwenye kujikumbusha matukio, atakubaliana nami kuwa kipindi fulani Sheikh Yahaya Hussein aliteuliwa na Mufti wa zamani, Sheikh Mkuu Hemedi bin Jumaa, ambaye sasa ni marehemu, kuwa Mwenyekiti wa Idara ya Habari ya Bakwata.

Baada ya kuteuliwa akiwa amekuwa na mkwaruzano na Bakwata kwa muda mrefu, Hussein alifurahi na kuamua kumtumikia hasimu wake aliyedhani kageuka rafiki.

Baada ya muda Mufti alimtimua Sheikh Yahaya. Mie binafsi nilipata bahati ya kwenda kumhoji. Nilimpa sifa yake aipendayo ya mtabiri maarufu Afrika Mashariki na Kati. Alifurahi sana hata kunisifia.

Nilipomgeuzia kibao juu ya ni kwanini kama yeye kweli ni mtabiri maarufu Afrika Mashariki na Kati, alishindwa kutabiri kuwa Sheikh Mkuu angemtimua, aliishia kunimwagia mvua ya matusi, nami nikaamua kuaga toka kwenye mkutano huo baada ya kupata nilichokuwa nataka kukipata.

Tukirejea kwenye mada ya leo kuwa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa alikaririwa hivi karibuni na vyombo vya habari akijilisha pepo kwa kujilinganisha na Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, akiwa na maana ya kujenga picha kuwa kuna siku atarudi, licha ya kumdhalilisha Mwinyi, asahau.

Wakati Mwinyi akiwajibika kwa makosa ya mauaji huko Kanda ya Ziwa, ilijulikana kuwa yalifanywa na wengine chini ya wizara yake. Pia ifahamike kuwa, Mwinyi hakuwa na tuhuma yoyote ya ufisadi zaidi ya kuwajibika kutokana na makosa yaliyofanywa na watu wa wizara yake.

Hivyo, muda na mazingira ya kujiuzulu kwa Mwinyi ni tofauti kabisa. Kwanza Mwinyi hakujiuzulu baada ya kutajwa katika kashfa kama ilivyokuwa kwa Lowassa.

Pia kuibuka upya kwa Mwinyi hakukuchangiwa na watabiri kama Lowassa anavyoanza kutabiriwa sasa kuwa kuna siku ataibuka na kuwa kiongozi tena. Hawezi kwa kuzingatia uzito wa yaliyomsababishia kuachia ngazi. Na si hilo tu, hata yaliyokuwa yamesemwa na gwiji wa siasa za nchi hii, Mwl. Julius Kambarage Nyerere.

Japo Lowassa kama binadamu yeyote ana haki ya kujitetea, njia anazotumia za kuongopa si sahihi na hatafika wala kufanikiwa.

Kwa mfano Mwl. Nyerere alimrushia kombora miaka zaidi ya kumi iliyopita kuwa alikuwa kajilimbikizia mali nyingi. Hadi leo hajawahi kujibu tuhuma hizi wala kuweka wazi mali zake!

Hata ukiangalia kashfa iliyomuangusha inahusiana na hizo hizo mali. Hapa tunataka kumdanganya na kumpumbaza nani?

Anachopaswa kuelewa na kukubali ni kujilaumu kwa matendo na historia yake.

Pili, kuelewa kuwa mazingira ya wakati ule wa kina Mwiniyi ni tofauti kabisa na sasa. Pia aelewe kuwa jani kudondoka toka kwenye shina na kurejea si rahisi abadan.

Ndiyo anapaswa aelewe watabiri ni waganga wa kienyeji ambao mara nyingi riziki zao hutegemea kuwadanganya watu, tena wenye matatizo kama yeye. Wanachoweza kumfanyia ni kula pesa yake na kumpa imani na matumaini, vitu visivyo na msaada huko tuendako.

Arejee watu wengi walivyoishia kuwa maskini baada ya pesa zao kuliwa na waganga hawa hawa waliowatoa pesa wakiwaaminisha kuwapa dawa za kupata utajiri wasiweze.

Watabiri wanaweza kutabiri lolote. Kama wangekuwa mahiri wa kutabiri Tsunami na majanga mengine yasingeteketeza watu.

Kimsingi anachoweza kujivunia Lowassa ni kumuokoa kwa muda rafiki yake Kikwete. Na kama anadhani anaweza kurejea kwa kuutumia ushawishi hasi kwa sasa na madaraka yaliyoko tafarani ya Kikwete atakuwa anakosea kabisa.

Hebu kwa mfano amuulize sheikh wake huyo mtabiri maarufu, ni nani atatawala baada ya Rais Kikwete? Hawezi kujua. Maana siasa za sasa si za kurithishana kama kule tulikotoka.

Mimi na wachambuzi wengine si watabiri. Tulionya kuwa CCM ikiendelea kujichimbia kwenye ufisadi na kukosa uongozi wenye visheni itaumia. Sasa iko wapi CCM? Hata kama bado inashika dola, inaliendesha kwa kusuasua na mizengwe vitu ambavyo tuendako vitaitokea puani kama ilivyotokea kwa KANU kule Kenya.

Kama Sheikh Yahaya mwaka 2002 angeulizwa na Daniel arap Moi juu ya ‘probability’ ya kushinda kwa mgombea wake, Uhuru Kenyatta asingesita kusema angeshinda ingawa matokeo hayakuwa hivyo.

Akina Adolf Hitler, Benito Musolini na Idi Amin waliteketeza wengi kwa kudanganywa na watabiri. Na isitoshe kuwategemea watabiri ni upofu na upogo visivyo vya kawaida. Maana watabiri ni wafanyabiashara ya kutafuta pesa kama wengine wote.

Kimsingi Lowassa anajitahidi kuzidi kujichanganya kiasi cha kuitia matatani serikali ya rafiki yake. Hebu angalia maneno yake aliyosema juzi juzi huko Monduli:

“Mimi sikuwa mtu wa kukaa ofisini na kupokea taarifa, bali nilikuwa nafuatilia kwa ukaribu na kwa umakini taarifa za watendaji wangu, ambao kuwaamini kwangu ndiko kulikoniponza.”

Lowassa hapa anadanganya. Angekuwa mfuatiliaji asingedanganywa kama anavyotaka tuamini. Wangemdanganya vipi wakati yeye ndiye alikuwa anawashinikiza kina bangusilo Ibrahim Msabaha waipe upendeleo Richmond?

Angalia uongo mwingine: “Baada ya kugundua kuna matatizo kwa watendaji wangu katika kulishughulikia suala la Richmond, niliamua kuachia ngazi kwa moyo mweupe bila kushinikizwa… nawaombeni wapiga kura wangu mnielewe hivyo.”

Kwa mtu anayejua kilichotokea, Lowassa kusema aliamua kuachia ngazi ni uongo wa mchana. Alifukuzwa na Kamati Teule ya Bunge.

Anaposema aliachia kwa moyo mweupe, maneno ya kulalamika kwenye hotuba yake bungeni wakati akitimuliwa yalikuwa ya nini? Hebu tujikumbushe maneno yake: “Lakini la pili, nimpongeze Dk. Harrison Mkwakyembe, Mwenyekiti wa Kamati Teule kwa kuwasilisha kwa mbwembwe nyingi sana taarifa yake, mbwembwe zilikuwa nzuri kweli.” Huyu anakejeli tume. Anaonyesha alivyochanganyikiwa na ripoti ya tume.

Mwisho, hebu angalia maneno mengine ya mtu mwenye moyo ‘mweupe’: “Mheshimiwa Spika, wewe ni mwanasheria, unafahamu suala la ‘Natural Justice’. Kwamba Kamati Teule imesikiliza watu wengine wote pamoja na wanaoita minong'ono ya mitaani, wamesafiri mpaka Marekani kutafuta mashahidi, lakini mimi ambaye ni mmoja kati ya watuhumiwa mle, hawakunihoji hata siku moja.”

Kwa hoja hii, ningekuwa Lowassa nisingekubali kuachia ngazi maana ningesimama na kuonyesha nilivyoonewa badala ya kuanza sasa kulalamika.

Anachopaswa kufanya Lowassa ni kukumbuka kuwa yeye mtenda anaweza kusahau, lakini si sisi watendewa.

Kuna haja ya walio karibu na Lowassa kumshauri. Kama anataka mambo yaishe na arejee kwa kishindo kama anavyoaminishwa na Sheikh Yahaya, aweke mambo hadharani bila kujali kama rafiki yake ataumia au kulipia.

Pia asitarajie ya Jacob Zuma kule Afrika Kusini. Mzigo wake ulikuwa mzito sana na alikuwa amechafuka vibaya sana. Arejee umma alioamini alikuwa akiuongoza na kuutumikia ulivyoshangilia anguko lake.

Nihitimishe kwa kumtaka Lowassa asijilingashe na mzee Mwinyi kwani ni kumkosea adabu mzee wetu.



Source: Tanzania Daima Machi 2, 2008.

1 comment:

Unknown said...

Assalaam Alaykum mswahili mwenzangu(kwa maana ya azungumzae na kukiandika Kiswahili vilivyo)!

Sina taaliki juu ya uliyoyajadili, bali katika neno lako la makaribisho niruhusu kusahihisha kidogo kiingereza.
Badala ya sentesi kuwa: "Writing and reading are to different processes but which share the same goal-to educate, communicate and entertain." kama ulivyoiandika, ilistahiki liwe neno "two" badala ya "to" yaani ingesomeka:"Writing and reading are two different processes but which share the same goal-to educate, communicate and entertain."
Maneno "two" na "to" yana sauti moja, lakini maumbo na maana tofauti.

Nduguyo,
Razini wa Urazini