How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Wednesday, 16 April 2008

Hivi Yuda na Pilato nani hakuwa na dhambi?

BAADA ya jamaa mwenye majina yaliyopinda pinda kukiri juzi kuwa lisirikali limeshindwa kuwakamata na kuwasulubu vyangudoa na majambazi wa EPA na Richmond eti kwa vile wanaweza kulipua linchi, Kijiwe kimekuja na kauli rasmi ya kulaani upuuzi huu.

Mkuu sasa si siri amechoka, amechanganyikiwa. Hata huyu wa Kupinda naye choka, tena mapema. Hoja hii imeletwa na Mgosi Machungi baada ya kushuhudia matusi ya Butiama asiamini. Mgosi akiwa anamalizia kipisi chake cha bangi, analianzisha.

“Wagosi mnajua kwanini nimeamua kuvuta bangi?” Kabla ya kuendelea tunatikisa vichwa kuonyesha kutojua.

Anakwanyua mic. “Nimegundua: katika kaya hii ni haamu na haamu ni haai, nimeamua nivute bangi lau inibangue niwatoee uvivu mafisadi wetu. Juzi tiiambiwa na huyu jamaa mwenye majina yaiyopinda pinda eti siikai imeshindwa kuwakamata mafisi na mafisadi? Eti wataipua nchi! Kama anadhani tu wapumbavu titaiipua wenyewe tilioibiwa. Ebo, kazi ya siikai ni nini? Je, kazi ya usaama wa taifa aikotokea jamaa ni nini? Je, kazi ya mkuu ni nini?"

Mbwa Mwitu anamkatisha. "Hee Mgosi unahoji utadhani pilato! Mbona ya kupeleka mamluki Zimbabwe huitaji? Kweli hii kaya inaendeshwa kimshumaa! Yetu yanatushinda tunafakamia ya wengine!"


"Mbwa niache. Yaani kaya inavyonajisiwa unategemea kwei nikoshe la kusema hata kuaaani?" Anajibu Mgosi kwa huzuni na mawazo kibao kuona kaya yake inavyogugunwa na mibaka na mifisi na mafisadi. “We acha tu ingekuwa zamani ningeenda Ushoto kutafuta tungui na kuwamaizia mbai.”

Makengeza ambaye alikuwa amejiinamia kwa simanzi anaonekana hakupenda kinachoendelea.

Anakatua mic. "Mgosi mbona kama ni ufisadi kushindikana hili si siri wala jipya?” Mgosi anakatua mic bila kungoja Makengeza aendelee kujinoma na mic. “Siongeei ufisadi tiliozoea. Naongea hii biioni 155 tiiyoambiwa iliibiwa na Meemetameta na Tunituni.”

Makengeza. “Unataka kuniambia zaidi ya ile bilioni 133 ya EPA na milioni 365 tunayowalipa akina Richmond kwa mwaka kuna tena bilioni 155.” Machungi. “Kumbe sasa? We unaishi nchi gani ndugu yangu au na umepofuka kama ndugu zetu wa Butiama?” He mbona Tunituni na Lwasha wamevunja rekodi kwa wizi! Tena umenikumbusha. Umeiona taarifa ya katibu wa Mchonga Sam Kasorisori kwa vyombo vya habari?

Machungi anatikisa kichwa kuonyesha hajainyaka. Makengeza anaendelea. “Mzee kaamua kuweka mambo hadharani. Nimeinyaka Bwana. Kumbe Mchonga aliposema jamaa alikuwa amejilimbikizia mali nyingi za wizi haikuwa vijembe!

Jamaa anasema: “Lwasha alipobanwa na Mchonga akahofia angeukosa ubunge hivyo akataka eti Mchonga aende kwa kina Ole kumsafisha!”

Mara Mpemba anaingilia: “Huyu mpuuzi kweli. Yaani Nchonga ende kujivua salawili kwa ajili ya jizi moja?”

“Kama ulikuwapo Ami!” Anasema Makengeza huku akitabasamu na kuendelea. “Bwana we. Nasikia Mchonga aliendewa na rafiki yake mzee Rashidu baada ya jamaa kumtaka amtetee. Mchonga alitaka viitishwe vijiwe vya chama amsafishe kwa sharti Lwaasha awepo. Kwanza kabla ya hapo eti alimwambia katibu wake amwambie mzee Rashidu wa Lioni kuwa asiwe mjinga.”

Anainua kombe lake na kulipiga busu na kuendelea. “Jamaa anasema hadi Mchonga anarudisha namba alikuwa bado hajajibiwa swali lake kuu la ni kwanini kijana mdogo mwenye miaka kiduchu kwenye utumishi wa umma alikuwa na mimali kuliko yeye tena bigi wa Kaya?”

Anakatua kashata na kupiga tama kama mbili, tatu za kahawa.

Kabla ya kuendelea mara Mkurupukaji analamba mic. “Enhe na ikawaje?"

“Kijana tuliza boli wakubwa tukupe vitu.” Anasema Makengeza huku akijifuta jasho na kuendelea. “Nasikia mambo yalikuwa mazito. Mchonga alitaka wakutane wajumbe wa kamati na halmashauri kubwa popote kwa gharama yoyote angelipa yeye ili ‘amsafishe’ Lwaasha kwa sharti kuwa Lwaasha awepo. Enhee nilisahau. Kwanza aliwaita kwake Msasani mzee Rashidu na Lwaasha mwenyewe, lakini Lwaasha aliishia mitini. Nasikia aliposikia kichwa maji Tunituni kamteua kwenye genge lake la ulaji aliguna na kushangaa akajua alivyoukanyaga mkenge kwa kumuunga mkono kibaka.”

Kabla ya Makengeza kuendelea, mzee Ndomo anakumbushia: “Jamani mada ya leo ni kujadili ni kwanini jamaa ameshindwa kuwanyaka na kuwasulubu majambazi wa EPA?”

“Kweli hii ndiyo mada ya leo ingawa na taarifa ya mjumbe ni muhimu.” Anaingilia msomi huku akijikuna kichwa kutafuta mapwenti na kuendelea. “Kimsingi wanaodhani jamaa anaweza kuwakamata wenzake wanakosea sana. Nani amkamate nani iwapo hatujui nani ni nani katika hili?”

“Msomi umefumba sana na kuniacha nje,” analalama mzee Maneno. “Pole sana mzee wangu.” Anasema Msomi akitabasamu.

Anaendelea. “Nimaanishacho: tunamuuliza kambale kama ana masharubu. Siku zote nawaambia institutional corruption sorry uoza wa kimfumo. Ukiona sirikali inakiri imeshindwa mafisadi jua nayo ni fisadi na haina maana wala haki ya kuendelea kutawala. “Res clamat domino ad dominum” au mali humlilia mwenyewe. Mwenye mali nani? Naomba niwaulize swali. Hivi Yuda na Pilato nani hakuwa na dhambi? Acha niulize jingine. Hivi nguruwe na ngiri wana uhusiano gani? Hilo nalo naliacha. Je, ni ngamia gani amuue nundu kisa eti ana nundu?" Mzee Ndomo anaonekana kutoelewa kabisa.

Analalamika.“Msomi leo kusema ukweli umeamua kutufumba. Unataka kuniambia jamaa ana nundu kubwa kuliko jamaa wa EPA?”

“Ewaaa! Sasa kumbe?” Anajibu Msomi huku akikatua kitumbua chake.

Anaendelea. “Mfano Lwaasha alivyopigwa buti na kuletewa wa kupinda, watu walikenua wasijue ni wale wale! Nenda wizara ya serikali za shambani na mitaani ukaulizie jamaa kaacha harufu kiasi gani? Hata huko uhasama wa taifa alipokuwa si salama. Sana sana hawa ndio wamekuwa vinara wa kulinda uoza tunaouona na kuhangaishwa nao.

Akiwa anajiandaa kuendelea, kinokia chake kinalia. Anapokea na kuongea kwa haraka na kuendelea: “Jamaa yangu wa intelligence ananitaarifu sasa hivi kuwa jamaa yetu mmoja amehojiwa na usalama wa taifa!” “Nani huyo?” anauliza Mkurupukaji. “Si yule Enderea kuchenga.” Anajibu Msomi.

“Aaa! Kwa amri ya nani? Kama ni Cheka cheka, usanii. Kwanini alinteua kwenye genge lake la ulaji baada ya sie kumpinga? Hapa ni kufungana kamba tu kupitisha nnda,” alilalamika Mpemba.

Msomi anaendelea: “Iwe kweli iwe geresha ipo siku watawajibika. Leo nimeudhika naongea Kilatini samahanini. Upo msemo kuwa vita vivenda non vitanda, yaani maisha ni kuyaishi siyo kuyaepuka. Hivyo wanaokwepa au kutia zengwe kwenye kupambana na ufisadi ipo siku yatawarudia wanayofanya, watake wasitake, tulale tuamke au vinginevyo. Na isitoshe si kila siku ni Jumapili.”

Kabla ya kuendelea, mzee Maneno anachomekea. “Kweli Walatini kiboko; kumbe kwao maisha ni vita na kutoyaishi ni vitanda! Ndiyo maana waligundua salsafa.”

“Falsafa mzee siyo salsafa.” Anakosoa Mbwa Mwitu. Kijiwe hakina mbavu kwa wanavyokosoana na kutafsiri mambo.

Msomi hajali anaendelea. “Ukitaka kujua Kaya ilivyoishiwa hasa kimkakati na uongozi angalia wanavyoanza kuvuana nguo hata kwenye kijiwe cha Idodomya. Kuna nini pale? Angalia walivyompiga stop jamaa yao kutoka Iran. Siku si nyingi kilichomtoa nyoka miguu kitathibitika tena dhahiri. Hatuwezi kuendelea na upuuzi huu ambapo mibaka michache inataifisha kaya yetu sisi tukifa kwa ulofa. Si karne ya 21.”

Akiwa anajiandaa kumwaga falsafa, wale vibaka migambo ya Kondoro si walivamia wakitafuta ubwabwa wa kupelekea wake zao. Tulitimka wasitutie adabu, tukaamua kujibu na kunyotoa mtu roho. Ipo siku, ipo siku, ipo siku tutaanzisha mambo yetu yaleeeee, mtayajua wakati huo.


Source: Tanzania Daima Machi 16, 2008

No comments: